Muonekano wa chumba cha upasuaji
katika kituo cha afya Bunda mjini baada ya kuboreshwa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa gharama ya
shilingi milioni 500 kwa kujengewa majengo mapya na vifaa tiba vya kisasa.
Sehemu ya
majengo ya kituo cha Afya
Bunda mjini mkoani Mara baada ya kuboreshwa na kuanza kutoa huduma za
upasuaji kwa wananchi wa mji huo na maeneo ya jirani.
Utoaji wa huduma za Afya umeboreshwa baada
ya Serikali kutoa milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Bunda,
mkoani Mara.
Baadhi ya wakazi wa Bunda wameipongeza
Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwaboreshea na kuwasogezea huduma za afya hivyo
kuwaondolea adha walizokuwa wakizipata kabla ya hatua hiyo ya Serikali.
Mkazi wa Kijiji cha Nyasula, Elizabeth
Madimanya amesema kuwa Kituo kinatoa huduma nzuri na mandhari ya hospitali ni
nzuri.
Naye Rehema Malila, mkazi wa Kijeti, Bunda
ametoa pongezi kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John
Pombe Magufuli kwa kuboresha huduma za afya.
“Zamani tulikuwa tunahangaika kupata huduma
za afya mbali sana na kwetu hadi mtoto wangu alifia tumboni kwa kukosa huduma
ya karibu, Kituo kinatoa huduma nzuri, watumishi ni wazuri, utadhani wote ni
wachaMungu”, alisema Malila.
Kituo cha Afya Bunda kimekuwa msaada mkubwa
kwa wakazi wa maeneo hayo ambao walikuwa wanafuata huduma za afya umbali mrefu
zaidi ya kilomita 17.
Muuguzi Kiongozi wa Kituo hicho, Dorcas
Makaya anasema Kituo cha Afya Bunda kinahudumia takriban akina mama watano kwa
siku kwa ajili ya huduma za kujifungua. Anaelezea kuwa wanajitahidi kuwahudumia
wananchi kwani dawa na vifaa tiba vinapatikana kwa uhakika.
“Nawashukuru viongozi wa Halmashauri ya
Bunda Mji kwa ushirikiano wanaotupatia kiasi kwamba tunatoa huduma bila
wasiwasi, pia namshukuru Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa kutujengea Kituo
hiki”, anaongeza Makaya.
Kituo hicho baada ya ujenzi wake
kukamilika, kilianza kutoa huduma moja kwa moja baada ya Halmashauri ya Bunda
kupata vifaa vya hospitali hiyo kutoka kwa wahisani toka nje.
“Hatukusubiri Serikali kutuletea vifaa
ilibidi tujiongeze wenyewe kwa kuwasiliana na wahisani toka nje ili huduma
zianze”, anaeleza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bunda Mji, Janeth Mayanja.
Kwa mujibu wa Mayanja Kituo hicho kimekuwa
msaada mkubwa kwa wakazi wa Bunda Mjini na maeneo ya jirani kwa kusogeza huduma
za afya karibu.
Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria
kuboresha huduma za afya kwa kujenga zaidi ya vituo vya afya 362, hospitali za
wilaya 67 ambazo hivi karibuni zimeagizwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
TAMISEMI, Suleiman Jafo kuanza kutoa huduma mara moja baada ya kukamilika
ujenzi wake.
Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa akisikika akisema kuwa Serikali yake
imejipanga kuboresha huduma za afya kwa kuongeza bajeti ya Dawa na vifaa tiba
kutoka Shilingi bilioni 31 hadi bilioni 270.
“Tumeajiri watumishi wa kada mbalimbali za
11,152, tumejenga nyumba za watumishi 306 na pia tumeboreshana kuimarisha
huduma za kibingwa katika Hospitali yetu ya Taifa Muhimbili na Hospitali za
Rufaa za Bugando, KCMC na Mbeya. Hivi sasa watu toka nchi jirani wanakuja
nchini kupata matibabu ya magonjwa ya moyo, figo,kansa, mifupa ubongo na
kadhalika”, anasema Rais Magufuli.
Hakika huduma za afya zimeboreshwa na
kusogezwa karibu na wananchi hivyo kuwaongezea matumaini ya kuishi wakiwa na
afya bora. Karibu wilaya zote hapa nchini licha ya kuwa na hospitali za wilaya,
vituo vya afya na zahanati vimejengwa na vingine kuboreshwa.
0 comments:
Post a Comment