Naibu waziri wa viwanda na biashara Exaud Kigahe akiangalia ubora wa mbao zinazozalishwa katika kiwanda cha Sao Hill
Naibu waziri wa viwanda na biashara Exaud Kigahe akiangalia ubora wa mbao zinazozalishwa katika kiwanda cha Sao Hill
Na Fredy Mgunda,Iringa.
NAIBU waziri wa viwanda na
biashara Exaud Kigahe amevitaka viwanda vinavyozalisha nguzo za umeme
kuhakikisha wanazalisha nguzo zenye ubora unaotakiwa ili kuiondolea serikali
hasara ya kununua nguzo hizo mara kwa mara.
Akizungumza wakati wa ziara
aliyoifanya kwenye kiwanda cha kuzalisha nguzo za umeme cha Sao Hill kilichopo
wilayani Mufindi, Kigahe alisema kuwa kumekuwa na baadhi ya
viwanda ambavyo vimekuwa havizalishi nguzo zenye ubora na kuipatia hasara
serikali.
Alisema kwenye uzalishaji wa
nguzo kumekuwa na baadhi ya wazalishaji wa nguzo ambao hawaweki vizuri dawa ya
kutibia nguzo na kusababisha kuharibika kwa nguzo haraka sana tofauti na
makadilio ya serikali ya nguzo moja kuishi kwa zaidi ya miaka hamsini.
“Unakuta nguzo imekaa miaka
mitatu tu imeharibika na inaanguka kutokana na kuzalishwa chini ya kiwango
kutoka katika kiwanda ambacho kimezalisha nguzo na hasara hiyo inaenda moja kwa
moja kwa serikali na sio kwao”alisema Kigahe
Kigahe alisema kuwa TBS
wanapaswa kuanza kufuatilia ubora wa nguzo zinazozalishwa kwenye viwanda
ambavyo sio waadilifu katika kuzalisha nguzo hizo za umeme ambao zimekua
zikiharibika mara kwa mara.
Aidha Kigae aliwataka wanunuzi
wa nguzo kutoka kwa wakulima wa bidhaa hiyo kuhakikisha wananunua kwa bei
inayotakiwa na kuacha mara moja tabia ya kuwanyonya wakulima wa nguzo hizo.
Alisisitiza kuwa serikali
inapaswa kununua nguzo za umeme ambazo zinakidhi viwango vya TBS ili kuepukana
na kupata harasa ambayo wamekuwa wanaipata pasipokuwa na sababu ya msingi.
Naibu waziri wa viwanda na
biashara Exaud Kigahe aliwaponge viongozi wa kiwanda cha Sao Hill kwa kuzalisha
nguzo zenye ubora unaotakiwa ambapo nguzo zao zinauwezo kwa kukaa ardhini kwa
zaidi ya miaka hamsini.
Kwa upande wake mwenyekiti wa
wazalishaji wa nguzo nyanda za juu kusini Negro Sanga alisema kuwa kumekuwa na
unyonyaji kwa baadhi ya kampuni kwa kununua nguzo kwa gharama ndogo na kuiuzia
serikali kwa gharama kubwa nguzo hizo.
Alisema kuwa kila kampuni
imekuwa na bei yake inayojiamulia kiasi kwamba inakuwa inawanyonya wakulima wa
nguzo hizo zinapoka shambani hadi kufika kiwandani.
Naye meneja wa kiwanda cha Sao
Hill George Bottger alisema kuwa lengo la kiwanda hicho ni kuhakikisha
wanazalisha nguzo zilizo bora na zenye viwango vinavyotakiwa kimataifa kwa
lengo la kuiondolea hasra serikali ambayo imekuwa inaipata kutoka katika
viwanda vingine.
0 comments:
Post a Comment