Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai
ameliambia Bunge hilo leo Ijumaa Juni 28, 2019 kuwa amewandikia
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kumjulisha kuwa kiti cha ubunge
wa Singida Mashariki (Chadema) Tundu Lisu kipo wazi.
Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Mh.
Tundu Lissu, amevuliwa rasmi kiti hicho, baada ya kuvunja taratibu
mablimbali za Bunge ikiwemo kutohudhuria Mikutano na vikao vya bunge
bila kutoa taarifa.
Akiongea leo Juni 28, 2019 bungeni,
wakati wa kuhitimisha mkutano wa kumi na tano, kikao cha hamsini na tano
kilichoambatana na hoja ya kuahirisha bunge, Spika amesema, amemjulisha
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kujaza nafasi hiyo.
”Napenda kuwafahamisha waheshimiwa
wabunge kuwa kiti cha ubunge cha jimbo la Singida Mashariki kilichokuwa
kinashikiliwa na Mh. Tundu Lissu kipo wazi na nimemjulisha Mwewnyekiti
wa Tume ya Uchaguzi aendelee na taratibu za kukijaza”, amesema.
Ndugai amefafanua kuwa kutokana na Tundu
Lissu, kushindwa kutoa taarifa kwa spika kwa muda wote ambao hayupo
bungeni, pamoja na kutowasilisha tamko la mali zake anakuwa amevunja
sheria ya uchaguzi.
”Kifungu cha 37, kifungu kidogo cha 3 cha
sheria ya taifa ya uchaguzi sura ya 343, kinanitaka kumtaarifu
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi nini cha kufanya”.
Aidha spika ameongeza kuwa ni zaidi ya
mwaka mmoja umepita, ambapo Tundu Lissu amekuwa akionekana kwenye vyombo
mbalimbali vya habari katika nchi tofauti, huku akiwa hajafika bungeni
wala kutoa taarifa yoyote kwa spika au kupitia kwa uongozi wake kitu
ambacho ni kinyume na Katiba.
Ndugai amesema hajamfukuza Lissu bali
Katiba ndiyo imemuondoa mbunge huyo ambaye kikao chake cha mwisho cha
Bunge kilikuwa Septemba 7, 2017 ambapo mchana wa siku hiyo alipigwa
risasi zaidi ya 30 akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma.
Mara baada ya kushambuliwa, alipekewa
Hospitali ya Rufaa Dodoma kisha usiku huo huo alihamishiwa Hospitali ya
Nairobi nchini Kenya ambako alikaa hadi Januari 6 mwaka 2018
alikohamishiwa nchini Ubelgiji aliko mpaka sasa.
0 comments:
Post a Comment