Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Vietnam
nchini, Mhe. Nguyen Doanh, ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar
es salaam, Julai 3, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Balozi wa Vietnam
nchini, Mhe. Nguyen Doanh, ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni jijini
Dar es salaam, Julai 3, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………….
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na
Balozi wa Vitemam nchini, Mhe. Nguyen Doanh ambapo amewakaribisha
wafanyabiashara kutoka Vietnam waje nchini kuwekeze katika sekta
mbalimbali ikiwemo ya viwanda.
Amesema Rais Dkt. John Magufuli ameanzisha Wizara ya Uwekezaji iliyo
chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya kuifanya Tanzania kuwa ni
mahali bora na salama kwa wawekezaji na wafanyabiashara.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Julai 3, 2019), wakati
akizungumza na Balozi wa Vitemam nchini, Balozi Doanh. Mazungumzo hayo
yamefanyika kwenye Ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar Es
salaam.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaalika wafanyabiashara na
wawekezaji kutoka nchini Vietnam waje kuwekeza katika sekta ya viwanda
hususani vile vinavyotumia malighafi za mazao ya kilimo yanayolimwa hapa
nchini. Hatua hiyo itawawezesha wakulima wa Tanzania kuwa na soko la
uhakika la mazao yao.
“Serikali imeendelea kuondoa vikwazo vya kuanzisha
na kuendesha biashara kwa kupitia upya sheria, kanuni na taratibu za
biashara na kuzifuta zile ambazo zimethibitika kuwa zinayafanya
mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kuwa magumu.”
Waziri Mkuu amesema kwa kuwa nchi ya Vietnam imepiga hatua kubwa
katika ujenzi na uendeshaji wa viwanda vya nguo, Tanzania ingefurahi
kuona kwamba viwanda vya aina hiyo vinajengwa hapa nchini na wawekezaji
kutoka nchi hiyo.
Amesema kuwa ununuzi wa mazao ya kilimo kama vile pamba, koroshao,
kahawa na tumbaku ni fursa nyingine ya kibiashara ambayo wafanyabiashara
wa Vietnam wanakaribishwa kuichangamkia hapa nchini.
Akizungumzia kuhusu soko la korosho Waziri Mkuu amesema Tanzania ina
korosho za kutosha na inawakaribisha wafanyabiashara kutoka Vietnam
waje kuzinunua. Kwa wale wenye uwezo wa kujenga viwanda vya kuchakata
korosho nao amewakaribisha na kuahidi kuwa Serikali iko tayari wakati
wote kuwasaidia.
Kwa upande wake, Balozi Doanh alitumia fursa hiyo
kumweleza Waziri Mkuu juu wa ujio wa Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam, Mhe.
Trinh Dinh Dung anayetarajiwa kufanya ziara yake ya kikazi
nchini kuanzia Julai 9 hadi 11 mwaka huu.
Alisema Naibu Waziri Mkuu huyo anatarajiwa kuambatana na wafanyabiashara wasiopungua 20 kutoka kampuni kubwa za nchini Vietnam.
Nchi za Vietnam na Tanzania zilianzisha uhusiano wa kidiplomasia
mwaka 1965. Mwaka 1984, Vietnam ilifungua ofisi ya Ubalozi wake hapa
nchini kwa muda na kuufungua upya mwaka 2003.
0 comments:
Post a Comment