
Si jambo rahisi sana kuzungumzia mambo ya miaka mingi ijayo, kana kwamba yameshakuwa au yamekaribia.
Dunia nzima inazungumzia Qatar 2022? Unaweza kuonekana mwehu kuzungumzia 2026 wakati wenzio wapo makini kujiandaa na 2022.
Lakini katika yote hayo najiuliza je? Tunataka kujiweka kundi
moja na Morocco, Senegal, Brazil, Saudi Arabia, Korea kusini, Ufaransa,
Hispania nk? Kwamba kwa kuwa wao wanazungumzia Qatar basi nasi
tujiingize kwenye mjadala huo?
Ni vema tukawa “wehu” kwa sasa hivi, tukiwaacha wao waendelee,
kujiandaa na kupigania nafasi na sisi tuwekeze nguvu zetu zote kwenye
kufuzu 2026.
Tunaweza kufanya hivyo kwakuwa mtaji wa kufanya hivyo tunao na
tukiamua “kudunduliza” sasa nina uhakika ifikapo 2026 tutakuwa miongoni
mwa watu watakaokuwa wametulia wanakula “popcon” kusubiria kipyenga cha
kuanza kwa michuano hiyo kama washindani na si wasindikizaji au
watazamaji.
Serengeti boys, Ngorongoro heroes na Karume boys ndiyo mtaji wetu kwa sasa.
Tunahitaji serikali kupitia wizara, baraza la michezo na
shirikisho la soka kwa upande mmoja, na wadau wote wapenda soka kwa
upande mwingine tukae chini tuwaze na kuja na jibu moja muafaka la
kufanya mapinduzi makubwa ya mfumo wa uendeshaji soka nchini kwetu.
Badala ya kuwaahidi hawa vijana mamilioni ya fedha endapo
watafanya vzr kwenye michuano fulani, tuamue kuwa zawadi pekee ni
kuwapeleka na kuwalipia shule za soka huko barani ulaya kwenye nchi
angalau tatu tofauti.
Ungeniambia nichague ningesema Ureno, Ufaransa na Uholanzi
ambako pamoja na kufundishwa soka kitaalamu pia ingekuwa ni rahisi kwa
wao kupata mawakala timu za kuchezea wawapo kwenye shule hizo, wakati
huo huo tungekuwa tunawatumia kama timu ya taifa ya vijana ambayo
tungeipa majukumu ya kufuzu kwa AFCON NA KOMBE LA DUNIA kwa vijana U’17
na U’20.
Wakati haya yakiendelea tungeingia mkataba na moja ya vyama vya
soka huko barani ulaya pamoja na UEFA kwa msaada wa FIFA kutufundishia
waalimu wa soka “makocha” kwa VIWANGO mbalimbali ambao wangekuja
kutufundishia vijana wetu katika shule za msingi na sekondari.
Kama serikali ikiweza kuajiri mwalimu mmoja kila shule, au
kuwafundisha masomo ya “ukocha” waalimu wote wa michezo wa shule za
msingi na sekondari angalau kwa kiwango cha cheti na stashahada basi
maana yake Kwa miaka 7 tuna uwezo wa kuzalisha wachezaji zaidi ya elfu
tano waliokulia katika misingi sahihi ya soka ambao wanaingia katika
ngazi ya soka la ushindani.
Tunapofanya haya ni muhimu kutambua kuwa hakuna njia ya mkato kufikia mafanikio katika soka.
Tuanze sasa safari ya kombe la dunia 2026 na inawezekana.
Wakati wenzetu wana akina Samatta na Msuva kwa maelfu sisi
hatuna mpango wa kuzalisha wengine kwa uwingi huku tukisubiri kudra za
Mwenyezi ili kufuzu kwa michuano mikubwa ya kimataifa.
Wasaalamu
0 comments:
Post a Comment