Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu
Hassan amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Simiyu kuwa Serikali
itamaliza kabisa tatizo la uhaba wa dawa za kuuwa wadudu waharibifu wa
zao la pamba.
Mhe. Makamu wa Rais ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wananchi
wa Wilaya ya Busega kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya
Lamadi wakati akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake Mkoani Simiyu.
Amesema awamu ya kwanza ya dawa zimeshafika Simiyu kwa ajili ya
kuwagawia wakulima wa pamba na akaahidi kuwa awamu ya pili ya kuleta
dawa hizo inamalizika katika wiki inayoanza leo tarehe 19/02/2018, hivyo
tatizo hilo litakuwa limekwisha.
“Ninajua kuna kiasi kikubwa cha dawa kinakuja Simiyu dawa itakuwa
nyingi na wakulima wote watapata, hatuwezi kuacha nguvu zenu zipotee
bure na kwa kuwa Simiyu ni mkoa wa Viwanda na ndiyo unazalisha pamba kwa
wingi tutajenga viwanda vinavyotumia pamba, kwa maana hiyo hatuwezi
kuiacha pamba iharibike” alisema.
Katika hatua nyingine Mhe.Makamu wa Rais wakati akizungumza na
wananchi katika Kijiji cha Masanzakona baada kuweka jiwe la msingi
mradi wa maji wa Kiloleli amewahimiza wananchi kuchangia huduma za maji
ili miradi ya maji iwe endelevu.
Amesema Serikali imedhamiria kumaliza kabisa tatizo la maji hapa
nchini kwa kujenga miradi ya maji hivyo ni vema wananchi wakaunga mkono
juhudi za Serikali kwa kuchangia huduma za maji ili kusaidia miradi
hiyo kujiendesha.
Akiwasilisha taarifa ya mradi wa Kiloleli kwa Makamu wa Rais,
Mhandisi wa Maji Wilaya ya Busega, Mohammed Said amesema mradi huo
utagharimu jumla ya shilingi bilioni 1.6 mpaka kukamilika kwake mwezi
Machi 2018 na utawahudumia wananchi wa vijiji vitatu vya Yitwimila B,
Ihale na Ijitu.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Busega, Mbunge wa
Busega Mhe. Raphael Chegeni amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli kwa kutekeleza ahadi aliyoitoa kwa
wananchi wakati wa ziara yake mkoani Simiyu ya kuwapelekea mradi wa
Maji wananchi wa kata ya Kiloleli.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu
Hassan ameanza ziara ya kikazi ya siku nne(04) mkoani Simiyu, ambapo
amepata fursa ya kuzungumza na wananchi pamoja na kukagua miradi
mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya ya Busega na Bariadi.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment