Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya
Bunge ya Katiba na Sheria akiongoza kikao cha kamati hiyo kilicholenga
upokeaji wa taarifa ya utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya vijana,
kilichofanyika Oktoba 25, 2019 katika Ofisi za Bunge, Jijini Dodoma.
(Kulia) ni Stanslaus Kagisa (Mb).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
Mhe. Jenista Mhagama akizungumza katika kikao cha Kamati ya Bunge ya
Katiba na Sheria ambapo Ofisi yake ilikuwa ikiwasilisha utekelezaji wa
Mfuko wa Maendeleo ya vijana. (Kulia) ni Mhe. Jackline Msongozi (Mb).
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana
Bw. James Kajugusi akiwasilisha mada kuhusu mfuko wa Maendeleo ya Vijana
wakati wa kikao hicho.
Wajumbe wa Kamati ya Katiba na
Sheria wakiwa kwenye kikao cha kamati hiyo wakipokea taarifa ya
utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, kilichofanyika katika Ofisi
za Bunge, Jijini Dodoma.
Mwakilishi wa Kiwanda cha Chaki
cha Maswa, Bw. Kelvin Steven akitoa shuhuda kwa wajumbe wa kamati ya
kudumu ya Katiba na Sheria kuhusu mafanikio ya kiwanda hicho
kilichonufaika na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Mwakilishi wa Kampuni ya Vijana ya
JATU SACCOS Ltd, Bw. Peter Isare akiwasilisha mada kuhusu kampuni hiyo
ambayo imenufaika na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Mwakilishi wa Kampuni ya Vijana ya
JATU SACCOS Ltd, Bw. Peter Isare (wa nne kutoka kulia) akimkabidhi
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Najma
Giga. (Wa nne kutoka kushoto) ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe.
Jenista Mhagama.
PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)
*************************************
Na; Mwandishi Wetu
Kamati ya Bunge
ya Katiba na Sheria imeridhishwa na utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya
Vijana “Youth Development Fund” unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu
katika kuchochea maendeleo ya shughuli za kiuchumi za vijana.
Hayo yameelezwa
na Mwenyekiti wa kamati hiyo ya kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe.
Najma Giga (Mb) wakati kamati hiyo ilipokutana kwa lengo la kufuatilia
utekelezaji wa mfuko wa maendeleo ya vijana katika ukumbi wa Katiba na
Sheria Bungeni Jijini, Dodoma.
Akizungumza
wakati wa kikao hicho alisema kuwa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana umekuwa
ni kielelezo tosha kwa serikali katika kuonyesha dhamira ya dhati ya
kuwasaidia vijana sambamba na kuendeleza miradi yao ya kiuchumi.
“Tunapongeza
Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kusimamia vizuri mfuko wa Maendeleo ya vijana
kwa kuwa umeendelea kuwa chachu kwa vijana kuanzisha makampuni na
vikundi vya uzalishaji mali katika ngazi ya halmashauri za wilaya, miji
na manispaa ambazo zimeibua fursa ya ajira kwa vijana,” alisema
Mheshimiwa Giga
Aliongeza kuwa
kupitia mfuko huo vijana waendelee kuhamasishwa zaidi kujishughulisha na
kubuni miradi mbalimbali ya kiuchumi na aliwataka kuongeza ubunifu
katika shughuli zao za uzalishaji mali.
Aidha alitoa wito
kwa vijana waliopata mikopo hiyo kuitumia vizuri mikopo hiyo kwa kuwa
inamanufaa ili waweze kunufaika nayo pia kuifanya miradi yao kuwa
endelevu.
Akielezea kuhusu
mfuko huo wa Maendeleo ya Vijana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alieleza kuwa lengo la kuanzishwa mfuko
maendeleo ya vijana na Serikali mwaka 2013 ilikuwa ilikuwa kuwawezesha
vijana kupata mitaji yenye masharti nafuu.
“Katika kipindi
cha miaka mine ya Serikali ya awamu ya tano yaani mwaka 2015 – 2018
jumla ya bilioni 2 zimetolewa katika vikundi vya vijana 533 vyenye idadi
ya vijana 3,780 katika halmashauri 128 nchini,” alisema Mhagama
Akielezea miradi
ya vijana iliyoweza kunufaika na mikopo ya mfuko huo ikiwemo Kilimo,
Ufugaji, Viwanda vya kuchakata (Ngozi, Madini, kusindika mazao ya
chakula, vifaa vya ujenzi, kutengeneza taulo za kike, kusindika chakula
cha mifugo), Makampuni yanayotoa huduma za mawasiano, makampuni
yanayotoa huduma za kifedha na makampuni yanayotoa huduma za elimu.
Alieleza kuwa
Serikali inaendelea kuwahamasisha vijana pamoja na wenye ulemavu
kuendelea kuchangamkia fursa ya mikopo hiyo ambayo imekuwa kielelezo
katika kubadili mtazamo wa vijana kujijengea dhana ya kujitegemea na
kukuza vipato vyao.
“Mwaka huu wa
fedha 2019/2020 Serikali inatarajia kutoa mikopo yenye thamani ya
shilingi milioni 850 kwa vikundi vya vijana 224 katika halmashauri za
wilaya 56, kwa dhamira hii njema ya serikali ni wakati muafaka vijana
wakawa wabunifu katika kuanzisha miradi yenye tija itakayowawezesha
kukopesheka,” alieleza Mhagama
Aidha aliwashauri
vijana walionufaika na mfuko huo wahakikishe wanarejesha mikopo hiyo
kwa wakati ili mfuko huo uweze kuwa endelevu na manufaa kwa vijana.
0 comments:
Post a Comment