Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda amelitaka Shirika la Maji Safi na Maji Taka DAWASCO kuhakikisha linashughulikia kero zote za maji kwa Wananchi ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na kupatia ufumbuzi tatizo la Maji Taka yanayotiririka holela kwenye makazi ya watu.
RC Makonda ametoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Maji ambapo amesema tatizo la maji taka limekuwa kero sugu katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo jambo linalohatarisha hata Afya za wananchi.
Aidha RC Makonda ameitaka DAWASCO kuongeza jitihada za kufikisha huduma ya maji kwa wananchi ili kuenda sambamba na sera ya Serikali ya awamu ya Tano ya kumtua mama ndoo kichwani.
Hata hivyo RC Makonda ametoa wito kwa watumishi wa DAWASCO wanaokwenda kusoma mita kwa wananchi kuwa na lugha nzuri kwa wananchi pamoja na kushughulikia kero ya wananchi kubambikiziwa kiwango kikubwa cha malipo ya bili za maji.
Kuhusu changamoto ya upotevu wa maji RC Makonda amelitaka shirika hilo kulipatia majibu ya haraka tatizo hilo ili kiasi cha maji yanayopotea kiweze kuwahudumia wananchi.
Ili kufikisha huduma ya maji kwa maeneo yenye changamoto RC Makonda amejitolea kuchimba visima 50 vya maji ambapo amewasihi Wenyeviti wa mitaa hiyo kuainisha maeneo ya kuchimba visima hivyo.
Pamoja na hayo RC Makonda ametaka uwepo wa ushirikiano wa kikazi baina ya TANROAD, TANESCO, TARURA na DAWASCO ili kumaliza changamoto ya kukatwa kwa miundombinu ya maji wakati wa ujenzi wa barabara pamoja na uharibifu wa barabara.
0 comments:
Post a Comment