Washirika wa maendeleo wakiwa katika
picha ya pamoja na watendaji Serikalini. Katikati waliokaa ni Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Emmanuel Kalobelo; kulia kwake
ni Ofisa Mradi kutoka AFD, Katell Rivolet na Mkurugenzi Mtendaji wa
Mamlaka ya Maji Jijini Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Anthony Sanga na
kushoto kwake ni Mkuu wa Msafara wa AFD, Claire Fargeaudou na Mratibu
mradi kutoka EIB, Raoul Pedrazzani.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji,
Mhandisi Emmanuel Kalobelo akisisitiza jambo wakati wa majadiliano ya
utekelezaji wa miradi ya maji ya LV WATSAN. Kulia kwake ni Mkurugenzi
Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Jijini Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Anthony
Sanga na Naibu Mkurugenzi, Idara ya Usambazaji Maji wa Wizara ya Maji,
Mhandisi William Christian.
Ujumbe wa washirika wa maendeleo ulitembelea maeneo mbalimbali ya mradi. Pichani ni sehemu ya eneo la Tiba ya Maji.Washiriki
wa mkutano wakikagua miundombinu ya tiba ya maji kwenye mradi wa Maji
wa Lamadi. Wa kwanza ni Mratibu mradi wa LV WATSAN kutoka EIB, Raoul
Pedrazzani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji
Jijini Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Anthony Sanga akizungumza jambo
wakati wa mkutano. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji,
Mhandisi Emmanuel Kalobelo. Kushoto kwake ni Naibu Mkurugenzi, Idara ya
Usambazaji Maji wa Wizara ya Maji, Mhandisi William Christian.
Muonekano wa baadhi ya maeneo ya mradi wa maji wa Lamadi ambao ulitembelewa na ujumbe wa washirika wa maendeleo.Ujumbe
wa washirika wa maendeleo wakiwa katika picha ya pamoja na Watendaji
kutoka Serikali kwenye eneo la chanzo cha maji cha maji mradi wa Lamadi.
………………….
Serikali imesema imeridhishwa na kasi ya
ujenzi wa mradi wa maji wa Lamadi uliopo Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu
ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 93.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Emmanuel Kalobelo alisema hayo hivi karibuni wakati wa ziara yake kwenye mradi huo.
Katika ziara hiyo Mhandisi Kalobelo
alifuatana na washirika wa maendeleo wanaowezesha utekelezaji wa miradi
ya maji kupitia Programu ya Uboreshaji wa Huduma ya Majisafi na Usafi wa
Mazingira ijulikanayo kama LV WATSAN ambao ni Benki ya Uwekezaji ya
Ulaya (EIB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD).
Mhandisi Kalobelo alisema amefarijika
kushuhudia hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa mradi na aliongeza kuwa hadi
kufikia Agosti mwaka huu utakuwa umekamilika kwani shughuli iliyopo kwa
sasa ni ya ufungaji wa pampu na baada ya hapo maji yataanza kutoka.
Kwa upande wake Mratibu mradi kutoka EIB,
Raoul Pedrazzani alisema miradi inayotekelezwa chini ya Programu ya LV
WATSAN imeonyesha mafanikio makubwa na aliipongeza Mamlaka ya Maji
Mwanza (MWAUWASA) ambayo inajukumu la kusimamia miradi hiyo kwa niaba ya
Wizara ya Maji kwa usimamizi mahiri wa utekelezaji wake.
Pedrazzani alisema EIB ina nia ya dhati
ya kupanua ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika siku zijazo kwani
imeridhishwa na namna ambavyo Serikali inatekeleza miradi maeneo
mbalimbali kote nchini.
Naye Afisa Miradi kutoka AFD, Clement
Kivegalo akizungumza kwa niaba ya ujumbe alioambatana nao, alisema
wameridhishwa na hatua ya utekelezaji wa mradi na kwamba AFD itaongeza
udhamini kadri itakavyohitajika kufanya hivyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Busega,
Tano Mwera ambaye alikuwa mwenyeji wa ugeni huo wilayani hapo, alisema
mradi unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa kwenye wilaya na hususan
katika mji wa Lamadi na alitoa wito kwa wawekezaji kujitokeza kwani maji
ya yhakika yamepatikana na kwamba miundombinu mingine ipo vizuri
ikiwemo barabara na umeme wa uhakika.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA,
Mhandisi Anthony Sanga akiuelezea mradi alisema unafadhiliwa na Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia mia moja kupitia mkopo
wa masharti nafuu kutoka EIB na AFD kwa gharama ya Shilingi Bilioni
12.83.
Mhandisi Sanga alisema mradi utazalisha
lita Milioni 3.3 za maji kwa siku ambayo ni mara mbili ya mahitaji ya
sasa ya wananchi wa Lamadi na maeneo jirani hasa ikizingatiwa kwamba
mradi umebuniwa kuhudumia wananchi zaidi ya 60,000.
Aliongeza kuwa hatua ya kwanza ya
maunganisho kwa wananchi; mradi utaunganisha kaya zipatazo 5000 na
aliwataka wananchi kuchangamkia mradi ili kujiletea maendeleo.
Kabla ya ziara hiyo, washirika hao wa
maendeleo walifanya mkutano Jijini Mwanza na watendaji kutoka Serikalini
kwa ajili ya majadiliano na tathmni ya hatua za zilizofikiwa kwenye
ujenzi wa miradi ya maji inayotekelezwa chini ya Program ya LV WATSAN.
0 comments:
Post a Comment