Rais Mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Benjamin Mkapa akikata utepe kuashiria uzinduzi
wa safari ya miaka mitano ya Chuo Kikuu cha Mt. Augustino cha Tanzania
(SAUT) kuelekea Jubilei ya miaka 25 tangu kuanzishwa hicho mwaka 1998.
Uzinduzi huo umefanyika kwa kuweka jiwe la msingi katika jengo la ukumbi
wa mikutano unaojengwa kwa matumizi ya kitaaluma na kijamii. Wa pili
kushoto ni wa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha SAUT na Askofu wa Jimbo Katoliki la
Geita Askofu Flavian Kassala na Makamu wa Mkuu wa Chuo Balozi Prof.
Costa Ricky Mahalu (wa tatu kutoka kulia).
Rais Mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Benjamin Mkapa akiongea na wageni waalikwa
wakati wa uzinduzi wa safari ya miaka mitano ya Chuo Kikuu cha Mt.
Augustino cha Tanzania (SAUT) kuelekea Jubilei ya miaka 25 tangu
kuanzishwa hicho mwaka 1998.
Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu
Tanzania (TEC) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha SAUT na
Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita Askofu Flavian Kassala akiongea na
wageni waalikwa wakati wa uzinduzi wa safari ya miaka mitano ya Chuo
Kikuu cha Mt. Augustino cha Tanzania (SAUT) kuelekea Jubilei ya miaka 25
tangu kuanzishwa hicho mwaka 1998.
Rais Mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Benjamin Mkapa (kulia) akisalimia na Makamu wa
Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Baraza la Chuo cha SAUT na Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita Askofu
Flavian Kassala (kushoto) wakati wa uzinduzi wa safari ya miaka mitano
ya Chuo Kikuu cha Mt. Augustino cha Tanzania (SAUT) kuelekea Jubilei ya
miaka 25 tangu kuanzishwa hicho mwaka 1998.
Rais Mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Benjamin Mkapa (kulia) akipata maelezo kutoka
mmoja wa wanachuo wa SAUT wakati wa maonesho ya kitaaaluma chuoni hapo.
Baadhi ya washiriki wa hafla ya uzinduzi
wa miaka 20 na safari ya miaka mitano ya Chuo Kikuu cha Mt. Augustino
cha Tanzania (SAUT) kuelekea Jubilei ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwake
mwaka 1998.
(Picha na Gehaz Makoga na Abubakari Yusuf-SAUT)
…………………………
Na Eleuteri Mangi-SAUT
Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania
(SAUT) kimezindua safari ya miaka mitano kuelekea Jubilei ya miaka 25
tangu kuanzishwa kwake mwaka 1998.
Uzinduzi huo umefanywa na Rais Mstaafu wa
Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin Mkapa
uliofanyika chuoni hapo kwa kuweka jiwe la msingi katika jengo la ukumbi
wa mikutano unaojengwa kutumika kwa shughuli mbalimbali za kitaaluma na
kijamii.
Akiongea na hadhira ya viongozi
mbalimbali, wahadhiri, wanafunzi pamoja na wananchi waliohudhuria
katika tukio hilo liliotanguliwa na ibada ya misa takatifu iliyongozwa
na Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha SAUT na Askofu wa Jimbo Katoliki
la Geita Askofu Flavian Kassala, Rais Mstaafu Mkapa amesema kuwa vyuo
vikuu vya binafsi vinamchango mkubwa nchini katika kutoa elimu kwa
Watanzania bila kujali dini zao wala makabila yao hatua ambayo itawaweze
kutoa mchango katika kutekeleza Sera ya Maendeleo ya Taifa ya kuwa nchi
ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Kuhusu Sera ya Maendeleo ya Taifa, Rais
Mstaafu Mkapa amesema kuwa elimu ya juu ina mchango kwa taifa kwa
kuzalisha wataalam wengi wenye ubora, ujuzi na uwezo wa kutatua matatizo
ya jamii, kukabiliana na changamoto za maendeleo ili kufikia ushindani
katika ngazi za kikanda na za kimataifa.
“Serikali inatambua na inathamini mchango
wa sekta binfsi katika vyuo vikuu kwa kutoa elimu nchini, vyuo vikuu
binafsi vina nafasi ya kuzalisha wataalamu mbalimbali kwa manufaa kwa
mtu mmoja mmoja, jamii, taifa na hata nje ya mipaka ya Tanzania.”
amesema Rais Mstaafu.
