(Na Jovina Bujulu, MAELEZO)
Hivi
karibuni Serikali imetangaza kununua ndege nne katika kipindi cha mwaka
huu wa fedha kwa ajili ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ili
kuimarisha sekta ya usafiri wa anga hapa nchini zitakazogharimu Dola za
Kimarekani milioni 46.
Serikali
kwa kuanzia imetoa asilimia 40 ambazo ni sawa shilingi bilioni
39,937,939,200 kwa ajili ya ununuzi wa ndege mbili za awali .ambazo
zimelipwa Kampuni ya Bombadier Inc ya nchini Canada.
Azma
hiyo ya Serikali ya kununua ndege mpya inatokana na ahadi za Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kutaka
kufufua Shirika la Ndege Tanzania na kulipatia mtaji ili lianze upya
kutoa huduma hiyo kwa Watanzania.
Ujio
wa ndege hizo utaimarisha huduma za usafiri wa anga na kuongeza
ushindani katika utoaji wa huduma za anga hapa nchini kati yake na
kampuni binafsi za ndege zinazotoa huduma hiyo kwa sasa.
Mara
baada ya ndege hizo kuwasili hapa nchini zitaanza kutoa huduma ya
usafiri wa anga hapa nchini kabla ya kupanua wigo wake wa utoaji wa
huduma katika ngazi ya ukanda wa Afrika Mashariki na baadaye katika
anga.nyingine za Kimataifa.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (MB)
aliwasilisha Bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha
hivi karibuni alisema kuwa Shirika la ATCL lina ndege moja aina ya Dash
8-Q300 na ndege ya kukodi aina ya CRJ 200.
“Kwa
sasa ATCL ina ndege moja na ndege nyingine ni ya kukodi ambazo
zinawezeshwa na Serikali kutoa huduma za usafiri wa anga kati ya Dar es
salaam, Mwanza, Mtwara, Kigoma na Moroni Comoro” alisema Profesa
Mbarawa.
Aidha,
Prof. Mbarawa aliongeza kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na kampuni ya
ATCL na wadau wengine imekwishaainisha ndege mbili zinazofaa
kununuliwa ambazo zitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 78 na baadaye
ndege nyingine mbili kubwa zitakazokuwa na uwezo wa kubeba abiria 155
ambazo zitanunuliwa kwa kipindi cha mwaka huo fedha.
Mchakato
wa ununuzi wa ndege hizo mbili ambazo zitanunuliwa katika awamu ya
kwanza ulihusisha wawakilishi wa viwanda vya ndege vya Boeing ya
Marekani, Airbus ya Ufaransa, Embraer ya Brazil na Bombadier ya Canada.
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani
alisema kuwa ndege hizo ambazo zinatarajiwa kununuliwa zitatumia anga la
Tanzania ambapo hivi sasa anga hilo linatumiwa na ndege zinazotoka nje
ya Afrika, hivyo upatikanaji wa ndege hizo utasaidia kutoa fursa kutua
kwenye anga za nchi jirani.
“Muda
si mrefu tutapata ndege mbili mpya, mwakani tutaongeza nyingine mbili,
Serikali imejipanga kufufua Shirika la Ndege na kubadilisha mfumo wa
uendeshaji ili liweze kujiendesha lenyewe” alisema Mhandisi Ngonyani.
Kwa
mujibu wa Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
(Mawasiliano) William Budoya , amesema kuwa msukumo wa kununua ndege
hizo ni jambo la muda mrefu kuanzia Serikali ya Awamu wa Nne
2005-2015,na katika kuendeleza utekelezaji wa juhudi hizo Serikali ya
Awamu ya Tano imetoa msisitizo na kulipa kipaumbele suala hilo.
Aidha,
Afisa Mawasiliano huyo amesema kuwa ndege zitakazonunuliwa ni aina ya
Bombadier kutoka kampuni ya Bombadier Inc ya nchini Canada.
Serikali
ilichagua kampuni ya Bombadier Inc kwa sababu iliainisha mchanganuo wa
biashara ambao ulishauri kuanza na ndege ndogo, kwa kuangalia soko la
ndani baadaye ndege zinaweza kuongezwa kwa kuangalia soko la kimataifa.
Aliongeza
kwa ndege hizo zinatarajia kufika nchini ifikapo mwezi Septemba mwaka
huu, na kwa kuanzia zitaanza kutoa huduma kwa safari za ndani ya nchi.
Aidha
alisema kuwa Serikali imemteua mshauri mwelekezi ambaye ataweka
manejimenti imara katika uendeshaji ikiwa ni pamoja na kuajiri
wafanyakazi walio na weledi na wenye utayari wa kufanya kazi kwa
ufanisi.
Shirika
la ndege la Tanzania (ATC) lilianzishwa mwezi Machi, 1977 chini ya
sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1969 na baada ya kuvunjwa kwa
lililokuwa Shirika la ndege la Afrika Mashariki.
Katika
kutekeleza sera ya ubinafsishaji na ushirikishwaji wa sekta binafsi
katika uendeshaji wa Mashirika ya Umma ya mwaka 2002, Shirika la ndege
la Tanzania (ATC) liliundwa upya huku Serikali ikimiliki asilimia 49
ya hisa zake kwa Shirika la ndege la Afrika Kusini hatua ambayo
ilipelekea kuundwa upya kwa kampuni ya ndege Tanzania (ATCL).
Pamoja
na kuwepo kwa kampuni ya ndege ya ATCL, kwa sasa kuna kampuni binafsi
zinazojihusisha na huduma za usafiri wa anga nchini na nje ya
nchi.Kampuni hizo ni Precision Air, Fastjet, Auric na Coastal Air.
Akizungumzia
mpango wa Serikali wa kukabiliana na changamoto ambazo zimekuwa
zikiikabili kampuni ya ATCL , Budoya alisema kuwa mshauri mwelekezi
aliyeteuliwa na Serikali atatayarisha mpango madhubuti wa kibiashara
utakaoifanya kampuni ya ATCL kujiendesha kwa faida na kuweza kuteka soko
la ndani na nje ya nchi.
0 comments:
Post a Comment