Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa barabara
za kiwango cha lami katika mji wa Serikali utakaogharimu zaidi ya bilioni 89
ikiwa ni ahadi aliyotoa mara baada ya kutangaza Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi
ili kutekeleza tamko alilolitoa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka
1973 zaidi ya miongo mine iliyopita.
Akizungumza leo Jijini Dodoma wakati
akiweka jiwe la msingi la mradi huo na baadae kuzindua jengo la Ofisi za Wakala
wa barabara Mijini na Vijijini (TARURA) alisema wakala huo umetekeleza majukumu
yake kwa ufanisi na kuwataka kuongeza kasi zaidi.
“Ujenzi wa barabara hii utakua na njia
nne zenye urefu wa km 11.2, njia mbili zenye urefu wa km 28, njia za waenda kwa
miguu, njia za baiskeli na limetengwa eneo la huduma za kijamii,”
“Dodoma ni mji unaokua vizuri, kuna
miradi mikubwa iliyokwishatekelezwa na inayotarajiwa kutekelezwa ikiwemo ujenzi
wa barabara ya mzunguko ya njia nne yenye urefu wa km 110 itakayogharimu zaidi
ya shilingi bilioni 600 na ujenzi wa Uwanja wa Ndege mkubwa utakaogharimu
shilingi bilioni 500” alisisitiza Rais Dkt. Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli alitoa tahadhari
kwa TARURA kutumia fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara na sio
kuendelea kujenga ofisi zingine katika wilaya mbalimbali nchini na badala yake
watumie majengo ya Serikali katika mikoa na wailaya mbalimbali nchini.
Vilevile, Taasisi za Serikali
zimetakiwa kujenga majengo yake badala ya kuendelea kulipa pango katika majengo
ya kukodi, na ameitaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kumaliza ujenzi
wa jengo lake hapa jijini Dodoma kabla
ya mwaka 2020 kumalizika.
Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa Bodi
ya Wakurugenzi ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) imeidhinisha dola za Marekani
milioni 14.3 za msamaha wa kodi ya madeni ambayo nchi ilikuwa ikidaiwa na
kutaja sababu ya msamaha huo kuwa nchi imefanikiwa kupambana vizuri dhidi ya
ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid-19) unaosababishwa na virusi vya Corona.
“Kwa niaba ya watanzania nitamuandikia
barua Mkurugenzi Mkuu wa IMF kumpongeza kwa kutambua juhudi zetu na fedha
hizi tutazitumia vizuri katika kupambana na ugonjwa huu pamoja na kushughulikia
mambo mengine yakayosaidia ugonjwa huu usije tena” alisisitiza Rais Magufuli
Wakati
huo huo,
Rais Magufuli amekabidhi pikipiki kwa Maafisa Tarafa kwa lengo la kutatua
changamoto ya usafiri iliyokuwa ikiwakwamisha katika kusimamia utekelezaji wa
miradi mbalimbali katika maeneo yao.
“Nilitoa kiasi cha shilingi bilioni 1
kwa ajili ya kununua pikipiki hizi, zimepatikana pikipiki 448 na Maafisa
Tarafa ni 570 nchi nzima, hivyo natumaini hakuna Ofisa Tarafa atakayekuwa
hana pikipiki kwani kuna waliogawiwa zamani, watakaoharibu ama kupoteza
watazilipa” alisisitiza Rais Magufuli.
Akizungumzia kuhusu ugonjwa wa corona,
Rais Magufuli ameitaka Wizara ya Afya kukiendeleza Kitengo cha Tiba Asili
kuendelezwa sambamba na kuongeza bajeti yake, na kuwataka wanaotengeneza dawa
za asili kutodharauliwa.
“Corona bado haijaisha lakini imepungua
sana, hivyo tuendelee kuchukua tahadhari, watu waliodhani tutafariki wengi
wameshindwa. Mungu wetu anatupenda na tuendelee kumtegemea yeye” aliongeza Rais
Magufuli.
Katika
hatua nyingine, Rais Magufuli wakati wa ufunguzi wa jengo la Makao Makuu ya Jeshi
la Zimamoto na Uokoaji amesema kuwa moja ya changamoto zilizokuwa zikilikabili
Jeshi hilo ni upandishwaji wa vyeo kwani waliokuwa juu hawakujali wa chini,
hali iliyosababisha tuchukue hatua kwa kuwapandisha vyeo Makamanda 889.
Tunawahakikishia tutaendelea kuwapandisha kadri itakavyowezekana.
Akizungumzia utendaji wa Jeshi hilo,
Rais Magufuli amesema kuwa ameshatoa maagizo kwa Taasisi ya Nyumbu kushirikiana na Jeshi hili kuanza kutengeneza
magari ya zimamoto nchini.
“Kulikuwa na mapendekezo ya Makamishna
wanne wa jeshi hili kushushwa vyeo au kufukuzwa kazi lakini kwa kuwa mmefanya
marekebisho ya kutosha nimewasamehe, hata aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Jeshi,
Thobias Andengenye nimemsamehe lakini nitampangia kazi nyingine,”alisisitiza
Rais Magufuli.
Aidha, ametoa wito kwa Viongozi wa
Manispaa, Majiji na Wizara ya Ardhi kuhakikisha wanawaelimisha watu kuwa katika
kila jengo itengenezwe njia zitakazotumiwa na jeshi hili mara yanapotokea
majanga ya moto.
Kwa kutambua umuhimu wa jeshi Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji, Rais ameahidi kuwaunga mkono kwa kuwapa shilingi bilioni 5
ndani ya wiki hii ili kutatua changamoto ya makazi ikizingatiwa tayari jeshi
hilo limetafuta eneo la kujenga makazi ya familia 80.
Kwa
upande wake, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John
Masunga alimshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwapa kiasi cha shilingi
bilioni 2,656,146,300 kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Jeshi hilo jijini
Dodoma.
Aidha, Jeshi hilo limepata mafanikio katika kukabiliana na
matukio ya moto 6,398 na maokozi 2,663 yalishughulikiwa kuanzia mwaka 2015/2016
hadi 2019/2020 ambapo maeneo 319,389 na vyombo vya moto 17,740 vimekaguliwa ili
kuimarisha hali ya usalama wa wananchi na mali zao.
0 comments:
Post a Comment