METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, November 25, 2018

HALMASHAURI NA MIJI ILIYOFANYA VIBAYA KATIKA MASHINDANO YA AFYA NA USAFI WA MAZINGIRA ZATAKIWA KUJITATHMINI

                    
                 ..................................................................................................
NA WAMJW-DODOMA

Halmashauri za Miji, Majiji, Wilaya, Vitongoji na Vijiji zilizofanya vibaya katika mashindano ya afya na usafi wa mazingira zimetakiwa kujitathmini na kuhakikisha zinaweka mikakati madhubuti ya utunzaji wa mazingira.

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa kilele cha wiki ya usafi wa mazingira ulioenda sambamba na mkutano uliojumuisha Maafisa Afya nchini na Wadau mbalimbali wa maendeleo kilichofanyika jijini Dodoma.

Waziri Ummy alisema hayo wakati akitaja washindi waliofanya vizuri katika Halmashauri za Miji, Majiji, Wilaya, Vitongoji na Vijiji viliyofanya vizuri katika mashindano ya afya na usafi wa mazingira ambayo Wizara imekuwa ikitekeleza tangu mwaka 1988.

“Mashindano hayo huanza katika ngazi ya Kitongoji na kuhitimishwa kwa kupata washindi wa kitaifa. Kila mwaka tumekuwa tukiboresha mashindano haya ambapo kwa mwaka huu tumeongeza makundi manne kutoka sita ya awali. Makundi yalioongezeka ni; Hospitali za Rufaa za Binafsi, Shule za Msingi za Vijijini, Shule za Sekondari za Bweni za Serikali, na Shule za Sekondari za Bweni za Binafsi”. Alisema Waziri Ummy.
Aidha, waziri huyo alitaja makundi ya washindi waliofanya vizuri na makundi ya Halmashauri, Majiji na Mikoa iliyofanya vibaya.

Katika kundi la Halmashauri za Manispaa na Majiji lilihusisha Manispaa 25, ambapo Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ilikua kinara kwa asilimia 92.7, ikifuatiwa na mshindi wa pili Halmashauri ya Jiji la Arusha asilimia 90.5 na mshindi wa tatu ikiwa ni Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa asilimia 89.7.

Kundi la pili lilikua la Halmashauri za Miji ambapo lilihusisha Halmashauri za miji 22 nchini. Mshindi wa kwanza ni Halmasahuri ya mji wa Njombe asilimia 93.4, Halmashauri ya Mji wa Kahama ikishika nafasi ya pili kwa asilimia 75.0 na Halmashauri ya Mji wa Tunduma ikiwa nafasi ya tatu kwa asilimia 73.5.

Kundi la tatu la Halmashauri za Wilaya, ambapo lilishirikisha Halmashauri za Wilaya 25. Mshindi wa kwanza ni Halmasahuri ya Njombe ikiongoza kwa kupata asilimia 98.3, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Meru Asilimia 88.0 na mshindi wa tatu ni Halmasahuri ya wilaya ya Mufindi Asilimia 80.2.

Kundi la nne lilihusisha Halmashauri za Vijiji ambapo vilishiriki vijiji 47 kwa wastani wa vijiji viwili kwa kila Halmashauri ya Wilaya iliyoshiriki. Kiongozi wa kundi hili ni Kijiji cha Ikuna, Kata ya Ikuna, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe asilimia 97.3. Mshindi wa pili ni Kijiji cha Kidegembye, Kata ya Kidegembye, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe  asilimia 97.0. Na kijiji cha cha Kikwe, Kata ya Kikwe, Halmashauri ya Wilaya ya Meru kilishika nafasi ya tatu kwa asilimia 86.5.

Kundi la Tano lilihusisha shule za msingi za vijiji, ambapo Shule za msingi 47 za serikali zilishiriki. Katika kundi hili shule iliyoongoza ni Shule ya Msingi Ikuna, Kata ya Ikuna, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe  kwa asilimia 98.7. ikifuatiwa na Shule ya Msingi Kidegembye, Kata ya Kidegembye, Halmshauri ya Wilaya ya Njombe kwa asilimia 97.8 na mshindi wa tatu ilikua Shule ya Msingi Kikwe, Kata ya Kikwe, Halmashauri ya Wilaya ya Meru ikiwa na asilimia 89.7.

Katika kundi la sita lilimujuisha shule za sekondari za bweni kutoka katika mikoa 25 nchini. Shule iliyoibuka kidedea ni Shule ya Sekondari Njombe, iliyopo Halmashauri ya Mji wa Njombe kwa asilimia 91.7. Ikifuatiwa na  Shule ya Sekondari ya Ufundi Tanga, Halmashauri ya Jiji la Tanga asilimia 90.9, na mshindi wa tatu ni Shule ya Sekondari ya Wasichana Ifakara, Halmashauri ya Mji wa Ifakara yenye asilimia 90.5.
Kundi la saba lilihusisha Shule za Sekondari za Bweni za Binafsi ambapo Shule ya Sekondari St. Francis, Halmashauri ya Jiji la Mbeya iliongoza kwa asilimia 99.0, ikifuatiwa na Shule ya Sekondari ya Wasichana St. Monica, Halmashauri ya Jiji la Arusha iliyokua na asilimia 97.6 huku msahindi wa tatu ikiwa Shule ya Sekondari ya Savannah Plain, Halmashauri ya Mji Kahama  yenye asilimia 97.0.
Kundi la nane lilikua linajumuisha Hospitali za Rufaa za Mikoa za Serikali ambapo Hospitali 25 za Rufaa za Mikoa za Serikali zilishiriki. Mshindi katika kundi hili ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro iliyokua na asilimia 89.8, ikifuatiwa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara yenye asilimia 88.3 na mshindi wa tatu ni Hospitali ya Rufaa ya Mt. Meru yenye asilimia 88.0.
Kundi la tisa lilishirikisha Hospitali za Rufaa za Binafsi ambapo washiriki walikua tisa (9). Kundi hili lina washindi wawili kutokana kuwa na washiriki wachache. Ambao ni Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center yenye asilimia 95.4 na Hospitali ya Dodoma Medical Center iliyokua na asilimia 80.6.
Kundi la kumi na la mwisho lilihusisha Hoteli ambapo washiriki walikua 26 ikiwa ni hoteli moja kwa kila mkoa. Hoteli ya Melia Mkoa wa Mara imeibuka mshindi wa kundi hili kwa asilimia 98.5, ikifuatiwa na Hoteli ya Ruhuwiko Hunt Club iliyoko Mkoa wa Ruvuma kwa asilimia 96.3 na Hoteli ya Mt. Meru ya Mkoa wa Arusha ilishika nafasi ya tatu kwa kuwa na asilimia 93.3.
Waziri Ummy alitaja mgawanyo wa zawadi zilizotolewa  ni pamoja na Tuzo Maalum, Trekta yenye Tela, Gari (FWD) Ford Ranger, Vyeti vya ushindi, pamoja na Pikipiki. Zawadi hizo zilitolewa kulingana na makundi kumi  yaliyoshindanishwa  kuanzia ngazi za Vijiji  hadi Halmashauri za Majiji na Manispaa
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com