METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, September 19, 2019

MPANGO KAZI WA TAIFA WA KUTOKOMEZA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO WAJADILIWA

Mratibu Taifa wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) Bi. Happiness Mugyabuso akifungua kikao kazi cha kujadili na kufanya tathimini ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kwa kipindi cha robo ya kwanza 2019/2020 kilichofanyika katika Ukumbi wa Bwalo JKT UMWEMA mkoani Morogoro.
Konstebo wa Polisi Bi. Tunu Mohamed akieleza kuhusu takwimu za madawati ya jinsia na watoto yaliyopo katika vituo vya polisi nchini  wakati wa kikao kazi hicho.
Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Bi.Juliana Tarimo akifafanua jambo wakati wa kikao kazi hicho.
Afisa Takwimu Munir Mdee kutoka Ofisi ya TAKWIMU akifafanua jambo kuhusu masuala ya takwimu wakati wa kikao hicho.
Bi. Juliana Ntukey akiongoza majadiliano katika kazi za vikundi wakati wa kikao kazi hicho.
Mratibu Taifa wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) Bi. Happiness Mugyabuso pamoja Bw.Emmanuel Burton ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii wakijadili jambo wakati wa kikao hicho.
Mwenyekiti (ambaye ni kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango) Wizara Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Bi. Sophina Mjangu akizungumza jambo wakati wa Kikao kazi cha kujadili na kufanya tathimini ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kwa kipindi cha robo ya kwanza 2019/2020 kilichofanyika katika Ukumbi wa Bwalo JKT UMWEMA mkoani Morogoro tarehe 19 Septemba, 2019.
 (PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
******************************
NA.MWANDISHI WETU
WADAU wa masuala ya Wanawake na Watoto wamekutana ili kujadili na kufanya tathimini ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kwa kipindi cha robo ya kwanza 2019/2020.
Akizungumza wakati akifungua kikao kazi hicho cha siku mbili kuanzia Septemba 18 hadi 19, 2019 kilichofanyika katika Ukumbi wa Bwalo la JKT UMWEMA mkoani Morogoro Mratibu wa Taifa wa Mpango huo Bi. Happiness Mugyabuso amesema, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo wameandaa kikao kazi hicho ili kujadili na kufanya tathimini ya utekelezaji wa Mpango Kazi huo.
 “Leo tumekutana hapa kwa pamoja kwa lengo la kufanya tathimini ya utekelezaji wa mpango kazi huo katika kipindi cha robo ya kwanza kwa Mwaka 2019/2020. Aliongezea kuwa, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika robo ya kwanza ya utekelezaji wa Mpango Kazi, kikao kazi kitajadili pia changamoto zilizojitokeza katika kipindi husika na kuweka mikakati mahsusi ya kuimarisha utekelezaji wake kwa vipindi vya robo zinazofuata,”alisema Bi. Happiness.
Aidha kikao hicho kilitoa fursa ya kujadili namna bora ya kuboresha mfumo wa ukusanyaji na uchakataji wa taarifa za takwimu za utekelezaji wa MTAKUWWA ili kuimarisha upatikanaji wa takwimu za msingi (baseline data). Hatua hii ni muhimu kwani itasaidia kupima hali ya utekelezaji wa Mpango Kazi katika vipindi mbalimbali vikiwemo vya mwaka na miaka mitano (5).
Mmoja wa washiriki wa kikao hicho Bw.Emmanuel Burton ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii alieleza kuwa, Miongoni mwa maeneo yaliyojadiliwa ni pamoja na namna bora ya upatikanaji wa taarifa sahihi za utekelezaji katika sekta mbalimbali ambazo zinatekeleza mpango huo na kuwa na mikakati ya namna ya kuwafikia walengwa kikamilifu ili kukidhi lengo mpango ifikapo mwaka 2021/ 2022.
“Kikao kazi hiki ni muhimu kwa kuzingatia kuwa, malengo mahsusi ya utekelezaji wa Mpango wa MTAKUWWA yanajadiliwa na kuhakikisha tunaandaa taarifa sahihi zenye tija kuhusu makundi hayo ili vita dhidi ya ukatili wa wanawake na watoto inapiganwa na kuleta matokeo chanya,”alisema Burton
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com