Serikali kupitia Balozi wa Tanzania nchini Ubeligiji na Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Ulaya imesema kuwa Bunge la Umoja wa Ulaya halijatoa azimio lolote kuhusu Tanzania kupitia kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje ya Bunge hilo.
Akizungumza
mapema leo kupitia televisheni ya Taifa (TBC), Balozi wa Tanzania nchini Ubeligiji na Mwakilishi wa Tanzania katika
Umoja wa Ulaya Jestus Nyamanga alisema kuwa kuna taarifa za upotoshaji na
zisizo na ukweli wowote zinazosambazwa
kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii
zikidai kuwa Bunge la Umoja wa Ulaya jana Novemba 19 limeazimia kusitisha
misaada na mikopo kutoka umoja huo na mashirika yake, kwa nchi ya Tanzania
sambamba na kuiwekea vikwazo.
Halikadhalika
taarifa hizo za upotoshaji zinadai kwamba Bunge hilo la Umoja wa Ulaya
limeazimia kuiwekeza vikwazo Tanzania na kuzuia kuuza bidhaa zake katika nchi
za Umoja wa Ulaya.
“Novemba
19 asubuhi hapa Ubeligiji, Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje ya Umoja wa Ulaya
ilikutana katika kikao chake cha kawaida, moja ya masuala yaliyojadiliwa
ilihusu Tanzania na hali ilivyo baada ya Uchaguzi Mkuu kukamilika, huu ni
utaratibu wa kawaida kabisa wa Kamati
hiyo kuijadili nchi ambayo ni mdau wao mkubwa wa maendeleo
mara tu baada ya Uchaguzi Mkuu kukamilika”, alisema Balozi Nyamanga
Balozi
Nyamanga alifafanua kuwa kikao hicho ni kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya
Nje na si Bunge lote na hata hivyo kikao hicho kilitoa nafasi kwa wabunge kutoa
mawazo yao na kujadili kuhusu hali ya Tanzania baada ya Uchaguzi Mkuu ambapo ni wabunge watano tu
ndio walitoa mawazo yao kati ya wabunge 71 wa Kamati hiyo. Ambapo hilo lina
idadi ya wabunge 705 na hivyo halijatoa azimio lolote kuhusu
Tanzania.
Alibainisha
kuwa pia kuna taarifa ambazo si za kweli
zinazoenezwa na watu wenye nia mbaya na
Tanzania zikidai kwamba Bunge hilo la Umoja wa Ulaya limeazimia kuifutia
Tanzania msaada wa euro milioni 626
ambazo Tanzania inapewa na Umoja wa Ulaya kila mwaka, si kweli kwamba Umoja huo
unaipa Tanzania fedha hizo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi. Aidha Serikali
inaendelea kutekeleza miradi yake mbalimbali.
“Hakuna
mjadala wala majadiliano yanayoendelea katika Umoja wa Ulaya wala hakuna azimio lililowekwa na Kamati hiyo ya Bunge,
wala kuizuia Tanzania kuuza bidhaa zake katika nchi hizo za Umoja wa Ulaya,
hata hivyo naomba niwahakikishie watanzania wenzangu kwamba uhusiano wa Tanzania
na Umoja wa Ulaya ni mzuri sana kwa zaidi ya miaka 45 sasa na tunaendelea
kushirikiana katika masula mbalimbali
yanayohusu maendeleo kwa pande zote mbili”, alisema Balozi Nyamanga.
0 comments:
Post a Comment