METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, October 21, 2020

JUKUMU LETU NI KUPIGA KURA NA KUILINDA AMANI

Anaandika Patrick Myovela

Ni siku nane tu ndizo zilizobakia, kabla  ya Watanzania  hawajafanya maamuzi ya  kumchagua Rais, wabunge na madiwani watakao waongoza Watanzania wenzao  kwa muhula wa kuanzia mwaka 2020 hadi 2025. Mpaka sasa sera za wagombea wote kwa nafasi ya Urais, wabunge na madiwani zimekwisha elezwa kwa kiasi cha kutosha kwa umma wa Watanzania na kuwaacha wakiendelea kufanya tafakuri itakayowaongoza kufanya maamuzi sahihi pasi na kukosea ifikapo tarehe 28.10.2020.

Kwanza kabisa makala yangu leo hii imejikita kwenye eneo la kuwataka Watanzania wote wenye sifa ya kupiga kura, kujitokeza kwa wingi tarehe 28.10.2020 kwenda kupiga kura kwa lengo la kutimiza haki yao ya kimsingi na ya kikatiba ya kuwachagua  viongozi walio sahihi na wenye tija kwa Taifa hili.  Katika hili kila Mtanzania  popote alipo ndani ya nchi hii anawajibu wa kumkumbusha Mtanzania mwenzake mwenye sifa hiyo kutokufanya kosa la kuacha kupiga kura wakati ukifika.

Msisitizo katika hili uende sambamba na vyombo vya  usalama kuhakikisha kuwa wazee wote na kina mama wanapewa ulinzi wa kutosha  siku hiyo ya tarehe 28.10.2020 ili wawe huru kutoka majumbani na kwenda kupiga kura pasi na kupata manyanyaso na vitisho vyovyote.

 Nayasema haya kwasababu kwa baadhi ya  chaguzi zilizopita kumekuwa na kundi la vijana wa vyama fulani fulani kujihusisha na tabia za kutoa vitisho kwa wazee na kina mama ili kuwanyima fursa hiyo adhimu ya kushiriki  kwenye kufanya maamuzi sahihi kupitia boksi la kura.

Jambo la pili ni la kuwataka Watanzania wenzangu kuendelea kukumbuka kauli za viongozi wakuu wa nchi hii juu ya suala la kulinda na kudumisha amani ya Taifa hili.

Ninaposema jukumu letu ni kupiga na kulinda amani nina maanisha kuwa kila mmoja kwa nafasi yake ayabeze na kuyaepuka kabisa maneno ama kauli zinazotoka midomoni mwa baadhi ya wagombea, zenye kuwataka kulinda kura zao baada ya uchaguzi.

Kauli hizi zimekuwa zikiwahimiza hasa vijana kutokuondoka eneo la vituo vya kupigia kura kwa kile kinachoitwa kulinda kura.
Ndugu zangu Watanzania na hasa kwa wale wenye sifa za kupiga kura, ni lazima tuelewe kuwa mantiki ya kuwa na mawakala wa uchaguzi kutoka vyama mbalimbali vya kisiasa lililenga kwenye maana hii ya kulinda kura za wagombea. Sasa tujiulize unapotaka kuwa na kundi la vijana nje ya kituo cha kupigia kura kwa muda wote kwa madai ya kulinda kura nini hasa kinachotafutwa?

Nchi nyingi duniani na hasa katika bara la Afrika zimekubwa na matukio mengi ya uvunjifu wa amani yatokanayo na miongozo batili na mibovu ya baadhi ya viongozi wa vyama vya kisiasa. Na katika hili mara nyingi vijana ndiyo wamekuwa wakitumika vibaya kuanzisha machafuko huku wakisahau kuwa kuna kundi kubwa la wazee, walemavu, kina mama na watoto wanaoweza kuwa waathirika wakubwa pindi machafuko yanapotokea.

Mifano ya nchi zilizopata madhara ya kudumu yatokanayo na uvunjifu wa amani tunayo na bado tutaendelea kuzisikia zikiendelea kudumu katika machafuko hayo.

Ni mtanzania gani asiyejua machafuko yaliyowapata wenzetu wa jirani kama Kenya, Rwanda, Burundi na Rwanda kutokana na uvunjifu wa amani utokanao na chokochoko zinazopandikizwa na watu wabaya kwenye kipindi cha uchaguzi mkuu? Hima watanzania wenzangu tuwe makini sana na kauli za baadhi ya viongozi wa vyama vya kisiasa zisizoitakia mema nchi yetu ya Tanzania. Na kwa sisi vijana, kubwa kwetu iwe kuhimizana juu ya suala la kulinda amani ya nchi yetu ili tuweze kuendelea kuijenga nchi yetu kwa faida ya sasa na ya vizazi vijavyo.

Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, ndicho kipindi mahususi cha sisi wakazi halali wa maeneo yetu katika nyumba, mitaa, vijiji, kata na kadhalika kuhakikisha kuwa tunakuwa makini kuwabaini wageni wote tunaowatilia mashaka kwa kuwa na ukazi usio sahihi. Hii itasaidia sana kubaini pia wachochezi wa uvunjifu wa amani katika maeneo yetu.

Mwisho nitoe rai kwa mabalozi wa nyumba kumi kumi kuwa makini katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu kwa kutambua wakazi halali wa maeneo wanayo yasimamia ili kuepukana na hatari ya kuishi na maadui wasio na huruma na nchi yetu. Ni wazi kabisa kuwa kupitia kwao taarifa sahihi za nani kaja ama nani kaondoka katika maeneo yao zitapatikana ili kuyaweka maeneo yetu salama.

Wamiliki wa nyumba za wageni kadhalika nao wanajukumu la kuhakikisha kuwa wanatambua mienendo ya wageni wao wanaofika katika maeneo yao na kutoa taarifa sahihi na rafiki kwa vyombo vya usalama ili kutoruhusu mwanya wa watenda maovu kuweza kusambaza sumu zenye viashiria vya uvunjifu wa amani.

Jukumu letu kama Watanzania ni kuuvaa uzalendo wenye kiwango kikubwa cha kuto waonea haya wale wote wenye tabia za ushawishi mbaya kwa vijana na kuwatumia kama chambo kwa uvunjifu wa amani.

Vijana wenzangu kabla ya kuingizwa kwenye mkenge na wale wanaodai tulinde kura zetu, kwanza kabisa tugeuke nyuma na kuwaangalia babu, bibi ,baba, mama, dada na wadogo zetu na kujiuliza swali moja tu. Nini hatma yao baada ya machafuko kutokea?

Tunatakiwa kupiga kura na kuilinda AMANI
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com