
****************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewatakaviongozi wote na watendaji wa Serikali kuanzia ngazi ya kijiji,
kata, tarafa, wilaya, mkoa hadi wizara kuwajibika ipasavyo na kudumisha
nidahmu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.
Amesema ili kufikia lengo na
dhamira ya kutekeleza Mpango na Bajeti ya Serikali ya 2019/2020 kwa
ufanisi, viongozi hao wanatakiwa waendelee kuwasisitiza wananchi
washiriki ipasavyo kulinda miundombinu inayojengwa kwa gharama kubwa na
Serikali.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
(Ijumaa, Juni 28) wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, Bungeni
jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Septemba tatu mwaka huu.
Pia, Waziri Mkuu amezitaka
mamlaka husika zishirikiane na wadau wengine katika kudhibiti uharibifu
wa mazingira kwa kukomesha ukataji hovyo wa misitu, uchafuzi wa bahari,
mito na maziwa na taka za plastiki ili kulinda mazingira asilia.
Akizungumzia kuhusu bajeti ya
Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Waziri Mkuu amesema Serikali
imepanga kutumia jumla ya sh. trilioni 33.11, kati yake sh. trilioni
20.86 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 63.
“Aidha, sh. trilioni 12.25, sawa na asilimia 37 ya bajeti yote
zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo
kuwasihi Watanzania pamoja na Washirika wa Maendeleo waiunge mkono
Serikali katika kutekeleza vipaumbele vilivyowekwa kwenye bajeti ya
mwaka 2019/2020 ili viweze kutoa mchango wa haraka katika maendeleo ya
uchumi na ya watu.
Wakati huo huo,Waziri Mkuu
amezungumzia kuhusu uboreshwaji wa daftari la kudumu la wapiga kura,
ambapo amesema kwa sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inakamilisha
maandalizi hayo ikiwa sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu
utakaofanyika mwakani.
“Uboreshaji huo, unatarajiwa
kuanza tarehe 18 Julai, 2019 katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro
ambapo litafanyika kwa muda wa siku 7 kwa kila kituo na kuendelea hadi
tarehe 5 Machi, 2020 litakapohitimishwa katika mkoa wa Dar es Salaam.”
Waziri Mkuu amesema uboreshaji
huo hautahusisha wapiga kura walioandikishwa mwaka 2015 isipokuwa
utawahusu wapiga kura wapya waliotimiza umri wa miaka 18 na kuendelea au
watakaotimiza umri huo ifikapo siku ya uchaguzi mkuu ujao.
Ametaja kundi lingine
litakalohusika na zoezi hilo kuwa ni pamoja na wale watakaoboresha
taarifa zao, kama waliohama jimbo au kata na kuhamia katika maeneo
mengine ya kiuchaguzi, waliopoteza au kadi zao kuharibika,
watakaorekebisha taarifa zao pamoja na kuwaondoa waliopoteza sifa kama
vile kufariki.
Hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito
kwa wananchi wote wenye sifa kutumia fursa hiyo kujitokeza kwa wingi
kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la
wapiga kura ili kutimiza haki yao ya kikatiba.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema
kuwa Novemba mwaka huu kutakuwa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambao
ni sehemu muhimu katika kuimarisha utawala bora na demokrasia ambayo
imeendelea kunawiri nchini. Amewataka wananchi wenye sifa kujitokeza
wakati utakapofika.
Amesema Serikali imeendelea
kutumia mbio za mwenge kuhamasisha wananchi washiriki uchaguzi huo
kupitia kaulimbiu isemayo “Maji ni haki ya kila mtu, tutunze vyanzo
vyake na tukumbuke kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”.
“Napenda kutumia fursa hii
kutoa wito kwa wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla hususan wale
wenye sifa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kupiga kura ili waweze
kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua au kuchaguliwa katika
uchaguzi huo.”
Kwa wananchi wenye nia ya
kugombea katika uchaguzi huo, Waziri Mkuu amesema ni lazima wajue
majukumu wanayoomba kwamba yanahitaji umakini mkubwa na uchapaji kazi
kwa sababu Serikali imewekeza miradi mingi kote nchini, hivyo
wanahitajika watu walio tayari kuhakikisha wanasimamia miradi hiyo ili
itoe matokeo yanayokusudiwa.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amesema Serikali itaendelea kuhakikisha uwepo wa mazingira salama
na tulivu kwa kipindi chote cha uchaguzi.
0 comments:
Post a Comment