Na Asha Said, DAR ES SALAAM
LIGI Kuu ya soka Tanzania Bara inatarajiwa kuanza Agosti 23, mwaka huu
wakati watani wa jadi, Simba na Yanga watamenyana Januari 4, mwakani.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Boniface Wambura amesema
hayo leo katika mkutano na Waandishi wa Habari mjini Dar es Salaam
kwamba.
Wambura amesema kwamba Ligi Kuu itafunguliwa kwa mchezo wa Ngao ya Jamii
kati ya mabingwa watetezi, Simba SC dhidi ya Azam FC washindi wa Kombe
la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports
Federation Cup (ASFC) Agosti 17, mwaka huu.
Alisema Ligi itafunguliwa rasmi Agosti 23, Simba ikianza kutetea taji na
kuwania ubingwa wa tatu mfululizo kwa kucheza na JKT Tanzania, huku
watani wao, Yanga wakifungua dimba na Ruvu Shooting ya Pwani.
Alisema upangaji wa ratiba ya Ligi hiyo
umezingatia michuano mbalimbali ya kimataifa kwa upande wa timu za taifa
na klabu za Simba, Yanga, Azam na KMC.
“Ratiba imepangwa kwa kuangalia mechi zote za Kimataifa, hakutakuwa na
upanguaji wa mechi. Ikiwa ni pamoja na kila timu ijue haitakubaliwa
kubadilishwa mechi zote zitachezwa kama zilizopangwa,” amesema Wambura.
Aidha, Wambura alisema kupunguzwa gharama kwa klabu zitakuwa zikicheza
mechi zake kwa timu za mkoa mmoja kwa mfulululizo na si kwenda na
kurudi.
0 comments:
Post a Comment