Wanawake wamepewa wito wa kushiriki katika nafasi za uongozi katika Vyama vya Ushirika hususani Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) nchini pindi nafasi hizo zinapojitokeza.
Wito huo umetolewa na Naibu
Mrajis wa Vyama vya Ushirika kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Bw. Charles
Malunde alipokuwa akifungua Kongamano la Wanawake kuelekea maadhimisho ya Siku
ya Kimataifa ya Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo. Maadhimisho yaliyoanza
tarehe Oktoba 12, 2020 na kilele chake kufanyika Oktoba 15, 2020 Jijini Arusha.
Naibu Mrajis amesema Ushirika
nchini umekuwa chachu ya maendeleo katika kuhakikisha kuwa makundi ya watu wa
kipato cha chini na maskini katika jamii wanakuwa na chombo cha kuaminika cha
kuwawezesha kufikia malengo yao ya kiuchumi na kijamii.
Aliongeza kuwa licha ya
ushirika nchini kuendelea kushamiri katika sekta mbalimbali za kiuchumi na
Vyama kujiendesha kwa kufuata Misingi ya Ushirika kimataifa bado kuna
changamoto katika sekta ya Ushirika katika masuala yanayohusu jinsia na nafasi
ya mwanamke katika uongozi wa vyama vya Ushirika.
“Ushiriki wa wanawake katika
sekta ya Ushirika umekuwa kidogo sana hivyo hali hii ikiendelea kuwa hivi
itapelekea kutokuwa na uendelevu katika shughuli za kiushirika katika miaka
ijayo. Kukosekana kwa chombo cha kitaifa cha kuwaunganisha wanawake katika
sekta ya Ushirika kunapelekea kukosa uwakilishi katika anga za kimataifa na
kukosa fursa za kimaendeleo,” alisema Naibu Mrajis
Akifafanua suala la nafasi ya uongozi kwa wanawake Naibu huyo alisema katika kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika shughuli za ushirika nchini. Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na wadau wengine itahakikisha kuwa uhamasishaji unaendelea kunafanyika ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika Vyama vya Ushirika vikiwepo Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo kwa kuwatengenezea mazingira rafiki ikiwemo kuwa na chombo cha kitaifa kitakachoratibu na kusimamia masuala ya Wanawake kwa kuwa na idara au dawati la wanawake kwa kila chama cha ushirika nchini.
Bw. Malunde alieleza
Kongamano hilo kuwa utayari na kujiamini kwa Wanawake wajasiriamali katika
kukopa nako ni sehemu ya changamoto zilizopo katika Vyama vya Akiba na Mikopo.
Akitolea mfano Katika utafiti uliochapishwa na shirika la kazi duniani (ILO)
mwaka 2014 unaonyesha kuwa zaidi ya 80% ya maombi ya mikopo ilitengwa kwa ajili
ya wajasiriamali wanawake na 90% iliiva kwa ajili ya kuwapatia wanawake, lakini
ni 18% ya wanawake wajasiriamali ndio walioomba mikopo hiyo na 28% walioomba
katika taasisi nyinginezo za kifedha.
“Takwimu zinaashiria kuwa sio
tatizo la kuwepo kwa fedha isipokuwa ni masuala mengine kama vile riba na
masharti magumu kama chanzo kikuu cha wanawake kushindwa kukopa,” alieleza
Naibu Mrajis Malunde
Kwa Upande wake Makamu
Mwenyekiti wa Muungano wa Vyama vya Akiba na Mikopo nchini (SCCULT) Somoe
Nguhwe katika Kongamano hilo amewataka Viongozi wanawake katika Vyama vya Akiba
na Mikopo kutumia nafasi zao za uongozi kuhamasisha, kutoa elimu na fursa za
kuwaandaa wasichana kuwa viongozi. Makamu huyo alisistiza kwamba ni muhimu
Wanawake kuingia kwenye Uongozi kwani nafasi ya Mwanamke kwenye jamii ni kubwa
na muhimu hususani kama mlezi na msingi wa familia, Jamii na Taifa kwa ujumla.
Kongamano hilo limehudhuriwa
na Wanawake kutoka maeneo mbalimbali nchini ikiwemo mikoa ya Dar es salaam,
Mbeya, Arusha, Kilimanjaro, Kagera, Iringa na Mbeya. Kongamano hilo
limedhamiria kuwajengea uwezo Wanawake katika masuala mbalimbali ikiwemo
uongozi pamoja na kubadilishana mawazo ili kuongeza tija na ufanisi katika
Vyama vyao vya Ushirika.
0 comments:
Post a Comment