Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka amewaongoza mamia ya waombolezaji kutoka Mikoa ya Simiyu, Shinyanga,
Mwanza , Dar es Salaam na maeneo mengine nchini, katika mazishi ya aliyekuwa
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Marehemu Brigedia Jenerali Mstaafu, Dkt. Yohana
Daudi Balele, ambayo yamefanyika Mei 09, 2019 katika eneo la Malinoni
Mtaa wa Kidinda Mjini Bariadi.
Akizungumza na waombolezaji hao kabla
ya kuaga mwili wa Marehemu Dkt.Balele, Mtaka amesema mkoa wa Simiyu unatambua
mchango wa Marehemu katika jitihada za kuanzisha mkoa wa Simiyu na mapinduzi
makubwa aliyoyafanya katika Elimu na kuahidi kuweka alama yake katika mkoa
kumuenzi.
"Uongozi wa Mkoa kwa kutambua
mchango wa Marehemu Dkt.Balele katika kuanzisha mkoa huu na katika mapinduzi ya
Elimu aliyoyafanya wilayani Bariadi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, tunaweka
alama ya maisha yake kama kumbukumbu katika Shule ya Sekondari Majahida ambayo
itabadilishwa Jina kuwa Dkt.Balele Sekondari na Barabara moja katikati ya Mji
wa Bariadi itaitwa Barabara ya Dkt.Balele" alisema Mtaka.
Akisoma Wasifu wa Marehemu,
Kapteni Zaharani Masimba wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) amesema
marehemu amelitumikia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa zaidi ya miaka
32 na kutunikiwa medali mbalimbali, ikiwemo ya Vita, Kagera, miaka 20 ya JWTZ,
Miaka 40 ya JWTZ, Utumishi wa muda mrefu na Utumishi uliotukuka.
Naye mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo, Brigedia Jenerali, Robson Mboli Mwanjela
amesema, licha ya Marehemu kustaafu Jeshi, alitumia vizuri taaluma yake ya Udaktari
kuwasaidia watu mbalimbali na kuwataka wananchi wa Simiyu kuiga mema mengi
aliyoyafanya.
"Marehemu atakumbukwa daima kwa
mchango wake mkubwa alioutoa wakati wa utumishi wake jeshini na kwa Taifa
kwa ujumla, katika vyeo na madaraka mbalimbali aliyopewa wakati wa utumishi
wake na hata baada ya kustaafu; aidha atakumbukwa kwa umakini wake wa kutibu
binadamu na ufundishaji wanafunzi katika kada ya afya " alisema Brig. Jen.
Mwanjela.
Nao baadhi ya viongozi waliofanya
kazi na Marehemu Dkt. Balele wamemuelezea kuwa alikuwa mwaminifu, mchapakazi,
hodari na mwenye Upendo huku wakitoa wito kwa wananchi Mkoani Simiyu na hapa
nchini kwa ujumla kuyaenzi mema yake.
"Dkt.Balele alikuwa kiongozi
halisi alitumia uwezo na ushawishi wake kuwafanya watu wake wawe kama
anavyotamani wawe, alipenda sana Elimu alitaka watu wasome na pengine hata
zaidi yake, ndiye aliyehamasisha Wafanyabiashara kujenga Biashara Sekondari
hapa BARIADI, naomba wana Simiyu tumuenzi kwa kuwekeza katika elimu"
alisema Mbunge wa Bariadi, Mhe. Andrew Change
"Marehemu Dkt.Balele alikuwa
mdau mkubwa wa Elimu, katika kipindi chake alifanikiwa kuanzisha shule za
Sekondari 44 Wilaya ya Bariadi na Itilima ambayo pia kipindi hicho ilikuwa
sehemu ya Bariadi, lakini pia wakati wa mpango wa kuugawa mkoa wa Shinyanga alikuwa
na mchango mkubwa wa kuanzisha mkoa wa Simiyu na makao makuu kuwa Bariadi,
naomba tuendelee kuenzi mema yake" Baraka Konisaga, Mkuu wa Wilaya ya
Bariadi Mstaafu.
Marehemu Dkt.Balele ambaye alikuwa
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga mwaka 2006 hadi mwaka 2011 alizaliwa Desemba
28, 1948 katika Kijiji Cha Kasoli wilayani Bariadi na alipatwa na mauti Mei 02,
2019 katika Hospitali ya Lugalo jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa
matibabu.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment