METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, June 25, 2015

Mgombea urais alia kuombwa rushwa

Waziri wa mambo ya ndani, Mathias Chikawe

MMOJA wa makada 39 wa CCM waliojitosa kuwania kuteuliwa na chama hicho kuwania urais wa Tanzania baadaye mwaka huu, Boniface Ndembo jana alirudisha fomu huku akilalamikia hali ya rushwa, akisema ni mbaya na kwamba kuna baadhi ya maeneo watu walitishia kumkataa kumdhamini kama asingetoa fedha.

 Ndembo ambaye ni mmoja wa wagombea waliorejesha fomu jana, alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari. Mwingine aliyerudisha fomu ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe.

Chikawe alirejesha fomu kimya kimya. Aidha, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani naye alirejesha fomu . Ndembo alisema ni lazima ifike mahali suala la rushwa likome.

“Changamoto kubwa niliyoikuta mahali ambapo nimepita kama mgombea ni kuona jinsi ambavyo rushwa ilikuwa imetawala inatia hofu juu ya taifa inapokwenda,” alisema.

Alisema katika mchakato wake wa kuzunguka mikoani ameshuhudia na kuona watanzania na wananchi wa kawaida ni sehemu ya zao la rushwa.

“Kuna mahali unafika watu wanakataa kukudhamini kwa vile huna fedha za kuwapa wanakuambia waziwazi mbona fulani alitupa fedha na wewe lazima utoe…

“Sijajua kwa nini baadhi ya wagombea wanaandikwa sana kwenye magazeti wakati wa kutafuta wadhamini na wengine hawaandikwi, kuna wakati nimekumbana na hilo na nikapata changamoto,” alisema.

Alisema ifike mahali Watanzania wakaachana na rushwa hasa katika mambo yanayoligusa taifa kama kutafuta kiongozi wa nchi ili apatikane kiongozi asiyehusishwa na rushwa.

Alisema rushwa imekuwa adui mkubwa na nchi itaweza kupata kiongozi anayetokana na rushwa jambo ambalo ni hatari kubwa.

“Mahali pengine unaambiwa mbona fulani katoa kiasi fulani hiyo ni changamoto kubwa ya kupata viongozi wanaotokana na rushwa, waandishi wa habari wakiwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa jambo hilo litafanikiwa,” alisema.

Alisema waasisi wa taifa hili waliweka misingi mizuri na hakukuwa na matabaka ya mwenye nacho na asiye nacho, lakini misingi hiyo itaondolewa na watu wanaotafuta uongozi wa nchi kwa kutumia rushwa.

Alisema CCM ni chama chenye mfumo wa demokrasia bila kujali nyadhifa ma nafasi zao katika jamii.

Alisema ameweza kuzunguka mikoa 15 ikiwemo 12 ya Tanzania Bara na mikoa mitatu ya Zanzibar.

Alisema amefanikiwa kupata wadhamini 602. Naye Dk Kamani ambaye amekuwa Mwanachama wa nane kurudisha fomu ya kuomba kuchaguliwa na chama hicho akizungumza na waandishi wa habari mara alisema amezunguka jumla ya mikoa 17 huku 14 ikiwa ni ya Tanzania Bara na 3 ikiwa ni ya Tanzania Visiwani.

Alisema aliamua kutafuta wadhamini katika maeneo ya vijijini ili aweze kujua matatizo yanawakabili ili aweze kuyatatua pindi atakapopewa ridhaa ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema kama atapewa nafasi ya kuwa Rais atahakikisha anajikita katika kilimo kwani anaamni ndio kutapunguza pengo la mtu aliyenacho na yule ambaye hana.

‘’Sina cha kuficha mimi ni mtu safi na ninajiamini ndio maana hata kwa sasa ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Simiyu,nawaomba mniombee ili niwe Rais wenu nitatue matatizo ya Watanzania pamoja na suala la rushwa ambalo kwetu limekuwa janga kubwa’’alisema Dk Kamani.


Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com