
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
ameipongeza timu ya kandanda ya Taifa, Taifa Stars kwa kufanikiwa
kuiondoa Harambee Stars katika mashindano ya CHAN 2020 na kuiondoa
Burundi na kufanikiwa kuingia hatua ya makundi ya kufuzu Kombe la Dunia
huko Doha, Qatar 2022.
Pia, Waziri Mkuu ameipongeza
timu ya Taifa ya Wanawake chini ya Umri wa Miaka 20 (Maarufu Tanzanite)
kwa kutwaa kombe la mpira wa Miguu kwa Nchi za COSAFA huko Port
Elizabeth, Afrika ya Kusini.
Waziri Mkuu ametoa pongezi
hizo leo (Ijumaa, Septemba 13, 2019) , wakati akiahirisha mkutano wa 16
wa Bunge la 11, Bungeni jijini Dodoma. Amesema hatua hiyo ni nzuri
na muhimu kwani inaiweka timu katika nafasi nzuri kushiriki fainali za
mashindano hayo.
Amesema timu ya Taifa itarudi
dimbani kupambana na Sudan tarehe 22 Septemba, 2019 kwenye Uwanja wa
Taifa. “Kama kawaida yetu twenda tukaujaze Uwanja wetu wa Taifa na
kuishangilia kwa nguvu timu yetu ya Taifa.”
Vilevile, Waziri Mkuu
amevipongeza vilabu vya Azam, Malindi na Yanga kwa kufanikiwa kusonga
mbele kuingia hatua ya pili katika michuano ya vilabu ya Shirikisho la
Soka Barani Afrika (CAF).
“Kwa vilabu vya KMC, KMKM na
Simba, ambavyo vimeondolewa katika hatua ya mwanzo kabisa, vichukulie
hali hiyo kama changamoto ya kujitathmini na kujiandaa kwa ajili ya
michezo ya ndani na mashindano yajayo ya kimataifa badala ya kutumia
muda mrefu kujadili kuhusu kutolewa mapema.”
Akizungumzia kuhusu mchezo wa
masumbwi, Waziri Mkuu amesema bendera ya Tanzania imeendelea
kupeperushwa vyema kufuatia wana masumbwi wengine wawili wa Kitanzania
kuendelea kufanya vizuri katika medani za Kimataifa.
“Nitumie nafasi hii
kuwapongeza mwanamasumbwi Abdallah Shaaban Pazi maarufuDullaMbabe kwa
kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Dunia wa WBO baada ya kumpiga kwa knockout
kwenye raundi ya tatu mpinzani wake Mchina anayejulikana kwa jina la
Zulipikaer Maimaitiali.”
Pia, Waziri Mkuu amempongeza
mwanamasumbwi mwingine wa Kitanzania Bruno Tarimo (maarufuvifuaviwili)
kwa kumnyoosha mpinzani wake Mserbia, Scheka Gurdijeljac kwenye pambano
la ubingwa wa Dunia lililofanyika mwanzoni mwa mwezi huu huko Serbia.
“Hongereni sana wanamichezo
wetu na endeleeni na moyo huo wa kizalendo mliouonesha katika
kuipeperusha vema bendera ya Taifa letu.”
Mbali na kuwapongeza
wanamasumbwi hao, pia, Waziri Mkuu amempongezaMiss Tanzania 2019, Sylvia
Bebwa pamoja na Queen Magese aliyeshika nafasi ya pili na Greatness
Nkuba aliyeshika nafasi ya tatu.
“Tunamtakia matayarisho mema
Miss Tanzania ili akapeperushe vema Bendera ya Taifa letu nchini
Uingereza kwenye mashindano ya Urembo ya Dunia (Miss World) ambako pia
ataitangaza nchi yetu na vivutio vya utalii tulivyonavyo.
Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iendelee kuratibu vizuri shughuli
za michezo, utamaduni na sanaa ili zilete ufanisi wa hali ya juu na pia
kuweka msisitizo sambamba na kuwa na mikakati ya kuendeleza michezo
ikiwemo shuleni, vituo maalumu vya michezo na kuwa na mifumo mizuri ya
upatikanaji wa fedha.
0 comments:
Post a Comment