METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, July 20, 2018

TIJA KWENYE KILIMO NI KUUZA KUPITIA MFUMO RASMI (USHIRIKA)-DKT TIZEBA

Waziri wa kilimo Dkt Charles Tizeba akisisitiza umuhimu wa ushirika kwenye sherehe za siku ya kilimo biashara kwa wadau wa kilimo inayofanywa kwa pamoja na Taasisi ya utafiti wa kilimo TARI-SERIAN na baraza la nafaka Ukanda wa Afrika Mashariki (EAGC) katika viwanja wa Taasisi ya utafiti SERIAN Mjini Arusha jana tarehe 20 Julai 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-WK)
Waziri wa kilimo Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo mara baada ya kutembelea shamba la maonesho ya mahindi kwenye sherehe za siku ya kilimo biashara kwa wadau wa kilimo iliyofanyika jana jana tarehe 20 Julai 2018 katika viwanja wa Taasisi ya utafiti SERIAN Mjini Arusha.
Waziri wa kilimo Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo mara baada ya kutembelea shamba la maonesho ya vitunguu kwenye sherehe za siku ya kilimo biashara kwa wadau wa kilimo iliyofanyika jana jana tarehe 20 Julai 2018 katika viwanja wa Taasisi ya utafiti SERIAN Mjini Arusha.
Waziri wa kilimo Dkt Charles Tizeba akisisitiza umuhimu wa ushirika kwenye sherehe za siku ya kilimo biashara kwa wadau wa kilimo inayofanywa kwa pamoja na Taasisi ya utafiti wa kilimo TARI-SERIAN na baraza la nafaka Ukanda wa Afrika Mashariki (EAGC) katika viwanja wa Taasisi ya utafiti SERIAN Mjini Arusha jana tarehe 20 Julai 2018.
Waziri wa kilimo Dkt Charles Tizeba akiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu EAGC, Mtendaji Muu wa TARI, Mawakala wa pembejeo za kilimo, Watafiti na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Arusha mara baada ya kuhutubia mamia ya wananchi kwenye sherehe za siku ya kilimo biashara kwa wadau wa kilimo katika viwanja wa Taasisi ya utafiti SERIAN Mjini Arusha jana tarehe 20 Julai 2018.

Na Mathias Canal-WK, Arusha

USHIRIKA ni dhana ya kuleta maendeleo kwa kushirikiana, Dhana hii imefanikiwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, Kutokana na changamoto mbalimbali zilizoikumba sekta hii ya ushirika watu wengi walikosa imani na vyama hivyo kutokana na viongozi wake kutokuwa waaminifu (Wabadhilifu).

Ni wazi kuwa katika kipindi cha miaka miwili hivi, imani kwa vyama vya ushirika imeongezeka na vyama vingi vinaendelea kuundwa hasa vile vya kuweka na kukopa, yaani SACCOS.

Waziri wa kilimo Dkt Charles Tizeba ameyasema hayo jana 20 Julai 2018 wakati wa hotuba yake katika siku ya kilimo biashara kwa wadau wa kilimo inayofanywa kwa pamoja na Taasisi ya utafiti wa kilimo TARI-SERIAN na baraza la nafaka Ukanda wa Afrika Mashariki (EAGC).

Alisema kuwa uanzishwaji wa vyama vingi vya ushirika kwa sasa unatokana na elimu watu wengi waliyoipata kuhusu Ushirika na watu kuendelea kuelewa kuwa changamoto zilizoko ndani ya ushirika zinatatulika ikiwa ni pamoja na hivi karibuni kutangaza kiama kwa baadhi ya viongozi wabadhilifu wa vyama hivyo ambao wanautumia ushirika kama sehemu ya kujinufaisha wao pasina kuwa na mtazamo wa mafanikio kwa wanachama wote.

Alisema, Dhamira ya Ushirika ni nzuri na kama itafanya kazi vizuri ni njia nzuri ya kuleta mabadiliko kwa watu wengi huku akisisitiza Wanachama wa Ushirika kujiimarisha katika misingi ya uaminifu, uwazi, uwajibikaji kwa jamii na kuwajali wengine.

Dkt Tizeba alisema Ushirika ni muungano wa watu ambao wanafanya kazi pamoja kwa hiari ili kufanikisha mahitaji yao ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kupitia shughuli ya biashara inayomilikiwa kwa pamoja na kudhibitiwa kidemokrasia kwani njia pekee yenye tija na mafanikio ya kilimo kwa mkulima ni kuuza mazao yao kupitia mfumo huo rasmi wa ushirika.

“Kupitia ushirika kutamfanya mkulima kujihami na bei kwa kuuza kwa pamoja kwani kwa muda mrefu kilimo cha masoko kimekuwa kikitengenezwa na wakulima wenyewekwa sababu ya kutojiunga pamoja na kuwa na mfumo rasmi” Alikaririwa Dkt tizeba na kuongeza kuwa

“Kunapokuwa na chama imara cha Msingi, chama hiki kinaunda chama kikuu kilicho imara kwa kufanya hivyo tutaondokana na uduni wa bei kwa mkulima kutokana na kushuka bei kwa mazao kwa sababu ya mkulima mmoja mmoja kuuza mazao yake mwenyewe” Alisema

Waziri huyo wa kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba alisema Serikali imeamua kufufua ushirika kwa sababu ndiyo mkombozi wa wakulima. "Tumeamua kurudisha ushirika aminifu kwa wakulima, na nirudie kutoa onyo kwa viongozi waliopata dhamana ya kuongoza ushirika wasidhani kule wameenda kupata ulaji.” Alisema

Alisema kuwa pamoja na kwamba serikali inatambua kuwa ushirika ni nyenzo muhimu ya kuwasaidia wananchi katika upatikanaji wa mtaji na kuwawezesha kuunganisha nguvu zao za katika kujiendeleza kiuchumi lakini kuongezwa somo la ushirika kwenye mtaala wa elimu italeta mageuzi makubwa kwa wakulima.

Alisema kuwa pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanahamasishwa na hatimae kujiunga kwenye vyama vya ushirika kulingana na shughuli zao za kiuchumi ili kuondoa dhana  ya kudhani kwamba vyama vya ushirika ni kwa ajili ya Kilimo cha Mazao ya biashara ya nchi za nje lakini juhudi hizo zitakuwa na mabadiliko chanya zaidi kama ushirika utafundishwa mashuleni.

MWISHO.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com