SERIKALI ya Tanzania imelaani
vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Serikali ya Marekani dhidi ya Cuba
na Zimbabwe kwa sababu vinadhoofisha biashara, uwekezaji na ustawi wa
wananchi na imetaka vikwazo hivyo viondolewe.
Tamko hilo limetolewa leo
(Jumamosi, Oktoba 26, 2019) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye
Mkutano wa 18 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Zisizofungamana na
Upande Wowote (NAM) ulioanza leo huko Baku, Azerbaijan.
“Vizuizi na vikwazo vya
kiuchumi vilivyowekwa dhidi ya Cuba na Zimbabwe vinadhoofisha maendeleo
ya uchumi, uwezo wa kufanya biashara, fursa za uwekezaji na ustawi wa
wananchi wake.”
“Tanzania inaungana na Jumuiya
ya Kimataifa kutaka yawepo majadiliano ya msingi ambayo yataondoa
vizuizi kwa Serikali ya Cuba na vikwazo kwa Serikali ya Zimbabwe ili
kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa manufaa ya watu wa nchi hizo,”
amesema.
Mwaka 2001, Marekani na
Jumuiya ya Ulaya (EU) ziliweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Zimbabwe
baada ya Serikali ya nchi hiyo chini ya uongozi wa Rais Robert Mugabe
kuamua kuchukua ardhi yote iliyokuwa ikimilikiwa na wageni.
Waziri Mkuu ambaye anahudhuria
mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali kwa niaba ya Rais Dkt. John
Pombe Magufuli, aligusia mambo kadhaa ikiwemo mabadiliko ya tabianchi,
masuala ya Sahara Magharibi, usalama wa Palestina na msimamo wa Tanzania
kwenye Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM).
Kuhusu mabadiliko ya tabia
nchi, Waziri Mkuu amesema suala hilo ni mojawapo ya changamoto kubwa
zinazoikabili dunia na wanadamu kwa sasa. “Tunaiomba Jumuiya ya
Kimataifa iweke njia muafaka ambazo zitasadia kurekebisha tishio ambalo
tunakabiliana nalo hivi sasa. Tunazitaka nchi zilizoendelea zitimize
ahadi zao na michango ya kifedha, zisaidie kujenga uwezo na kutoa
wataalamu watakaozisaidia nchi zinazoendelea,” amesema.
Akizungumzia Sahara Magharibi,
Waziri Mkuu amesema suala la kujitawala kwa nchi hiyo limeingia sura
mpya baada ya Morocco kujiunga tena na Umoja wa Afrika na kwamba hivi
sasa imekuwa mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
“Ipo fursa kubwa hivi sasa kwa
Umoja wa Mataifa pamoja na mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa ya kuweza kushirikiana na chombo kipya cha Troika kilichoundwa
na Umoja wa Afrika katika kuliangalia suala zima la Sahara Magharibi.
Tanzania inaunga mkono jitihada hizo,” amesema Waziri Mkuu.
Kwenye suala la Palestina,
Waziri Mkuu amesema Tanzania inatambua kwamba nchi hiyo ina haki ya
kufurahia amani na uhuru wake kama ilivyo kwa Israeli, kwa mujibu wa
mkataba wa Umoja wa Mataifa. “Ni matumaini yetu kwamba kuendelea kuwepo
kwa jitihada za kimataifa, mgogoro huo utapatiwa ufumbuzi katika muda
muafaka na mataifa haya mawili yataishi kwa amani na utulivu.”
Waziri Mkuu alitumia fursa
hiyo kuelezea msimamo wa Tanzania kwenye umoja huo na kusisitiza kwamba
Tanzania bado ina imani na chombo hicho. “Tanzania itaendelea kuheshimu
kazi zinazofanywa na umoja huu kama ambavyo tumekuwa tukifanya kwa miaka
58 iliyopita.
Tunaomba ushirikiano baina ya nchi za Kusini uimarishwe.
Ushirikiano baina ya nchi zinazoendelea na zilizoendelea nao pia
uimarishwe.”
Amesema: “Serikali ya Tanzania
inapongeza uhusiano ulipo baina ya Umoja wa Nchi Zisizofungamana na
Upande Wowote (NAM), kundi la nchi 77 (G77) na China na kwamba
tunatamani ujizatiti zaidi kutetea maslahi ya umoja huu ambao wanachama
wake wengi ni nchi zinazoendelea.”
Waziri Mkuu Majaliwa
ameambatana na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika ya
Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro na Balozi wa Tanzania nchini Urusi ambaye
pia ni Balozi wa Azerbaijan, Meja Jenerali Mstaafu, Simon Mumwi.
0 comments:
Post a Comment