…………………..
Na Munir Shemweta, WANMM NYAMONGO
Zoezi
la uthamini kulipa fidia kwa wananchi wa Nyamongo wilaya ya Tarime mkoa
wa Mara kupisha upanuzi wa Mgodi wa Dhahabu North Mara kwa ajili ya
ujenzi wa Bwawa la Maji Taka limekumbwa na changamoto kufuatia baadhi ya
wananchi kujenga nyumba ama kuongeza sehemu za nyumba zao maarufu kama
‘Tegesha’ ili kujipatia faida kupitia thamani ya fidia.
Wathamni
katika zoezi hilo walibaini tofauti kubwa katika uthamini walioufanya
awali na pale walipoenda kwa mara ya pili kwa ajili ya uhakiki ambapo
ilibainika baadhi ya vyumba katika nyumba zilizofanyiwa uthamini kuwa
wazi baada ya waliokuwa wakiishi kuondoka baada ya kuthaminiwa.
Imeelezwa
kuwa lengo wananchi wanaofanya ujanja wa ‘Tegesha’ ni kujipatia posho
ya makazi ambayo kwa kawaida hutolewa kama fidia kwa wamiliki kulingana
na idadi ya vyumba kwenye nyumba ya mmiliki.
Kwa
mujibu wa Wathamini wa zoezi hilo, mbali na wamiliki walioathirika na
zoezi hilo kulipwa gharama nyingine kama vile nyumba na mazao pia
hulipwa posho ya makazi kwa kipindi cha miezi 36 lengo kumuwezesha mpangaji kupata mahali pa kuishi kabla ya kuanza zoezi la kuondolewa.
Mwandishi
wa Gazeti hili alishuhudi moja ya nyumba iliyopo kitongoji cha Kigonga A
katika kijiji cha Matongo ikiwa na vyumba ishirini na moja wakati
nyumba hiyo ilistahili kuwa na vyumba vitatu na baadhi ya vyumba havina
hata madirisha.
Mthamni
Mkuu wa Serikali Evaline Mugasha ambaye alitembelea baadhi ya nyumba
hizo kukagua maendeleo ya kazi ya uthamini katika eneo hilo aliweka wazi
kuwa Ofisi yake inafanya kazi kwa kufuata sheria ya Uthamini na hatua
kali zitachukuliwa kwa mtu atakayeonekana kufanya udanganyifu kwa kwa
lengo la kujipatia kipato.
Kwa
mujibu wa Mugasha, zoezi la uthamini katika eneo la Nyamongo
linalohusisha vitongoji vitatu katika kijiji cha Matongo limekuwa
likifanyika kwa uwazi na kushirikisha pande zote wakati wa kuorodhesha
mali na kufafanua kuwa hata mwananchi asiyeridhika na uthamini katika
eneo lake hupewa fomu maalum ya kujaza lengo likiwa kutoa haki.
‘’Tumeona
watu walihamisha magodoro, vitanda na mizigo mingine lengo ni kupata
posho ya makazi ili kujipatia faida na cha kushangaza baadhi ya
wapangaji hawajui hata choo cha nyumba wanayoishi kilipo, ofisi yangu
haitavumilia vitendo hivyo kila mtu atalipwa anachostahili’’ alisema
Mugasha.
Mthamini
kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Lazaro Magumba alieleza kuwa
wakati zoezi la uthamini kumekuwa na changamoto hasa wakati wa kukagua
mali za wananchi kutokana na baadhi yao kuwa na dhana ya kujipatia
utajiri kupitia mradi huo ambapo hufanya maendelezo ya kuegesha maarufu
kama ‘tegesha’ ili kulipwa fedha nyingi.
‘’
Wananchi wanajenga nyumba zilizopangana na hakuna hata nafasi na wakati
wa uthamni usiku kucha watu wanahamisha vyombo, magodoro na wengine hata
wanyama ili ionekane ni makazi halali’’ alisema Lazaro.
Alisema
wanachokifanya wao ni kukagua kwa awamu kwa lengo la kujiridhisha kama
kweli walionekana wakati wa uthamini kama ni wakazi halali ama walienda
kutegesha.
Baadhi
ya wakazi wa kijiji cha Matongo wilayani Tarime mkoa wa Mara ambao
hawakupenda majina yao yawekwe wazi kutokana na sababu za kiusalama
walikiri kuwepo mchezo huo wa Tegesha lakini walidai hufanywa na watu
wasio wakazi wa muda mrefu katika kijiji hicho bali walienda kwa lengo
la kujipatia faida kupitia zoezi hilo.
Kwa
mujibu wa wakazi hao, baadhi ya wananchi kutoka nje ya kijiji hicho
walinunua nyumba ama maeneo kwa wenyeji na kuongeza vyumba na
kuwakodisha watu kuishi ili kuvizia zoezi la uthamini wa fidia wapate
faida.
Kwa
muda mrefu wananchi wa Nyamongo wilaya ya Tarime mkoa wa mara hasa wale
wanaoishi vitongoji vinavozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara
wamekuwa wakilalamikia uchafuzi wa mazingira hasa maji yanayovuja kutoka
Mgodi huo kuwa yana sumu inayoathiri afya zao jambo lililomlazimu Rais
John Pombe Magufuli wakati wa ziara yake katika eneo hilo kuagiza
kufanyika utafiti ili kubaini ukweli huo.
0 comments:
Post a Comment