Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila akisoma hotuba ya uzinduzi kabla ya kuzindua Soko la Madini Chunya.
Sehemu ya wananchi waliofika kushuhudia uzinduzi wa Soko la Madini Chunya wakifuatilia hotuba ya uzinduzi iliyokuwa inatolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila. (hayupo pichani).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Soko la Madini Chunya. Kulia ni Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula.
Na Greyson Mwase, Chunya
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila amezindua Soko la Madini
Chunya ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ya kutaka Wilaya ya Chunya
kuhakikisha imekamilisha na kuzindua soko la madini ndani ya kipindi cha siku
saba. Rais Magufuli alitoa agizo hilo tarehe 27 Aprili, 2019 wilayani Chunya
katika mkutano wake na wachimbaji na wachenjuaji wa madini.
Uzinduzi
huo ulishirikisha Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Mkuu wa
Wilaya ya Chunya, Mary-Prisca Mahundi,
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara ya
Madini, Issa Nchasi, Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Anthony Tarimo na
Kamishna Msaidizi- Uendelezaji wa Migodi kutoka Wizara ya Madini, Ali Ali.
Wengine
walioshiriki katika uzinduzi huo ni pamoja na Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara
ya Madini kutoka Tume ya Madini, Dk. Venance Mwase, wawakilishi wa wachimbaji
na wafanyabiashara wa madini, viongozi wa dini pamoja na vyombo vya habari.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi huo, Profesa Msanjila alisema kuwa, tangu kuingia madarakani
kwa Serikali ya Awamu ya Tano, imekuwa ikisisitiza dhamira yake ya kuhakikisha
Sekta ya Madini inakua, inanufaisha watanzania pamoja na kuchangia ukuaji wa
Pato la Taifa.
Akielezea
mafanikio ya Serikali kupitia Wizara ya Madini kwenye usimamizi wa rasilimali za madini, Profesa Msanjila
alisema kuwa, ili kuhakikisha kuwa
wananchi wote wananufahika na rasilimali za madini, Serikali ilitunga Sheria ya
Mamlaka ya Nchi Kuhusiana na Umiliki wa
Maliasili Namba 5 ya Mwaka 2017; Sheria ya Mapitio na Majadiliano Kuhusu
Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi Namba 6 ya mwaka 2017 pamoja
na kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini Sura ya 123.
Aliendelea
kueleza kuwa Serikali pia imefuta baadhi ya tozo ambazo zilikuwa kero kwa
wafanyabiashara wa madini hususan wachimbaji wadogo na kufafanua kuwa tozo hizo
kuwa ni pamoja na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) asilimia 18 na kodi ya zuio
ya asilimia tano kwa wachimbaji wadogo.
Alisema
kuwa, kuwekwa kwa mazingira mazuri ya kibiashara kwenye sekta ya madini pamoja
na kufuta kodi na tozo mbalimbali zinazofikia asilimia 23 kutaondoa utoroshwaji
wa madini na kusaidia wachimbaji wadogo kutambuliwa kupitia uanzishwaji wa
masoko ya madini.
Alieleza
manufaa mengine kuwa ni pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli
za wachimbaji wadogo na kuongeza wigo wa mapato ya nchi.
Katika
hatua nyingine, Profesa Msanjila aliwataka
wachimbaji wote wadogo na wafanyabiashara wa madini kuendelea kushirikiana na mamlaka mbalimbali za Serikali katika kutekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria, kanuni, taratibu na
miongozo mbalimbali inayotolewa na
Serikali.
Akielezea
manufaa ya soko jipya la madini Chunya, Profesa Msanjila alisema soko litaziba
mianya ambayo imekuwa chanzo cha utoroshwaji wa madini, ukwepaji kodi na hivyo
kusababisha biashara nzima ya madini kufanyika kiholela katika maeneo mengi ya
nchi.
Aliongeza
kuwa kuanzishwa kwa Soko la Madini Chunya kutawezesha na kurahisisha biashara
nzima ya madini na kuwa kiungo muhimu cha kuwakutanisha wachimbaji na
wafanyabiashara kwa lengo la kuuza na kununua madini.
Profesa
Msanjila aliendelea kufafanua manufaa mengine ya soko kuwa ni pamoja na kuwa
suluhisho la tatizo la kupunjwa na kudhulumiwa na kuondoa vitendo vya dhuluma ambavyo vimekuwa vikiwahusisha wafanyabiashara wa madini
wasiokuwa waaminifu kwa baadhi ya wachimbaji wadogo.
“Soko
hili litaondoa uwezekano wa
wanunuzi wa madini kuibiwa na wajanja
wachache wanaojifanya kuwa na madini
wakati hawana, nawasihi wanunuzi wa madini kulitumia soko kikamilifu ili
kuepuka udanganyifu na matapeli tu” alisema Profesa Msanjila.
Katika
hatua nyingine Profesa Msanjila aliupongeza uongozi wa Wilaya ya Chunya,
wafanyabiashara wa madini kwa kuhakikisha Soko la Madini Chunya limezinduliwa
ndani ya muda uliopangwa.
Wakati
huo huo akizungumzia hali ya uanzishwaji wa masoko ya madini nchini, Mwenyekiti
wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula alisema kuwa, hadi kufikia sasa masoko matano
ya madini yameshafunguliwa katika mikoa ya Geita, Singida, Kahama, Arusha –
Namanga na Chunya.
Aliongeza kuwa masoko mengine ya madini yanatarajiwa
kufunguliwa kabla ya tarehe 05 Mei, 2019 ikiwa ni pamoja na Soko la Madini ya
Dhahabu na Vito vya Thamani Ruvuma, Soko la Madini Shinyanga, Soko la Madini
Dodoma na Soko la Madini Mbeya.
Profesa Kikula alitaja masoko mengine ambayo
yanatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni kuwa ni pamoja na Soko la Madini ya Bati
(tin) na Soko la Madini ya Dhahabu
Handeni.
Alisisitiza kuwa mikoa mingine ipo katika
hatua za mwisho kukamilisha vigezo mbalimbali vikiwemo vya kiusalama na
miundombinu.
0 comments:
Post a Comment