Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza umuhimu wa sekta binafsi nchini wakati akifungua warsha ya Wadau wa Baraza la Kilimo na Mifugo Tanzania (ACT) katika Hoteli ya New Afrika Jijini Dar es salaam tarehe 26 Novemba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo)
Sehemu ya Wadau wa Kilimo na Mifugo nchini wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati akifungua warsha ya Wadau wa Baraza la Kilimo na Mifugo Tanzania (ACT) katika Hoteli ya New Afrika Jijini Dar es salaam tarehe 26 Novemba 2018.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua bidhaa zilizoongezwa thamani ndani ya nchi wakati wa hafla ya warsha ya Wadau wa Baraza la Kilimo na Mifugo Tanzania (ACT) katika Hoteli ya New Afrika Jijini Dar es salaam tarehe 26 Novemba 2018. Kulia ni Maryam Issa mtendaji wa Kampuni ya NatureRipe.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza wakati akifungua warsha ya Wadau wa Baraza la Kilimo na Mifugo Tanzania (ACT) katika Hoteli ya New Afrika Jijini Dar es salaam tarehe 26 Novemba 2018.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam
Serikali imedhamiria kufanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Kilimo ambapo Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara za Sekta ya Kilimo (ASLMs) na wadau wa kilimo inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (Agricultural Sector Development Programme Phase Two-ASDPII).
Katika utekelezaji wa ASDP II serikali imelenga kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo (mazao, mifugo na uvuvi) ili kuongeza uzalishaji na tija, kufanya kilimo kiwe cha kibiashara na kuongeza pato la wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha maisha na usalama wa chakula na lishe.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo tarehe 26 Novemba 2018 wakati akifungua warsha ya Wadau wa Baraza la Kilimo na Mifugo Tanzania inayofanyika katika Hoteli ya New Afrika Jijini Dar es salaam.
Alisema Utekelezaji wa lengo hilo ni kuhakikisha kuwa Taifa linaendelea kujitosheleza kwa chakula; kuimarisha uchumi; kuwa kichocheo cha kukua kwa viwanda; na kuongeza ajira ambapo ili kufikia malengo hayo; Utekelezaji wa ASDP II utazingatia mnyororo wa thamani wa mazao ya kipaumbele ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mhe Hasunga alisema kuwa Serikali itaendelea kuboresha mifumo ya upatikanaji wa pembejeo bora kwa wakulima na wafugaji na kwa bei nafuu.
“Tumeanza na mbolea ambapo kwa sasa inaagizwa kwa pamoja na tumeondoa kodi na tozo nyingi katika mbolea ili ipatikane kwa bei nafuu. Kwa sasa changamoto kubwa imebaki kuwa gharama kubwa ya usafirishaji hasa kwa maeneo ambayo hakuna usafiri wa reli ambapo Serikali bado inalifanyia kazi suala hili” Alikaririwa Mhe Hasunga na kuongeza kuwa
“Changamoto nyingine kama nilivyozitaja hapo awali tutaendelea kuzifanyia kazi na tunaomba wadau kupitia vyama vyenu na taasisi kilele kama Baraza la Kilimo, muendelee kutupa maoni yetu ya namna bora ya utatuzi na sisi tunaahidi kufanyia kazi maoni yenu”.
Kuhusu Masoko ya mazao ya kilimo Mhe Hasunga alisema kuwa serikali inatambua changamoto za masoko, usindikaji, miundombinu ya umwagiliaji na miundombinu mingine kwa ajili ya mifugo na uvuvi, upatikanaji wa pembejeo bora kwa wakati na kwa bei nafuu, uhaba wa maafisa ugani, kero za kodi na tozo mbalimbali, wingi na mwingiliano wa taasisi za udhibiti huku akiahidi kuendelea kuzitafutia ufumbuzi.
“Baadhi ya kero hizi zimeshaanza kufanyiwa kazi. Mifano michache ni kuhusu tozo na kodi ambapo Serikali imeondoa kodi na tozo nyingi katika sekta ya Kilimo na bado tunaendelea kufanya maboresho katika eneo hilo.” Alisema
Aidha, alisema kuwa Wizara ya Kilimo inatambua mahusiano ya moja kwa moja kati ya Sekta ya Viwanda na ile ya Kilimo na pia changamoto zilizopo.
“Pamoja na dhamira ya Serikali iliyokuwepo katika kuweka mazingira mazuri ya biashara, ACT kama sehemu ya timu ya Kikosi Kazi Cha Taifa Cha Kuishauri Serikali Kuhusu Masuala ya Kodi, imekuwa ikitekeleza jukumu hilo bila kuchoka ambapo kwa kupitia ushauri huo, katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 na 2018/2019 Serikali imepunguza kodi na tozo nyingi sana katika sekta ya kilimo” Alisisitiza Mhe Hasunga
Alisema kutokana na jitihada hizi za ACT katika kuona kuwa kilimo kinakuwa moja ya ajenda kubwa kitaifa, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imekubali kuwa na makubaliano maalumu na ACT (Memorandam of Understanding – MoU) kwa lengo la kuifanya sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Warsha ya Wadau wa Baraza la Kilimo na Mifugo yenye kauli mbiu isemayo“Kilimo na Maendeleo ya Viwanda Tanzania” itafanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 26-27 Novemba 2018 ambapo wadau wa sekta ya Kilimo katika maeneo mbalimbali ya mnyororo wa thamani yaani kuanzia wazalishaji (wakulima, wafugaji na wavuvi), wasindikaji, watoa huduma mbalimbali kama wasafirishaji na wauza pembejeo, wafanyabiashara ya mazao, wasindikaji ikiwa na mada mbalimbali zenye kuakisi juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya Kuwa na Uchumi wa Viwanda ifikapo 2015.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment