Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Uwekezaji), Jenista Mhagama (kushoto)
akisalimiana na baadhi ya Makamanda Waandamizi wa Jeshi la Magerza nchini
wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa mradi wa kiwanda cha Ngozi cha
Karanga kinachojengwa kwa Ubia baina ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa
Watumishi wa Umma (PSSSF) na Gereza la Karanga lilolopo Moshi Mkoani
Kilimanjaro. Ziara hiyo ya Waziri Mhagama ilifanyika jana Jumatano Januari
15, 2020.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,
Bunge, Kazi, Ajira na Uwekezaji) Jenista Mhagama (katikati) akitoa
maelekezo kwa watendaji mbalimbali wakiwemo Makamanda Waandamizi wa Jeshi
la Magereza Nchini wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa mradi wa
kiwanda cha Ngozi cha Karanga kinachojengwa kwa Ubia baina ya Mfuko wa
Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Gereza la Karanga
lilolopo Moshi Mkoani Kilimanjaro. Ziara hiyo ya Waziri Mhagama ilifanyika
jana Jumatano Januari 15, 2020.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira,
Vijana na Watu Wenye Ulemavu) Jenista Mhagama amesema Serikali haijaridhika na kasi
ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Karanga katika
Gereza la Karanga Mkoani Kilimananjaro na kumtaka mkandarasi kuikamlisha kazi hiyo
kabla ya tarehe 2 Februari mwaka huu.
Akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi
huo jana (Jumatano Januari 15, 2020), Waziri Mhagama alisema hakuna sababu kwa
mradi huo unaotekelezwa kwa ubia baina ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa
Watumishi wa Umma (PSSSF) na Gereza la Karanga, kutokamilika kwa wakati kwani
fedha zote zilizohitajika katika hatua muhimu za mradi huo zimekwishatolewa.
Kwa mujibu wa Waziri Mhagama alisema kiwanda
hicho ni miongoni mwa miradi muhimu ya kimkakati iliyopangwa kutekelezwa na
Serikali ya Awamu ya Tano, hivyo mkandarasi hana budi kuzingatia masharti ya
mkataba uliowekwa ili kuhakikisha kuwa kiwanda hicho kinakamilika kwa wakati na
kuweka kuleta tija iliyokusudiwa.
‘’Sijaridhishwa na kasi ya ujenzi wa
mradi huu, na nitoe maagizo kwa Jeshi la Magereza linalosimamia ujenzi wa mradi
huu kuhakikisha kuwa kunakuwepo na vifaa, vitendea kazi na wataalamu wa kutosha
katika maeneo yote ya ujenzi ili kuhakikisha kuwa tarehe 2 Februari mwaka huu
mradi huu unakamilika na baadhi ya mashine zinaanza kusimikwa’’ alisema Waziri
Mhagama.
Aidha Waziri Mhagama alisema iwapo
mradi wa ujenzi innaonekana ni mkubwa, Serikali itawaruhusu wakandarasi mbadala
ikiwemo Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Shirika la Mzinga, na Jeshi la
Kujenga Taifa (JKT), kuifanya kazi hiyo ili kukamilika kwa wakati na muda
uliopangwa kwani Serikali kupitia kiwanda hicho imekusudia kutengeneza ajira na
mapato ya fedha za kigeni.
Akifafanua zaidi Waziri Mhagama
alisema mwishoni mwa wiki hii Ofisi yake inatarajia kupokea mashine za mradi
huo na kuzikagua, hivyo ni wajibu wa mkandarasi wa mradi kuongeza kasi ya
ujenzi wa mradi huo kwa kuwa Serikali kupitia PSSSF kwa upande wake imetekeleza
wajibu wake kwa kutoa fedha zilizohitajika hadi kufikia hatua iliyopo.
Waziri Mhagama pia alizitaka taasisi
zote zinazohusika katika mradi huo ikiwemo PSSSF, Shirika la Maendeleo ya
Utafiti wa Viwanda Tanzania (TIRDO) pamoja na Jeshi la Magereza Nchini kusimamia
kwa ukamilifu vifungu vya kitaalamu ili kuufanya mradi huo ukamilike kwa
wakati, kwani Serikali haipo tayari kulipa fidia ya gharama za usimakaji wa
mashine ikisubiri kukamilishwa kwa ujenzi wa kiwanda hicho.
Kwa upande Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Jeshi la Magereza Nchini, Hamis Nkubasi alisema Jeshi hilo
limepokea maelekezo yote ya Serikali na imejipanga kuhakikisha kuwa mradi huo
unakamilika kwa wakati ili kuweza kufikia malengo yaliyowekwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Hosea Kashimba alisema
hadi sasa Ofisi yake imetoa kiasi cha Tsh Milioni 200 zilizotumika kwa ajili ya
ununuzi wa malighafi zote muhimu zilizohitajika katika hatua mbalimbali za
ujenzi wa mradi huo.
Alisema kuwa Ofisi yake imejipanga
kuhakikisha kuwa itatekeleza maelekezo yote yatakayolewa na Serikali na yanayohitajika
kwa mkandarasi ili kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika katika muda na wakati
uliopangwa kwa mujibu wa Mkataba.
0 comments:
Post a Comment