
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa maelekezo.
………………..
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo ameitaka Mamlaka ya Maji Safi Sumbawanga (SUWASA) kukaa na
Wizara ya Maji kuona namna ya kuweza kumaliza shida ya maji katika mji
mdogo wa Namanyere, Wilayani Nkasi ili wananchi waweze kuepukana na
shida hiyo ya muda mrefu na hatimae kuwa na Imani na serikali juu ya
utekelezaji wa ahadi zake kwa wananchi.
Amesema kuwa awali wananchi
waliaminishwa kuwa baada ya upanuzi wa bwawa la mfili shida ya maji
ingekuwa imekwisha, lakini matokeo yake baada ya upanuzi huo bado shida
ya maji imeendelea kuwepo ambapo sasa kuna mradi wa ujenzi wa matenki
mapya ambayo hayatakidhi mahitaji ya maji katika mji huo unaokuwa kwa
kasi na hivyo kuwataka kujipanga kumaliza tatizo hilo.
“Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha
Mapinduzi inasema huku kwenye miji mikuu ya wilaya inatakiwa kupata maji
kwa asilimia 85, ninyi mtatoa asilimia 46, sasa SUWASA mkae na
Wataalamu wa Wizara husika ya Maji muandae utaratibu ukae tayari tayari
juu ya namna gani ya kuweza kukimbiza huu mradi, watu wamechoshwa na
subiri subiri hata waswahili wanasema ngoja ngoja yaumiza matumbo,”
Alisisitiza.
Ameyasema hayo alipotembelea mradi
wa uboreshaji wa huduma ya maji safi unaoendelea kujengwa katika mji
mdogo wa Namanyere ili kujionea maendeleo ya mradi huo pamoja na kujua
changamoto zinazoukabili na hatimae kuona namna ya kuupatia ufumbuzi
huku akiwa ameambata na kamati ya ulinzi na Usalama ya mkoa pamoja na
wataalamu wengine kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa.
Awali akisoma taarifa ya mradi huo
meneja wa SUWASA Mhandisi Gibon Nzowa alisema kuwa shida inayosababisha
mradi huo kutofikia asilimia 85 ya upatikanaji wa maji katika mji huo
ni kutokana na kutokuwepo kwa mtandao wa kuyasambaza maji hayo kwa
kilomita 15 lakini maji yalipo katika chanzo yanatosheleza kwa asilimia
85 endapo tatizo la mtandao litatuliwa na kisha kueleza shughuli za
mradi huo.
“Kazi zinazotekelezwa ni ununuzi
na ufungaji wa pampu mbili za kusukumia maji, ulazaji wa bomba kuu
kutoka bwawa la mfili hadi kwenye tenki takriban kilomita 3.7, pia
ujenzi wa tenki la lita 500,000 ambalo limeinuliwa kwa mita 12 ili
kuwezesha maeneo mengi ya Namanyere kupata maji, ulazaji wa mtandao wa
usambazaji maji kwa kilomita 6.5, vile vile katika mradi huu kutakuwa na
dira za maji za kuunganishia wateja,” Alimalizia
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Nkasi Mh. Said Mtanda wakati akielezea hatua walizochukua kupambana
kumaliza tatizo hilo la upatikanaji wa maji katika mji wa Namanyere
alisema kuwa kama wilaya walikaa na kuandika andiko na kuhitaji Shilingi
Bilioni 2.5 na kuliwasilisha wizarani ambapo fedha hiyo ilipunguzwa
hadi kufikia shilingi Bilioni 1.5 hali iliyopunguza asilimia ya
upatikanaji wa maji katika mji huo.
“Tulitafuta wataalamu wakaandika
huu mradi, wakaleta kwangu tukapitia tukaona ni mradi wa Shilingi
bilioni 2.5 ambayo hiyo ingetuwezesha kusambaza maji maeneo yote yenye
upungufu wa maji katika mji wetu, kwahiyo Waziri alipokuja tulimkabidhi
akasema tuwape SUWASA nao baada ya kuipiti walipeleka wizarani ambapo
wakapunguza kiwango cha fedha, huu mradi ulikuwa ni wa Bilioni 1.8
lakini Mheshimiwa waziri akasema ipungue hadi kufikia shilingi bilioni
1.5 lakini kama ingekuwa ule mradi wetu wa Shilingi bilioni 2.5
tungekuwa na mtandao wa kilomita 15 kuliko huu wa sasa wa kilomita 6,”
alisema.
Mradi huo wa uboreshaji wa huduma
ya maji safi katika mji wa Namanyere unatarajiwa kumalizika mwezi Mei
mwaka 2020 na kugharimu shilingi Bilioni 1.58 fedha zinazotolewa na
serikali huku ukitarajiwa kuhifadhi maji kutoka lita 350,000 hadi lita
850,000 na kufikia asilimia 46 ya uaptikanaji wa maji katika mji huo.
0 comments:
Post a Comment