METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, November 26, 2018

FCS YAJITOLEA KUCHANGIA DAMU HOSPITALI YA MUHIMBILI, KITENGO CHA MOI

Taasisi inayojihusisha na kutoa ruzuku kwa asasi za kiraia hapa nchini ya Foundation for Civil Society mapema jana imeendesha zoezi maalum la kujitolea damu kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa mbalimbali wenye uhitaji wa damu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha MOI.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema  jana katika zoezi hilo la uchangiaji wa damu Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society Bw. Francis Kiwanga amesema kuwa, wao wameamua kuchangia damu kwa wagonjwa ikiwa ni kama njia moja wapo ya kurudisha kitu kwa jamii.

Aidha Mkurugenzi huyo aliendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kuchangia damu nakuwataka wajitokeze kwa wingi  katika zoezi hilo hasa vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa.

 “Tumekuja hapa kuchangia damu kwa kuwa ni hospitali ya Taifa na ni sehemu yenye uhitaji mkubwa sana wa damu. Tunawaomba watanzania wengine wajitokeze kuchangia ili kuwaokoa watanzania wenzetu lakini pia kuunga mkono jitihada za shirika la damu salama ambalo kila kukicha wanaelezea umuhimu wa wananchi kuchangia damu ili kunusuru maisha ya wananchi wenzetu ” Alisema Kiwanga

Ameongeza kuwa mbali na kujitoa kwao katika zoezi la kuchangia damu lakini pia wamejipanga kwenda kuwasaidia wasichana wanaoishi katika mazingira   magumu wa kituo cha New Hope for Girls kilichopo Kimara jijini Dar es salaam Tarehe 27/11 mwaka huu katika siku ya Jumanne ya kutoa.
Mmoja wa wachangiaji wa damu katika Kampeni hiyo iliyoendeshwa na Taasisi ya Foundation for Civil Society, Gloria Wangeleja(Mwenye nguo ya Rangi Nyekundu) akitoa        damu mapema jana katika Hospitali ya Muhimbili jijini 
                                 Dar es salaam.

KWA upande wake Mkuu wa Kitengo cha Maabara Moi Dokta Mbuta Jakckson alisema kuwa  licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na makundi ikiwamo wafanyakazi wa Taasisi mbalimbali, vikundi vya dini lakini bado changamoto hiyo haikuweza kumalizika na kusema kuwa kwa mahitaji ya kaiwada ya damu kwa siku ni unit 70 lakini zinazopatikana ni unit 40 mpaka 50 peke yake.

Amesema hospitali ina wataalamu wa kutosha wa kukusanya damu, watu hawana haja ya kutia shaka na uwezo wa taasisi hiyo katika kukamilisha zoezi hilo.

“Tumekuwa tukienda hata nje ya kituo hiki, kwa mfano tulikwenda temeke katika msikiti mmoja hivi jina nimelisahau, lakini pia tulifika kwenye makampuni mbalimbali kuchukua damu. Tunachohitaji ni utayari wa raia, tuko tayari wakati wote kufika mlipo ili tuchukue damu itakayowasaidia wagonjwa” alisema.

Aliendelea kusisitiza kuwa hapo mwanzo wagonjwa walikuwa wakichangiwa damu kutoka kwa ndugu na jamaa zao, lakini kwa sasa hali imebadilika na wanaochangiwa na ndugu zao ni wachache sana ukilinganisha na wasio na watu wa kuwachangia, hali inayosababisha kuchelewa kwa huduma kutokana na kutokuwepo na damu katika benki hiyo.
               Wachangiaji wakiendelea kujitolea damu.

Naye Shabani Mwin’juma Shekihenda, Mlemavu wa macho ambaye alijitokeza katika zoezi hilo la uchangiaji damu, ameshindwa kutimiza azma yake hiyo baada ya kupimwa na kugundulika kuwa damu yake ni ndogo na asingeweza kuhimili kama angetolewa.

Akizungumzia tukio hilo, Mwin’juma anasema amesononeshwa sana na kushindwa kuchangia damu kwani aliamini chupa ya damu yake ndogo ingeweza kunusuru maisha ya kiumbe mwingine.

Amesema Licha ya ulemavu wake lakini anauwezo wa kutembea sehemu yoyote ile, hivyo haina maana kuwa hana wajibu wa kusaidia wengine, ameguswa na tukio hilo na kuamua kutoka nyumbani kwakwe Buza kwa lengo la kutoa damu.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com