METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, June 25, 2015

Maofisa elimu wapewa somo

 Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi, Shukuru Kawambwa

SERIKALI imetoa jukumu zito kwa wakuu wa shule na maofisa elimu wa kata kusimamia kwa ukamilifu na kufuatilia shughuli za ufundishaji wa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu, kuwa zinatekelezwa.

Aidha, imewataka walimu kuongoza shule katika misingi ya utawala bora na kusimamia utekelezaji wa sera, kanuni na miongozo ya usimamizi na uendeshaji wa elimu nchini.


Hayo yalibainishwa jana na Kamishna wa Elimu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Eustella Bhalalusesa wakati akifungua mafunzo ya wawezeshaji wa ngazi ya Taifa, kuhusu kiongozi cha Mwalimu Mkuu pamoja na usimamizi wa ufundishaji wa kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) yaliyofanyika Bagamoyo mkoani Pwani.

Profesa Bhalalusesa alisema ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi nchini, ni lazima walimu wawe na uelewa wa kusimamia kanuni hizo za ufundishaji.

Alisema kutokana na ukuaji wa mfumo wa Sayansi na Teknolojia ni vema walimu kuendana na mabadiliko hayo ili kuweza kuboresha mfumo wa elimu hapa nchini. “Ni aibu kwa mtoto wa darasa la saba anamaliza shule hajui kusoma, kuandika wala kuhesabu.

Sasa hivi tuna changamoto kubwa kwani wazazi wanafikia hatua ya kusema ni bora mtoto akachunge ng’ombe kuliko kusoma na kwamba hata akienda shule atadumaa,” alisema Profesa Bhalalusesa.
Aliongeza kuwa tafiti zinaonesha mwanafunzi akifundsihwa kwa kutumia sauti anapata uelewa zaidi, hivyo ni muhimu walimu kufikiria kutumia mfumo huo.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (Adem), Dk Siston Masanja alisema wanaamini kuwa mafunzo wanayoyatoa kwa wakuu hao wa shule yatasaidia kukuza kiwango cha elimu.

Alisema zaidi ya bilioni 5.2 zimetumika kwa ajili ya kutoa mafunzo hayo, hivyo wanategemea wakuu wa shule wataimarisha usimamizi wa shule zao.

‘’Kupitia mafunzo haya, ni rai yangu kwa wawezeshaji wote wasitumie ukali na ubosi katika kuwafundisha walimu wakuu ili kuyafanya mafunzo haya kuwa bora na yenye matokeo chanya,’’ alisema Dk Masanja.

Katika mafunzo hayo, washiriki 170 kutoka katika Mikoa 17 ya Tanzania bara, ambao ni Maofisa elimu wa Mkoa, wilaya na Kata, wahasibu wa shule pamoja na wakaguzi walishiriki kupata mafunzo hayo.


Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com