METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, March 14, 2019

MHE BASHUNGWA AZINDUA TEKNOLOJIA ZA KILIMO HIFADHI SHADIDI ENDELEVU KWENYE MSETO WA MAZAO YA MAHINDI NA MIKUNDE




                       
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo

Pamoja na umuhimu wa mazao Mseto ya Mahindi na Mikunde kwa usalama wa chakula na kipato kwa wananchi, lakini uzalishaji wa mahindi bado ni mdogo , yaani wastani wa gunia 5 za mahindi kwa ekari, na gunia 1 mpaka 2 za mbaazi au maharagwe zenye uzito wa kilo mia mia kwa ekari katika mfumo wa kilimo mseto wa mazao hayo.

Mavuno hayo madogo yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiiko ya tabia nchi, uhamishaji (mining) wa rutuba ya udongo kwa miaka mingi, mmomonyoko wa udongo, kutokutumia mbegu bora zinazostahimili mvua chache, kutokuzingatia kanuni za kilimo bora, ukosefu wa ardhi kushindwa kuhifadhi unyevu kwa muda mrefu, magonjwa na visumbufu vya mimea na kutokuwepo na masoko ya uhakika.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa (Mb) wakati wa uzinduzi wa teknolojia za kilimo hifadhi shadidi endelevu kwenye mseto wa mazao ya mahindi na mikunde katika ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru, Jijini Arusha jana tarehe 13 machi 2019.

Bashungwa alisema kuwa lengo kuu la Mradi huo wa SIMLESA ni kuwasaidia wakulima kuzalisha zaidi na hivyo kuwa na uhakika wa chakula, lishe bora, kuongeza kipato ili kuondokana na umaskini pamoja na kuzingatia hifadhi ya ardhi na mazingira ambapo utekelezaji wake uliambatana pia na matumizi ya mbinu za kilimo hifadhi.

Lengo lingine la mkutano huu ni kuwakutanisha wadau wa kutoka sekta za umma na binafsi pamoja na wadau wa maendeleo ili kujadili na kupanga mikakati ya kusambaza teknolojia ya kilimo hifadhi shadidi endelevu kwa wakulima wengi katika maeneo mengi ili waweze kuongeza uzalishaji, uhakika wa chakula na kipato na hatimaye kuboresha maisha yao.

Sambamba na hayo, Bashungwa alisema kuwa Mradi wa SIMLESA umetekelezwa kwa kushirikiana na wadau hususani wakulima na maafisa ugani. Katika jitihada hizo, Mradi umegundua teknolojia ya Kilimo Hifadhi Shadidi Endelevu (CASI) katika mseto  wa mahindi na mikunde. CASI imethibitisha kuwa ni teknolojia inayoongeza tija, inaokoa muda (save time), inaboresha hali ya afya ya udongo, ni teknolojia rafiki na ni njia ya kukabiliana (coping) na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.

“Pamoja na mafanikio hayo, katika mazingira ya sasa na tukizingatia sera ya Serikali yetu ya Awamu ya Tano inavyotilia mkazo Ujenzi wa uchumi wa viwanda ili kufikia uchumi wa kati, kuna umuhimu mkubwa wa kushirikisha wabia mbalimbali katika kusambaza teknolojia hizo ili manufaa yake yaweze kuwafikia idadi kubwa ya wanufaikaji hasa wakulima wetu” Alikaririwa Mhe Bashungwa

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com