METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, November 20, 2020

Rukwa wazindua msimu wa kilimo huku zaidi ya tani milioni 1.5 za mazao zikitegemewa kuzalishwa 2020/2021

 

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (aliyeinua mkono) alipowasha trekta katika shamba la mfano kuashiria kuzindua msimu wa kilimo pamoja na kufungua matumizi ya zana bora na za kisasa za kilimo katika mkoa. 

Wakati mvua zikiendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi, wakulima wa Mkoa wa Rukwa leo tarehe 19.11.2020 wameshuhudia uzinduzi wa msimu wa kilimo wa mwaka 2020/2021 katika hafla fupi iliyofanyika katika Kata ya Ntendo, Manispaa ya Sumbawanga.

 

Uzinduzi huo uliofanywa na mgeni rasmi wa hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa kilimo wakiwemo wauzaji wa zana za kilimo, mbolea, mbegu na miche ya mazao ya Korosho na mibuni ambayo ni mazao kimkakati katika mkoa.

 

Wakati akiwahutubia wananchi waliohudhuria uzinduzi huo Mh. Wangabo alisema kuwa mkoa umepania kuongeza hekta za kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mazao hasa zao la Mahindi ambalo ndio zao kuu la chakula na biashara katika mkoa akitoa msukumo katika kilimo cha mazao mengine ya kimakati yakiwemo Alizeti, Kahawa, Korosho na Michikichi yatakayongeza wigo wa mazao ya kibiashara.

 

Kati ya eneo litakalo limwa katika msimu wa mwaka 2020/2021, jumla ya  hekta 483,380.63 ni kwa ajili ya kilimo cha mazao ya chakula na hekta 58,797.04 ni kwa ajili ya kilimo cha mazao ya biashara. Aidha, Jumla ya tani 1,568,067.67 za mazao zinategemewa kuzalishwa. Ambapo tani 1,464,140.63 ni za mazao ya chakula na tani 103,927.04 za mazao ya biashara. Malengo ya uzalishaji ya mwaka huu ni sawa na ongezeko la asilimia 22 ya uzalishaji wa mwaka uliopita wa 2019/2020

 

Katika msimu wa 2020/2021 jumla ya hekta 100.8 zinatarajiwa kupandwa miche ya Kahawa 252,000. Aidha, kwa upande wa Alizeti Mkoa unalenga kulima hekta 52,371.9 ambazo zitazalisha tani 60,205.88 na katika msimu wa Mwaka 2020/2021 Mkoa umeagiza kiasi cha tani 3.5 za mbegu ya korosho kutoka Bodi ya Korosho Tanzania ambazo zitaoteshwa kwenye vitalu. Kiasi hicho cha mbegu kitatosha kupanda eneo la ekari 125.” Alisema.

 

Kwa upande wake Mrajis wa vyama vya ushirika mkoa wa Rukwa Benjamin Mwangwala akieleza mipango ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania alisema kuwa tume hiyo imeendelea kutekeleza mpango wa kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali nchini kwa kumsaidia mkulima na vyama vya ushirika kuongeza kipato kwa kuongeza kiwango cha uzalishaji kwa kutumia zana bora za kilimo.

 

“Vyama vya Ushirika vipatavyo 45 vilifanikiwa kufikia matakwa ya masharti ya kupata mkopo wa matrekta kupitia Mikutano Mikuu ya Vyama vya Ushirika. Miongoni mwa masharti ni pamoja na kuwa na taasisi iliyosajiliwa kisheria, kutoa malipo ya awali ya asilimia 25 ya thamani ya zana hitajika. Aidha, kwa mtu mmoja mmoja ni lazima awe mwanachama wa Chama cha Ushirika,” Alisema.

 

Aidha aliongeza kuwa Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na serikali ya awamu ya tano wakulima hao wanakabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo suala la kukosa mfuko maalum wa pembejeo jambo linalochangia Chama Kikuu cha Ushirika Mkoani Rukwa kukosa dhamana ya kuagiza mbolea kwa kutumia mfumo wa Uagizaji wa Pamoja kama serikali ilivyoelekeza.

 

Mahitaji ya Pembejeo za kilimo Mkoani Rukwa kwa msimu wa Mwaka wa 2020/2021 ni tani 26,152 za mbolea ambapo DAP tani 10,164.00, UREA tani 9,402.00, CAN tani 3,044.00, NPK tani 2,143.50 na SA tani 1,398.50.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com