METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, February 3, 2021

RC KUNENGE ATOA ONYO KWA WALIOTOBOA BOMBA LA KUSAFIRISHA MAFUTA KIGAMBONI, AVIELEKEZA VYOMBO VYA DOLA KUWASAKA WAHUSIKA

Kamati ya Usalama Mkoa wa Dar es salaam ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Aboubakar Kunenge ikiambatana na Watendaji wa Mamlaka ya Bandari na Wadau wa Kampuni za Mafuta leo February 03 wametembelea na kujionea uharibifu wa miundombinu ya kusafirisha Mafuta yanayoshushwa kwenye meli kwenda nchi kavu ambapo Mkuu wa Mkoa huo ametoa onyo kwa waliohusika kufanya uharibifu huo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo RC Kunenge ameelekeza Kamati ya usalama Mkoa huo kuhakikisha wote waliohusika na hujuma hiyo wanakamatwa Mara moja na kuchukuliwa hatua Kali za kisheria kwakuwa kitendo walichofanya ni sawa na uhujumu uchumi.

RC Kunenge amesema kitendo Cha kutoboa Bomba hilo kinahatarisha usalama wa wananchi kwakuwa inaweza kusababisha Mlipuko lakini pia Mafuta yanayomwagika baharini yanaleta uchafuzi wa mazingira.

Aidha RC Kunenge amesema mbali na kuhatarisha usalama pia inasababisha Serikali kukosa Mapato, kusababisha uhaba wa Mafuta na pia kupoteza ubora wa Mafuta.

Pamoja na hayo RC Kunenge ameonyesha kuridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Mamlaka ya Bandari ikiwemo ya Kuanza kuchukuwa hatua ya kufunga mfumo wa kuonyesha eneo lenye hitilafu na kutoa taarifa pamoja na kuimarisha ulinzi Katika eneo hilo.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam Lazaro Mambosasa amesema wamejipanga kuhakikisha wanaanza msako wa pamoja na wanaamini watawatia mbaroni watu wote waliofanya hujuma hiyo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com