
***********************************
Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
DAR ES SALAAM
22.10.2019
MWAKA 1979 Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria Na. 4 ya mwaka 1979 kuhusu
uchaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa unaowawezesha mwananchi
kushiriki katika kuchagua Kiongozi kupitia uratibu wa Halmashauri za
Wilaya.
Moja ya malengo ya uchaguzi huo ni
kuwapatia wananchi na viongozi fursa ya kutafakari kujadili kuhusu
changamoto za maisha ya watu na namna bora ya kukabiliana nazo pamoja na
kuwakumbusha wagombea kuwa kura ni mkataba baina ya mwananchi na
mgombea.
Ibara ya nane ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatamka wazi kuwa Tanzania ni
nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, ambapo moja ya
misingi hiyo ni uhuru wa maoni, ushiriki na kupiga au kupigiwa kura.
Aidha moja ya haki za kijamii
afya, maji, kilimo, hifadhi ya jamii na elimu, hivyo kutokana na misngi
huo yapo mahusiano makubwa baina ya ushiriki katika uchaguzi huru na
upatikanaji wa huduma za jamii.
Pia kipengele cha pili cha Ibara
ya 21 ya Katiba kinatamka kuwa kila raia anayo haki na uhuru wa
kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomhusu
yeye, maisha yake au yanayolihusu Taifa, hivyo ni wazi kuwa uchaguzi ni
moja ya haki za kijamii inayomhusu kila Mtanzania.
Kwa mujibu wa ibara ya 145 ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Serikali za
Mitaa ndiyo mamlaka za wananchi ambazo huundwa, huendeshwa na huwajibika
kwa wananchi ambao ndiyo chimbuko la mamlaka yote katika nchi.
Aidha ibara ya 146 Katiba
inazitambua Mamlaka ya Serikali za Mitaa kama vyombo vya haki vyenye
mamlaka ya kuwashirikisha wananchi kupanga na kutekeleza shughuli za
maendeleo na utoaji wa huduma muhimu na kuhakikisha zinasimamia utoaji
huduma za kijamii ikiwemo elimu, maji, afya, kilimo, ufugaji na uvuvi,
barabara, maliasili na utalii n.k.
Aidha, mamlaka hizo zipo kwa lengo
la kukuza demokrasia kwa kuwashirikisha wananchi kuchagua viongozi wao
na kwa mantiki hiyo ushiriki wa wananchi katika chaguzi za vyama vingi
zilizo huru na haki (kidemorkasia) ni nguzo muhimu ya kukuza utawala
bora na dhana ya maendeleo kwa ujumla.
Tarehe 24 Novemba mwaka huu
Watanzania wanatarajia kushirki katika Uchaguzi wa uchaguzi wa sita
chini ya mfumo wa vyama vingi kuwachagua viongozi wa Vijiji, Vitongoji
na Mitaa wanaotakiwa kuwepo madarakani kwa kipindi cha miaka mitano
ijayo kuanzia mwaka 2019 hadi 2024.
Uchaguzi huo unatarajia kutoa
taswira na mwongozo juu ya namna wananchi watakavyoshiriki katika
maamuzi na pia katika shughuli za maendeleo, uchumi wa nchi, huduma za
jamii na maisha yao kwa ujumla ikiwemo usimamizi wa miradi ya maendeleo
ambayo itakuwa na manufaa kwa umma.
Uwepo wa viongozi imara katika
Mamlaka za Serikali za Mitaa utawezesha Serikali kuepuka hasara
katika mikataba mbalimbali ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo
ikiwemo afya, elimu, maji na ujenzi kutokana na ukweli kuwa Serikali za
Mitaa ndizo zinazofanya kazi moja kwa moja katika jamii katika kutoa
maamuzi.
Upo uhusiano mkubwa wa kura yako
na suala la maendeleo katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa kuwa
uchaguzi huo huweza kuleta viongozi wanaopaswa kusimamia rasilimali
muhimu ikiwemo makusanyo ya mapato ikiwemo kodi, mikopo na michango ya
kijamii, fedha zitokanazo na huduma, ada ya leseni, ushuru, vibali n.k.
Moja ya changamoto kubwa
zilizokuwepo hapo awali katika Mamlaka za Mitaa ni pamoja na usimamizi
na matumizi ya rasilimali fedha jinsi inavyokusanywa na kutumika, hivyo
kupitia uchaguzi huo wananchi wanapata fursa ya kutafakari kuhusu mtu
wanayemtaka kumchagua kama anatosha kusimamia rasilimali hiyo.
Ni wazi kuwa moja ya jukumu la
anayechaguliwa ni pamoja na kutatua kero au changamoto nyingine kuhusu
afya, elimu, maji, migogoro ya ardhi na mipaka, hivyo
mpigakura anapaswa kutambua kuwa anayepaswa kuchaguliwa anaweza
kuzikabili changamoto hizi katika kijiji, kitongoji au mtaa.
Pia Uchaguzi wa Mitaa utawawezesha
wananchi kuchagua viongozi wawajibakaji wanaopaswa kutoa na kusoma
taarifa ya mapato na matumizi katika mikutano maalum ya mitaa, vijiji a
vitongoji jambo limekuwa likikwepwa na Viongozi na watendaji katika
Mamlaka hizo na hivyo kuzua malalamiko kuhusu wajibu wa serikali za
vijiji, mitaa na vitongoji kwa wananchi.
Ni wajibu wa wadau na wananchi
kujitokeza kwa wingi kwenye upigaji kura ili kuitumia vyema haki yao ya
kidemokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa kwa kuwa serikali itahakikisha
uwapo wa utulivu na usalama katika kipindi chote cha uchaguzi huo.
0 comments:
Post a Comment