Ni miaka minne tangu Sheria ya Huduma za Habari
Namba 12 ya Mwaka 2016 imepitishwa nchini na Bunge mnamo Novemba 5, 2016 na
kusainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli
Novemba 16 mwaka huo huo.
Miongoni mwa matakwa ya sheria hiyo ambayo
yameainishwa kuisimamia na kuiboresha tasnia ya habari na kuifanya kuwa taaluma
kamili ili iheshimike kama taaluma nyingine ni hatua kuingiza kipengele cha
kiwango cha elimu, hatua itakayowasidia kuongeza weledi katika utendaji kazi
wanataaluma hao.
Kifungu cha 67(b) cha Sheria ya Huduma za
Habari Namba 12 ya Mwaka 2016 kikisomwa kwa pamoja na Kanuni ya 17(20(a) ya
Kanuni za Sheria ya Huduma za Habari, 2017 vinawataka wanahabari wote
kujiendeleza na kuwa na sifa ya kitaaluma ya angalau Stashahada (Diploma) ndani
ya kipindi cha miaka mitano baada ya kuanza kwa Sheria hiyo iliyoanza kutumika
rasmi nchini Desemba 31, 2016.
Akiwasilisha Bungeni Hotuba ya Makadirio ya
Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2020/2021 Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa kipindi cha miaka mitano
cha mpito kinakwisha mwezi Desemba 2021 ni vema wanataaluma hao wajiendeleze
wapate sifa za kitaaluma kwa kiwango kilichoainishwa kisheria ili waweze
kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria hiyo.
“Natumia nafasi hii kuwapongeza wengi
walioitikia wito na ambao kwa sasa wanajiendeleza au wameshamaliza masomo yao,
natoa wito kwa waandishi wa habari nchini ambao bado hawajajiendeleza kielimu
kukidhi matakwa ya sheria wafanye hivyo ili waweze kuendelea na kazi ya
uandishi wa habari baada ya muda huu wa mpito kuisha” alisisitiza Dkt.
Mwakyembe.
Hakika imebaki miezi 20 kwa wanataaluma ambao
bado hawajaanza kujiendeleza kielimu, sasa ni muda muafaka kufanya hivyo ili
kupata sifa za kuwa mwanataaluma kamili wa habari.
Sheria ya Huduma za Habari imekuja wakati
muafaka ambapo imekuwa ni hatua muhimu kwa tasnia ya habari kwa kuihamisha
taaluma ya hiyo kutoka fani ambayo mtu yeyote anaweza kujinasibu nayo hadi kuwa
taaluma kamili yenye sifa mahsusi, maadili yanayojulikana pamoja na vyombo vya
kusaidia kusimamia utekelezaji wake ikiwemo Bodi ya Ithibati na Baraza Huru la
Vyombo vya Habari.
Idara ya Habari (MAELEZO), inasimamia na
kuratibu shughuli za Serikali upande wa habari. Katika kutekeleza majukumu
yake, Idara hiyo imegawanyika katika sehemu tatu ambazo ni Sehemu ya Ukusanyaji
na Usambazaji wa Habari, Usajili wa Magazeti na Mawasiliano Serikalini ambapo
kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari Namba 12 ya Mwaka 2016 kifungu cha 4
(1) Mkurugenzi wa Idara ya Habari ndiye msimamizi mkuu wa Idara hiyo.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara hiyo, sehemu ya
Usajili wa Magazeti, Patrick Kipangula
amebainisha kuwa utekelezaji wa sheria hiyo unaenda vizuri hatua
inayoonesha kuwa kuna mwitikio mkubwa wa waandishi wa habari kujiendeleza
kielimu.
Aidha, amesema kuwa sehemu hiyo ya Idara ndiyo
yenye mamlaka ya kutoa vitambulisho vya waandishi wa habari (Press Card) ambapo
kuanzia mwezi Januari hadi Aprili 2020 vitambulisho vya wanahabari 638
vimetolewa na kati yao takribani asilimia 80 ya vitambulisho hivyo vya
waaandishi wana sifa na wana kiwango cha elimu kinachotakiwa kwa mujibu wa
sheria yaani Stashahada katika tasnia ya habari.
Aidha, Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa
Afrika (MISA-TAN) ikiwa mdau muhimu wa tasnia ya habari nchini ambayo miongoni
mwa malengo yake makuu ni kukuza, kuboresha na kuleta utofauti wa utendaji kazi
wa vyombo vya habari vikiongozwa na weledi katika utendaji kazi wao kwa
kuzingatia taaluma ya habari ikiwemo kiwango cha elimu.
Akizungumzia hotuba ya Waziri mwenye dhamana ya
habari aliyoitoa Bungeni jijini Dodoma hivi karibuni, Mwenyekiti wa MISA-TAN
nchini Salome Kitomari amesema kuwa tangu sheria hiyo imepitishwa na kufanya
kazi nchini, taasisi hiyo imekuwa ikitoa mafunzo na kuwasisitiza waandishi wa
habari kujiendeleza kielimu ambapo kwa upande wao wamekuwa wakitoa mafunzo
mbalimbali kuhusu sheria zinazosimamia taaluma hiyo.
“Wapo ambao walitusikia na kufuata matakwa hayo
ya kisheria na sasa wamemaliza vyuo vikuu na wengine wamemaliza diploma, lakini
kuna ambao wapo katika hatua mbalimbali ikiwemo kumalizia masomo yao katika
vyuo walivyojiunga kusoma” alisema Kitomari.
Aidha, Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa waandishi
wa habari nchini kutimiza takwa hilo la kisheria kwani imeshakuwa sheria tayari
na haina mbadala, hivyo lazima kila mwandishi wa habari ambaye atapenda kufanya
kazi hiyo awe na elimu angalau kiwango cha Stashahada katika tasnia ya habari.
Zaidi ya hayo, amesema kuwa muda ulioainishwa
kwa maana ya muda wa mpito uliotolewa kisheria unakaribia kuisha kwani muda huo
ulishatolewa tangu Desemba 31, 2016 na ukomo wake ni Desemba 31, 2021.
“Napenda kuwaambia waandishi wa habari
wenzangu, kama kweli unaipenda kazi yako ya uandishi wa habari, nenda darasani
ukasome ule wakati wa ujanja ujanja na kufanya mambo mbalimbali yaende
umekwisha, sasa hivi ni wakati wa kuhakikisha una cheti chako kwa sababu
itafikia wakati kama huna cheti hata ‘Press Card’ hutapata” amesisitiza
Kitomari.
Kwa upande wa usajili wa wanachama wa MISA-TAN,
Mwenyekiti huyo amesema kuwa taasisi hiyo ina wanachama wa zamani ambao
wamekuwa wakihimiza kila mara kujiendeleza kielimu na ikitokea kunapata na
kupokea wanachama wapya ambao bado wanaendelea na masomo wanawasisitiza
kumalizia masomo yao ili waweze kuwa na sifa stahiki zilizoainishwa kisheria.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 17 inayofafanua Sheria
ya Huduma za Habari Na. 12 ya 2016 imebainisha kuwa mtu mwenye sifa ya kupata
ithibati ya kuwa mwandishi wa habari ni pamoja na wahariri wa habari, waandishi
wa habari, watangazaji, waandishi wa habari wa kujitegemea, wapiga picha,
watayarishaji wa habari na watangazaji wa redio na runinga wanaofanya kazi
katika vyumba vya habari, watu waliofanya kazi ya kutukuka katika tasnia ya
habari pamoja na mtu mwenye shahada yoyote ambaye lazima awe na stashahada ya
tasnia ya habari.
0 comments:
Post a Comment