Na Mwandishi Wetu,MAELEZO
Dar Es Salaam
RAIS Dkt. John Magufuli amesema
Tanzania itaendelea kutekeleza kwa kasi kubwa miradi ya maendeleo nchini
kwa kuwa Serikali imeimarisha nidhamu katika usimamizi na matumizi ya
rasilimali zilizopo pamoja na ukusanyaji wa kodi.
Akizungumza katika hafla ya
upokeaji wa ndege mpya ya Serikali ya Boeing 787-8 Dreamliner katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere leo Jumamosi (Oktoba 26,
2019) Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli aliwataka Watanzania kujivunia
na kuendelea kuiunga mkono Serikali yao kwa kuwa imedhamiria kuwaletea
maendeleo ya kweli na ya haraka.
Rais Magufuli alisema Tanzania na
Bara la Afrika kwa ujumla lina uwezo wa kufanya mambo makubwa nay a
haraka kutokana na kubarikiwa na rasilimali nyingi ikiwemo madini na
hivyo Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kusimamia rasilimali hizo ili
ziweze kuleta manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi walio wengi.
‘’Watanzania sisi ni matajiri
tunaweza kufanya mambo makubwa na kununua vitu vizito kama ndege hizi,
na tukiamua tunaweza kinachotakiwa sasa ni kuweza kuwa na matumizi
mazuri ya fedha zinazopatikana kutokana na kodi tunazokusanya kutoka kwa
wananchi wetu’’ alisema Rais Magufuli.
Aliongeza kuwa malengo ya Serikali
ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa sekta ya usafiri wa anga inapiga
hatua kubwa ya maendeleo nchini na kwa kufanya hivyo Serikali imekusudia
kuliwezesha Shirika la Ndege Nchini ATCL kuweza kutekeleza mipango na
mikakati mbalimbali iliyojiwekea.
Akifafanua zaidi Rais Magufuli
alisema ATCL kwa sasa ina jumla ya ndege 7 kati ya ndege 11 zilizopangwa
kununuliwa na Serikali, hivyo aliitaka Menejimenti ya Shirika hilo
kujipanga vizuri ili kuhakikisha kuwa linamudu ushindani wa kibiashara
uliopo nchini ikiwemo kuimarisha mtandao wa usafirishaji abiria katika
soko la ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli
alisema ndege hiyo mpya ya Boeing 787-8 Dreamliner ni ndege kubwa ya
kisasa yenye uwezo wa kubeba abiria 262 ikiwemo abiria 22 wa daraja la
juu pamoja abiria 240 katika daraja la kawaida, hivyo kuitaka ATCL
kuweka mipango na mikakati endelevu ya kuhakikisha itangaza vyema
vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
‘ATCL hamna budi kujiendesha
kibiashara na mnapaswa kutambua ndege hii ni mali ya Serikali na si ya
ATCL hivyo na hilo linajionesha katika mkataba tuliosaini baina ya
Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu Mkuu (Uchukuzi), hivyo hakikisheni
mnafikia malengo yote tuliyowekeana’’ alisema Rais Magufuli.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dkt. Leonard Chamuriho
alisema Shirika la ATCL limeendelea kutekeleza kwa mafanikio makubwa
Mpango Mkakati wa Shirika hilo, ambapo sasa limeweza kufikia mafanikio
ya asilimia 73 la usafirishaji wa abiria katika soko la ndani.
Aidha Dkt. Chamuriho anaongeza
kuwa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya safari za abiria nje ya nchi,
Shirika hilo pia limefanikiwa kuongeza idadi ya upokeaji wa shehena za
mizigo kutoka nchini India na kufikia tani 178 na kuzisafirisha katika
nchi mbalimbali ikiwemo Zambia.
Aliongeza kuwa Shirika hilo
limepanga kushirikiana na Taaasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF) pamoja
na Chemba ya Biashara,Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) kwa ajili ya
kuweka nguvu na mkakati wa pamoja wa kuhakikisha kuwa inatanua mtandao
wa usafirishaji wa shehena za mizigo nchini India.
Kuhusu soko la ndani,
Dkt.Chamuriho aliongeza kuwa Shirika hilo limeweza kuongeza kituo cha
usafirishaji wa abiria katika Kituo cha Mpanda Mkoani Rukwa pamoja na
kupanga kuongeza idadi ya miruko ya ddege kutoka Dar es Salaam-Dodoma
kufikia mara nne kwa siku ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.
Naye Kaimu Balozi wa Marekani
Nchini , Dkt. Imni Patterson aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano
kutokana na juhudi na hatua mbalimbali za makusudi inazochukua katika
kuimarisha sekta ya usafiri wa anga kwani kwa kufanya hivyo kutaweza
kutangaza sekta ya utalii pamoja na kuimarisha uchumi
0 comments:
Post a Comment