Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Prof. Faustine Kamuzora akieleza jambo wakati wa sherehe za kuhitimu mafunzo ya Ushirika kwa Viongozi na Watendaji wa Ushirika. Mafunzo kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) kwa njia ya Masafa Sherehe zilizofanyika Bukoba, Kagera hivi karibuni.
Mrajis wa Vyama vya
Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege
akieleza masuala ya Sekta ya Ushirika wakati wa sherehe za kuhitimu mafunzo ya
Ushirika kwa Viongozi na Watendaji wa Ushirika.
Sehemu
ya Wahitimu wa mafunzo ya Ushirika Wakati wa sherehe za kuhitimu mafunzo kwa
njia ya Masafa zilizofanyika Bukoba, Kagera hivi karibuni.
Elimu
ya Fedha imetajwa kuwa moja ya nyenzo muhimu katika kuimarisha na kuendeleza
Ushirika kwa lengo la kuunga mkono jitihada za Serikali za kuondoa umaskini na
kuinua uchumi wa Wananchi.
Hayo
yamesemwa na Mgeni rasmi Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Prof. Faustine
Kamuzora wakati wa Sherehe zilizofanyika Bukoba Mkoani Kagera kukabidhi Vyeti kwa Wahitimu wa Programu za
mafunzo ya Uongozi na Usimamizi pamoja
na Utunzaji wa Hesabu za Vyama vya Ushirika kwa njia ya masafa. Mafunzo
yaliyokuwa yakitolewa na kuratibiwa na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi kwa
viongozi wa Vyama vya Ushirika wa mikoa ya Kagera, Tabora, Geita na Simiyu.
Akiongea
katika Sherehe hizo Prof. Kamuzora amewataka Wahitimu hao ambao wengi wao ni
Viongozi wa Vyama vya Ushirika kutumia elimu waliyopata katika kusimamia Vyama
vya Ushirika kwa weledi ili kulinda maslahi ya Wanachama wa Ushirika.
Akisisitiza suala la Viongozi hao kutumia elimu ya fedha waliyopata kuongeza na
kubuni mbinu mbalimbali za kuongeza vipato kwa Vyama vyao vya Ushirika
wanavyosimamia.
“Hakikisheni
mnaendelea kuitumia elimu ya Fedha mliyoipata kwaajili ya kuimarisha na
kuongeza mapato ya Vyama vya Ushirika na elimu hiyo mkawashirikishe Wanachama
katika Vyama vyenu vya Ushirika” alisema Prof. Kamuzora
Mrajis
wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt.
Benson Ndiege katika hotuba yake amewataka Viongozi waliopata mafunzo ya
Ushirika kwenda kuleta mabadiliko chanya katika Vyama wanavyosimamia,
akisisitiza utendaji utakaondoa changamoto za ubadhilifu na Hati zisizoridhisha
ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara.
“Moja
ya sababu ambazo zimekuwa zikileta changamoto katika Sekta ya Ushirika ni
watendaji na Viongozi kutokuwa na uelewa sahihi wa namna bora ya utunzaji wa
hesabu na Kumbukumbu za Vyama vya Ushirika, ni imani yangu mafunzo haya
yanakwenda kuongeza ufanisi na Hati safi kwa Vyama vyetu,” alisema Mrajis
Aidha,
Mrajis ametoa wito kwa Wanawake wengi kushiriki nafasi mbalimbali za Uongozi wa
Vyama vya Ushirika hususani wakati huu ambao Vyama vingi vya Ushirika
vinakwenda kufanya Uchaguzi wa nafasi za Uongozi ikiwemo Wajumbe wa Bodi,
Mameneja na Watendaji wengine.
“Ushirika
ni Sekta ambayo inahitaji kutekeleza na kuonesha usawa wa Kijinsia kwa vitendo
kwa kuwa na viongozi wanawake katika Vyama vyetu vya Ushirika kwani wanawake
ndio msingi na walezi wa familia na Jamii kwa ujumla,” alisisitiza Mrajis
Mrajis
Ndiege pia amewataka Warajis Wasaidizi wa Mikoa kwa kushirikiana na Maafisa
Ushirika wa Wilaya katika Mikoa mingine kuendelea na jitihada za kujiendeleza
kimaarifa hususani katika masuala ya Uandishi mzuri wa Vitabu vya Ushirika mara
baada ya msimu wa mazao ili kuondokana na dosari mbalimbali zinazoleta taswira
hasi kwa Sekta ya Ushirika.
Kwa
upande wake Mkuu wa Chuo cha Ushirika Moshi (MoCU) Prof. Alfred Sife alieleza
kuwa mafunzo hayo awali yalikuwa yakifanyika kwa njia ya Posta, ambapo hivi
sasa kutokana na maendeleo ya kiteknolojia mafunzo ya Ushirika yanafanyika kwa
masafa. Mkuu huyo alifafanua kuwa utoaji huo wa elimu ni miongoni mwa mikakati
ya Chuo hicho katika kuhakikisha wigo wa upatikanaji wa elimu unaongezeka na
Vyama vya Ushirika vinakuwa imara zaidi kwa kuwafikishia mafunzo mahali walipo.
Baadhi
ya masuala yaliyotajwa kuwa ni sehemu ya mafunzo hayo ni pamoja uelewa wa dhana
ya Ushirika, Misingi ya Ushirika, Uongozi wa Asasi za Ushirika, Kanuni za
Utunzaji wa Mahesabu ya Ushirika, uchanganuzi wa Ushirika wa mazao, utunzaji
Kumbukumbu pamoja na mada nyingine zenye kuongeza tija ya utendaji wa Vyama vya
Ushirika.
Katika Sherehe hiyo jumla ya Viongozi 120 wamehitimu mafunzo hayo ya Ushirika na kukabidhiwa Vyeti vya kumaliza mafunzo. Akisoma risala kwa niaba ya Wahitimu Mjumbe wa Bodi KDCU Bw. Fidolin Kasenene ameshukuru Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi pamoja na Wadau wa Ushirika waliofanikisha mafunzo hayo, huku akiomba mafunzo kama hayo yawe endelevu ili kuongeza ufanisi na usimamizi bora wa Vyama vya Ushirika nchini.
0 comments:
Post a Comment