Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka Wakuu wa za wilaya
zinazotekeleza ujenzi wa hospitali za wilaya kuhakikisha wanafanya kazi usiku
na mchana ili kuweza kukamilisha ujenzi huo kwa wakati ikiwa ni kutekeleza kwa
ufanisi maaagizo ya serikali juu ya ukamilishwaji wa ujenzi wa hospitali hizo.
Amesema kuwa hakurudhishwa na maendeleo ya ujenzi wa hospitali mbili za
Wilaya ya Nkasi pamoja na Wilaya ya Sumbawanga huku akipongeza ujenzi wa
hospitali ya Wilaya ya Kalambo kwa kupiga hatua tofauti na alivyodhania tangu
alipotembelea katika eneo hilo la ujenzi wiki tatu zilizopita.
“Katika Wilaya hii ya Kalambo hali ya Ujenzi nikilinganisha na
nilivyofika hapa tarehe 19 mwezi wa nne ilikuwa hali ni mbaya, kwasababu mvua
zilikuwa zinanyesha magari yalikuwa hayapiti kuja hapa kwa hali hiyo hata vifaa
mbalimbali vya ujenzi vilikuwa vinashindwa kufika kwa wakati, lakini hali ya
leo baada ya mvua kukatika, hakika waefanya kazi kubwa sana kwasababu hawa ndio
walikuwa na changamoto kubwa sana kuliko hospitali zile nyingine mbili, sasa
mhandisi fanya kazi hapa usiku na mchana na Mkurugenzi msimamie,” Alisisitiza.
Halikadhalika amewataka wakurugenzi kuhakikisha wanakamilisha malipo ya
mafundi ili wasiweze kuzembea na hatimae kujenga chini ya kiwango na kuongeza
kuwa wakati wakiendelea kufikia hatua ya usawa wa linta wahakikishe wanaanza
kununua vifaa kama milango, mbao kwaajili ya kenchi na mabati tayari kwaajili
ya kufikiria hatua ya uwezekaji kwani fedha sio tatizo katika kulifanikisha
hilo.
Mh. Wangabo ameyasema hayo alipotembelea hospitali za wilaya tatu ndani
ya siku moja kwa kuzunguka zaidi ya kilomita 450 ili kujionea maendeleo ya
ujenzi wa hospitali hizo zilizopo katika mkoa huo ikiwa ni utekelezaji wa agizo
la Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh.
Suleiman Jafo, kuwa kabla ya tarehe 14 majengo yote ya hospitali hizo
yanatakiwa kufikia usawa wa linta.
Aidha, Mh. Wangabo amewataka mafundi wote kuhakikisha hadi kufikia
tarehe 12 mwezi Mei wanafikia katika usawa wa linta ili kutekeleza agizo hilo
kwa wakati na kuwataka wakuu wa wilaya hao kuwafikisha mafundi watakaoshindwa
kufukia hatua hiyo katika kamati za ulinzi na usalama za wilaya ili waweze
kujieleza.
Mkoa wa Rukwa unatekeleza ujenzi wa hospitali tatu za Wilaya ambazo tayari
zimeshapatiwa shilingi Bilioni 1.5 kila Wilaya kwaajili ya ujezni wa majengo
saba ya hospitali hizo ambayo yanatakiwa kumaliza na kuanza kutumika ifikapo
tarehe 30 mwezi juni mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment