
********************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka Wakuu wa Polisi katika nchi za Mashariki mwa Afrika waweke
mikakati thabiti ya kukabiliana na magenge yote ya uhalifu unaovuka
mipaka ili wahalifu hao wasipate mahali salama pa kufanya uhalifu bila
mkono wa dola kuwafikia.
Pia, Waziri Mkuu amewataka
viongozi hao wadumishe ushirikiano baina yao ili waimarishe utendaji
bila kujali mipaka ya nchi zao kwa sababu wahalifu wanatumia sana
udhaifu wa kukosekana ushirikiano madhubuti miongoni mwa nchi hizo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
(Alhamisi, Septemba 19) wakati akifunguaMkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho
la Wakuu wa Polisi Mashariki mwa Afrika (EAPCCO), uliofanyika kwenye
ukumbi wa AICC, jijini Arusha. Amefungua mkutano huo kwa niaba ya Rais
Dkt. John Magufuli.
Amesema mfumo wa uhalifu
duniani kwa sasa unachukua sura mpya kufuatia kukua kwa teknolojia
hususani ya habari na mawasiliano, uhuru wa watu na bidhaa kuvuka mipaka
pamoja na kuondolewa vikwazo vingi hususani visivyo vya kiforodha,
hivyo kumewezesha kuwepo kwa fursa ya maendeleo kwani bidhaa na watu
husafiri kwa wepesi na haraka zaidi hivyo kufanya ukanda huo na dunia
kwa ujumla kuwa kama kijiji kimoja.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema
maendeleo hayo kwa upande mwingine yameleta athari za kiusalama kwani
wahalifu nao wanatumia fursa hiyo kuimarisha magenge yao ya uhalifu
unaovuka mipaka, mfano biashara ya dawa za kulevya.
“Uhalifu mwingine ni wizi wa
magari, ujangili, utoroshaji madini na biashaa haramu ya binadmu, ugaidi
utengenezaji na uuzaji wa bidhaa bandia na uharamia katika maziwa na
baharini, utakatishaji wa pesa zinazotokana na uhalifu huo na vitendo
vya rushwa.”
Waziri Mkuu amesema ushirikiano
unahitajika katika kuzuia uhalifu ikiwemo mafunzo kwa watendaji hasa kwa
makosa yanayovuka mipaka, operesheni za pamoja, upelelezi wa pamoja na
ubadilishanaji wa taarifa za kiintelijensia ili kuyasaka, kuyabaini na
kuyakamata magenge ya watuhumiwa wanaofanya makosa katika nchi moja na
kwenda kujificha katika nchi nyingine.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema
kwamba anatambua katika jukumu lao la kutekeleza sheria bado
wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi
ili waweze kufikia lengo lao la kiutendaji kwa haraka zaidi.
Waziri Mkuu amezitaja baadhi ya
changamoto hizo ni pamoja na utashi wa kisiasa.“Ili kutokomeza uhalifu
wa aina yoyote utashi wa kisiasa unahitajika sana. Lengo ni kuvipatia
nguvu vyombo vya dola katika kusimamia sheria. Niwatake wanasiasa
wengine tutoe ushirikiano kwa vyombo hivi ili viwe na meno kwa kutunga
sheria zitakazo wawezesha kuafanya kazi zao ipasavyo”
Changamoto nyingine aliyoitaja
Waziri Mkuu ni utofauti wa sheria baina ya nchi zao. Amesema iwapo
sheria zao zitabaki kuwa tofauti, wataendelea kutoa mwanya kwa wahalifu.
“Wahalifu wataendelea kufanya uhalifu nchi moja na kukimbilia nchi
nyingine ambapo sheria haiwabani, lakini sheria zikiwa zinafanana
watakosa pa kukimbilia.”
Waziri Mkuu amesema suala la vita
dhidi ya rushwa lazima lisimamiwe kwa nguvu zote kwani kama hatua
madhubuti hazitachukuliwa katika kuimarisha uadilifu, vitendo vya rushwa
vitashamiri na kusababisha kuimarika kwa magenge ya uhalifu kwa vile
wahalifu watakua na uhakika wa kukwepa mkondo wa sheria.
Pia, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa
ustawi wa nchi zao katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii
utategemea hali ya usalama, amani na utulivu, hivyo katika ukanda wao
wa Afrika Mashariki wanategemea sana utekelezaji madhubuti wa mipango na
mikakati watakayojiwekea.
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la
Polisi Tanzania, IGP Simon Sirro ambaye leo amekabidhiwa uenyekiti
wa EAPCCO, amesema atashirikiana vizuri na viongozi wenzake ili
kuhakikisha hali ya amani na utulivu vinaendelea kuwepo kwenye nchi
zao.
Pia, IGP Sirro ametumia fursa hiyo
kuwashukuru marais wa nchi hizo kwa ushirikiano wanaowapa hali
inayowawezesha kutimiza majukumu yao ipasavyo. Amekabidhiwa uwenyekiti
wa shirikisho hilo na Mkuu wa Jeshi la Polisi la Sudan na Mwenyekiti wa
Shirikisho la Wakuu wa Polisi Mashariki mwa Afrika anayemaliza muda
wake, Luteni Jenerali Adil Mohammed.
Shirikisho hilo linaundwa na
nchi 14 ambzo ni Tanzania, Burundi, Jamuhuri ya Kimokrasi ya Congo
(DRC), Djibouti, Kenya, Sudan, Sudan ya Kusini, Somalia, Rwanda, Uganda,
Shelisheli, Comoro, Eritrea na Ethiopia.
0 comments:
Post a Comment