
**********************
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuweka
mazingira wezeshi ya kuvutia uwekezaji na biashara.
Amesema mpaka sasa, hatua
mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi
ya uwekezaji na biashara nchini.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Juni
27, 2019) jijini Dodoma wakati akifungua kongamano la uwekezaji la mkoa
wa Dodoma kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.
”Miongoni mwa hatua hizo ni uwepo
wa usafiri wa uhakika na wa haraka wa abiria na mizigo kwa kujenga reli
ya kiwango cha kimataifa (Standard GaugeRailway).”
Pia, Waziri Mkuu amesema uwanja wa ndege wa Dodoma umeboreshwa na kuruhusu ndege kubwa na ndogo kutua usiku na mchana.
”Mashirika ya ndege yanayotoa
huduma yameongezeka na maandalizi ya awali ya ujenzi wa uwanja wa
kimataifa wa ndege katika eneo la Msalato yanaendelea.”
Waziri Mkuu amesema mkoa wa Dodoma
una barabara za kuaminika za kiwango cha lami zinazoiunganisha na mikoa
mingine pamoja na nchi jirani.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano
imeendelea kuboresha huduma za afya na Dodoma kuna hospitali ya Benjamin
Mkapa yenye uwezo kama wa Muhimbili na Mloganzila.
Amesema ujenzi wa mradi wa kufua umeme katika Mto Rufiji ‘Stiegler’s Gorge’wenye uwezo wa kuzalisha MW 2,115, utaongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika nchini.
“Mradi huo utaongeza
upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika kwa ajili ya kukidhi
mahitaji ya viwanda na uwekezaji nchini ikiwemo na katika mkoa wa
Dodoma.
Waziri Mkuu amesema Serikali
itaendelea na utekelezaji wa mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara
na Uwekezaji (The Blue Print) utakaoanza Julai mosi mwaka huu.
Waziri Mkuu amesema anatarajia
kuwa kongamano hilo litawezesha kupatikana kwa wawekezaji mahiri kwa
maendeleo ya uchumi na wananchi wa Tanzania.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt.
Bilinith Mahenge alisema katika azma ya Selikali ya kujenga uchumi wa
viwanda wameandaa kongamano hilo ili kutangaza fursa zilizopo.
Alisema kaulimbiu ya kongamano
hilo ni ‘Dodoma Fursa Mpya Kiuchumi Tanzania, Wekeza Dodoma
Tukufanikishe’, inatanabaisha nafasi ya mkoa huo kwa sasa na baadaye.
Dkt. Mahenge alitaja baadhi ya
fursa za uwekezaji zilizopo mkoani Dodoma kuwa ni pamoja na uwepo wa
ardhi ya kutosha kwa ajili ya kilimo, viwanda na taasisi (afya, elimu).
0 comments:
Post a Comment