
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akifafanua jambo wakati
alipokwenda kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya
Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro unaosimamiwa na Shirika la
Nyumba la Taifa (NHC) jana

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua jalada la ardhi katika
ofisi ya ardhi ya halmashauri ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro jana
wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi. Kulia
ni Afisa Ardhi Mteule wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Jacob Muumba.

Mhandisi anayesimamia ujenzi wa
jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro kutoka
Shirika la Nyumba la Taifa Peter Mwaisabura akimueleza Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula Maendeleo ya
Ujenzi wa Ofisi hiyo jana wakati Naibu Waziri alipofanya ziara kukagua
mradi huo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akioongozana na Mkuu wa Wilaya
ya Hai mkoani Kilimanjaro Lengai Ole Sabaya kuelekea kukagua jengo la
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara yake
ya siku moja katika wilaya hiyo kukagua miradi inayosimamiwa na Shirika
la Nyumba la Taifa (NHC).(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
*****************************
Na Munir Shemweta, WANMM HAI
Naibu Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameagiza
ofisi ya Ardhi Kanda ya Kaskazini kuwatambua wamiliki 2,019 wa maeneo
katika halmashauri ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro ambao hawataki
kumilikishwa maeneo yao na kupatiwa hati.
Agizo hilo
linafuatia Dkt Mabula kuelezwa na Afisa Ardhi Mteule wa Halmashauri hiyo
Jacob Muumba kuwa pamoja na halmashauri hiyo kupima viwanja 2,019
lakini wamiliki wake hawajajitokeza kumilikishwa jambo lililomstua
Naibu Waziri wa Ardhi.
‘’Watu wana maeneo lakini hawataki kumilikishwa, wanakwepa kitu gani maana hawalipi kodi’’ alisema Dkt Mabula.
Naibu Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameagiza wale wote wenye maeneo
yaliyopimwa katika halmashauri ya wilaya ya Hai kutambuliwa na
kujulikana wanamiliki maeneo yao toka muda gani na kusisistiza kuwa
hakuna atakayeachwa na zitaangaliwa hatua za kuchukua.
Katika hatua
nyingine Dkt Mabula ameagiza kufuatiliwa kwa maeneo yote ya biashara ya
hamashauri ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro ambayo hayalipiwi kodi ya
pango la ardhi ili yaweze kulipiwa.
Alisema,
pamoja na halmashauri hiyo kuwa na maeneo ya kibiashara yaliyopimwa kama
vile Stendi na Soko lakini hakuna hata eneo moja lililolipiwa kodi ya
pango la ardhi hivyo basi Mkurugenzi wa halmashauri lazima ahakikishe
analipia maeneo yake ya biashara.
‘’DED wa Hai
hujawahi kulipia kodi ya pango la ardhi ya Stendi na Soko wakati
vimepimwa na kama halamashauri hailipi je mtu wa kawaida itakuaje?
alihoji Dkt Mabula.
Hata hivyo,
Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya aliagiza kupatiwa taarifa ya
maandishi kuhusiana na halmashauri ya wilaya ya Hai kushindwa kulipia
kodi ya pango la ardhi katika maeneo yake ya biashara na kumuahidi Naibu
Waziri Mabula kuwa atalifanyia kazi suala hilo katika kipindi cha muda
mfupi pamoja na lile la wamiliki wa maeneo wasiotaka kumilikishwa.
Hata hivyo, Ole
Sabaya alimueleza Dkt Mabula kuwa pamoja na changamoto mbalimbali katika
sekta ya ardhi wilayani humo Ofisi yake kwa kushirikiana na idara ya
ardhi imeweza kuzipatia ufumbuzi kero za ardhi za wananchi wa wilaya
hiyo zipatazo 350 kati ya 432 zilizowasilishwa wakati wa siku maalum ya
ardhi maarufu kama Ardhi Day.
Wakti huo
huo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline
Mabula amekagua ujenzi wa mradi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Hai
mkoani Kilimanjaro unaojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na
kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa ofisi hiyo ambapo alilitaka
Shirika la Nyumba kukamilisha ujenzi katika muda uliopangwa.
Kwa mujibu wa
Kaimu Meneja wa Shirika la Nyumba mkoa wa Kilimanjaro Mradi huo
unaogharimu takriban shilingi milioni 910 unatarajiwa kukamilika Desemba
mwaka 2019.
0 comments:
Post a Comment