Katika kukuza na kupanua wigo wa kutoa
elimu ya juu nchini, Rais Mstaafu Mkapa atakumbukwa kwa mchango wake wa
kuwezesha dini mbalimbali nchini kuwa na vyuo vikuu vyake ikiwemo Chuo
Kukuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT) kinachomilikiwa na Baraza
la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Chuo Kikuu cha Kiislamu cha
Morogoro (MUM) kinachomilikiwa na Kinachomilikiwa na Baraza la Waislam
Tanzania, Chuo Kikuu Cha Mt. John Dodoma kinachomilikiwa na Kanisa la
Waangikana Tanzania, Chuo Kikuu cha Tumaini kinachomilikiwa na Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania pamoja na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu cha
Sebastian Kolowa.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Baraza
la Maaskofu Tanzania (TEC) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo
cha SAUT na Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita Askofu Flavian Kassala
ameishukuru Serikali ya Tanzania kuwa msaada kwa kwa sekta binafsi
ambapo baraza hilo linathamini na linaiunga mkono Serikali kwa kutoa
elimu nchini ili wanaoipa waweze kutoa msaada kwa watu wanaohitaji
msaada huo kwa wakati.
“Kanisa linatoa shukrani kwa Serikali,
watu binafsi na taasisi zinazoendelea kutoa mchango kwa SAUT, elimu
tunayotoa katika ngazi zote imewasaidia watu kutatua matatizo katika
mazingira yao” amesema Askofu Kassala.
Aidha, Askofu Kassala aliendelea kusema
“Tunajenga watu ambao wanazingatia maadili na utu wa mtu kwa kusaidia
jamii inayohitaji msaada kutoka kwa watu ambao wamepata elimu, SAUT
inamchango mkubwa katika kuwajenga na kuwalea watu kiroho na kimwili
kupitia elimu” alisisitiza Askofu Kassala.
Naye Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho Balozi
Prof. Costa Ricky Mahalu amesema chuo chao kinaendelea kuzalisha
wataalam kwa kwa ajili ya nchi hatua ambayo amemshukuru Rais Mstaafu
Benjamin Mkapa kuwa mlezi na msaada mkubwa kwa maendeleo ya SAUT.
Balozi Prof. Mahalu amesema kuwa
wataalamu wanaoandaliwa katika chuo hicho watokana na vitivo vingine
vinne (4) ambavyo ni Kitivo cha Sayansi ya Jamii na Mawasiliano ya Umma,
Kitivo cha Biashara na Utawala, Kitivo cha Ualimu, Kitivo cha Sheria na
Kitivo cha Uhandisi.
Hatua hiyo imeungwa mkono na Waziri wa
Madini Dotto Biteko ambapo alitoa wito kwa Wanzania na wanafunzi
wanaosoma na wanaotarajia kujiunga na chuo hicho kuwa katika utoaji wa
elimu ya juu SAUT imejipambanua kuwa ni kinu cha kuandaa wanataaluma na
viongozi mbalimbali nchini.
“Tunabahati ya kuzaliwa kwenye nchi yenye
usawa na haki, SAUT inatoa haki ya elimu kwa vijana wetu hatua
inayowapelekea kuhama kwenye taifa la kulalamika na kuwa taifa la watu
wa matokeo, tunathamini kazi inayofanywa na chuo hiki ambacho kimekuwa
kuwa chachu ya malezi kwa kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.”
Alisisitiza Waziri Biteko.
Chuo Kikuu cha SAUT kinamilikiwa na
kusimamiwa na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kimeanzishwa kwa mujibu
wa sheria za nchi na kinafanya kazi chini ya Tume ya vyuo vikuu Tanzania
(TCU) kwa mujibu wa masharti ya vyuo vikuu sheria namba 7 ya mwaka 2005
ambapo awali kilikuwa kinajulikana kama Chuo cha Maendeleo ya Jamii
Nyegezi (NSTI) kilichoanzishwa tangu mwaka 1960 na wamisionari wa kanisa
katoliki ambao kwa sasa wanajulikana kama Wamisionari wa Afrika wakiwa
chini ya Askofu Joseph Blomjous wa Jimbo Kuu la Mwanza.
0 comments:
Post a Comment