Na Mwandishi Wetu,
BEKI wa kati na kiungo mkabaji, Mbrazil Gerson Fraga Vieira amesaini
mkataba wa miaka miwili kujiunga na mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania
Bara, Simba SC.
Vieira mwenye umri wa miaka 26 ametambulishwa leo na Mwenyekiti wa
Kamati ya Usajili ya klabu, Zacharia Hans Poppe na anajiunga na Wekundu
wa Msimbazi akitokea klabu ya ATK ya India baada ya kumaliza mkataba
wake.
“Fraga ambaye amewahi kuwa nahodha wa timu ya Taifa ya wachezaji chini
ya miaka 17 ya Brazil iliyokuwa na wachezaji maarufu kama Neymar,
Philippe Coutinho, Casemiro na golikipa Alisson, pia alicheza timu ya
Taifa ya wachezaji chini ya miaka 20 na alicheza klabu kadhaa za Brazil
ikiwepo Grêmio amejiunga na klabu yetu akitokea ATK FC ya India,”imesema
taarifa ya Simba leo.
Gerson Fraga mzaliwa wa Porto Alegre
nchini Brazil, kisoka aliibukia timu ya vijana ya Gremio mwaka 2000
ambayo aliichezea hadi mwaka 2012 alipopandishwa timu ya wakubwa na
akadumu hadi 2016.
Lakini kwa sababu mbalimbali, akiwa Gremio alitiolewa kwa mkopo timu
mbalimbali zikiwemo Oeste (2012), Red Bull Brasil (2014), Atenas
(2014–2015), Red Bull Brasil (2015–2016) kabla ya kuuzwa moja kwa moja
Mumbai City ya India mwaka 2016.
Mwaka 2017 alihamia Atletico Tubarao alikocheza mechi 14 na kufunga bao
moja kabla ya kurejea Mumbai City alikocheza hadi mwaka jana akahamia
Renofa Yamaguchi ambako baada ya muda mfupi, akaondoka pia.
Vieira ambaye pia amechezea pia timu za taifa za vijana za Brazil chini
ya umri wa mkiaka 15 (U15) na U17, Renofa Yamaguchi alicheza mechi nne
tu akahamia ATK alikocheza mechi 13 na kufunga bao moja pia kabla ya
kuja kujaribu bahati yake Simba.
Pamoja na Viera, Simba SC iko mbioni kumsajili mshambuliaji Ryan Moon
kutoka Kaizer Chiefs ya kwao, Afrika Kusini ambaye naye amemaliza
mikataba na klabu yake.
Moon mwenye umri wa miaka 22, mzaliwa wa Pietermaritzburg,
KwaZulu-Natal, Afrika Kusini baada ya kufanya vizuri na timu ya
Maritzburg United aliyojiunga nayo akitoka kuzichezea Woodlands FC na
Pirates FC, alipandishwa timu ya wakubwa mwaka 2016.
Baada ya hapo alihamia Kaizer Chiefs mwaka 2016 ambako alidumu hadi
mwishoni mwa msimu alipoachwa na sasa anakuja kujaribu bahati yake Simba
SC.
Amewahi pia kuchezea timu ya taifa ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ kuanzia mwaka 2017 kwa mechi nane na kufunga bao moja tu.
Fraga anakuwa mchezaji mpya wa tano kusajiliwa na Simba msimu huu baada
ya kipa Beno Kakolanya kutoka Yanga, beki wa kati, Kennedy Wilson Juma
kutoka Singida United wote Watanzania, kiungo wa kimataifa wa Sudan,
Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman na mshambuliaji Mbrazil, Wilker
Henrique da Silva kutoka Bragantino ya Daraja la Nne nchini kwao.
0 comments:
Post a Comment