METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, July 20, 2018

DKT TIZEBA AITAKA (TASTA) KUPUNGUZA GHARAMA ZA MBEGU

Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye sherehe za Siku ya Kilimo Biashara kwa wadau wa kilimo iliyofanyika kwa pamoja na Taasisi ya utafiti wa Kilimo TARI-SERIAN na Baraza la nafaka Ukanda wa Afrika ya Mashariki (EAGC) katika viwanja vya Serian mjini Arusha, Jana tarehe 20 Julai 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-WK)
Baadhi ya wakilima wakifatilia hotuba ya Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba wakati akihutubia kwenye sherehe za Siku ya Kilimo Biashara kwa wadau wa kilimo iliyofanyika katika viwanja vya Serian mjini Arusha, Jana tarehe 20 Julai 2018.
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akizungumza na wafanyabiashara wa mazao mbalimbali alipowatembelea kwenye banda la mafunzo wakati wa sherehe za Siku ya Kilimo Biashara kwa wadau wa kilimo iliyofanyika kwa pamoja na Taasisi ya utafiti wa Kilimo TARI-SERIAN na Baraza la nafaka Ukanda wa Afrika ya Mashariki (EAGC) katika viwanja vya Serian mjini Arusha, Jana tarehe 20 Julai 2018.
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye sherehe za Siku ya Kilimo Biashara kwa wadau wa kilimo katika viwanja vya Serian mjini Arusha, Jana tarehe 20 Julai 2018.
Mtafiti Mkuu wa kituo cha utafiti wa kilimo SERIAN Dkt John Saria akimueleza Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba umuhimu wa mashine ya kupandia Mahindi, Maharage, Alizeti, na Mbaazi kwenye sherehe za Siku ya Kilimo Biashara kwa wadau wa kilimo iliyofanyika katika viwanja vya Serian mjini Arusha, Jana tarehe 20 Julai 2018. 

Na Mathias Canal, Arusha

Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba ameiagiza Taasisi ya udhibiti wa Ubora wa mbegu (TOSCI) kukutana na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa mbegu Tanzania (Tanzania Seed Trade Association-TASTA) leo 21 Julai 2018 ili kujadili namna ya kupunguza gharama za uuzaji wa mbegu jambo litakaloongeza tija na unafuu wa bei kwa wakulima.

Waziri Tizeba ametoa agizo hilo Jana tarehe 20 Julai 2018 wakati akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye sherehe za Siku ya Kilimo Biashara kwa wadau wa kilimo iliyofanyika kwa pamoja na Taasisi ya utafiti wa Kilimo TARI-SERIAN na Baraza la nafaka Ukanda wa Afrika ya Mashariki (EAGC) katika viwanja vya Serian mjini Arusha.

Agizo hilo linajili Mara baada ya wakulima kulalamika mbele ya Waziri huyo wa kilimo kuhusu gharama za mbegu kuwa juu mara baada ya kupata fursa ya kuuliza maswali katika mkutano huo ambapo pamoja na mambo mengine wananchi hao walimpongeza Mhe Tizeba kwa maagizo hayo.

"Nimemuona hapa Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mbegu Tanzania (TASTA) Bwana Bobu Shuma akijaribu kuhalalisha bei ya mbegu kwamba ni rafiki kwa wakulima wetu siwezi kukubaliana naye na haiwezekani serikali imefuta kodi zote kwenye mbegu lakini wakulima bado wanatozwa kiasi kikubwa cha fedha hivyo ni lazima mpunguze bei" Alisisitiza Mhe Tizeba

Aliongeza kuwa endapo wafanyabiashara hao watashindwa kupunguza bei serikali itarejesha kodi zote kwenye mbegu ama kuwafutia leseni baadhi ya wafanyabiashara watakaoshindwa kufuata na kutekeleza maagizo ya serikali  .

"Natoa Siku moja kuanzia sasa mpaka kesho jioni (Leo) kwa TOSCI na TASTA mkutane mjadiliane majibu mnipatie kabla sijaondoka Arusha kwamba mmepunguza gharama za mbegu mkishindwa kufanya hivyo mtakuwa mmekiuka matakwa ya utaratibu wa serikali" Alikaririwa Mhe Tizeba

Katika hatua nyingine Mhe Tizeba amewasihi wafanyabiashara wa mbegu nchini kuuza mbegu zinazozalishwa nchini badala ya kushadadia mbegu zinazozalishwa nje ya nchi huku akiongeza kuwa sio lazima kila mzalishaji wa mbegu azalishe mbegu za nje kwani kufanya hivyo kunawanufaisha wamiliki wa lebo za mbegu hizo kilimo na kuongeza faida kubwa kwa nchi zingine.

Sambamba na hayo Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba ameiagiza Taasisi ya udhibiti wa Ubora wa mbegu (TOSCI) kufanya utafiti wa mara kwa mara ili kujiridhisha kama mbegu zinazotolewa kwa wakulima ni sahihi ama vinginevyo.

Aidha, ameushukuru uongozi na wataalamu wa utafiti SERIAN, uongozi wa wafanyakazi wa Baraza la Nafaka Ukanda wa Afrika ya Mashariki, uongozi na watumishi wa makampuni ya pembejeo kama SEEDCO, Zambia, ETG, PANNAR, KIBO, MERU, SYGENTA, MONSANTO, SUBA AGRO, MAMS, EAST WEST SEED, Kampuni ya mbolea YARA na ETG kwa kushiriki kikamilifu kuonyesha aina za mbegu zenye Mazao mengi.

Katika maonesho hayo mbegu za maharage, Mahindi, soya, Ngano, shairi, mbaazi, aliseti na mazao ya mbogamboga zilionyeshwa huku wananchi wakipata fursa ya kujifunza mbinu bora za kilimo ikiwa ni pamoja na kuunganisha uelewa wa pamoja na wataalamu wa mazao hayo

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com