Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akijibu swali bungeni leo tarehe 24 Aprili 2019 wakati wa mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali
imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha pembejeo za kilimo (mbegu,
mbolea, viuatilifu na zana za kilimo) zinapatikana kwa wakati na kwa bei nafuu.
Hatua hizo
ni pamoja na uagizaji wa pamoja, ruzuku, kufuta au kupunguza tozo na kodi
zinazochangia kuongezeka kwa bei ya pembejeo na kufanya tafiti katika mnyororo
wa thamani wa mazao.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) ameyasema hayo bungeni
Jijini Dodoma leo tarehe 24 Aprili 2019 wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo
la Ndanda Mhe Cecil David Mwambe aliyetaka kufahamu kwanini Pembejeo za
kilimo ni ghali sana, hivyo wakulima wengi hushindwa kununua na kusababisha kupata
mavuno haba na kama Serikali ipo tayari kupunguza au kuweka bei elekezi iliyo
nafuu kwa mkulima ili aweze kupata pembejeo za madawa, mbolea na zana za kilimo.
Alisema
kuwa Serikali ina utaratibu wa
kuweka bei elekezi ya mbolea kupitia Mfumo wa Ununuzi wa pamoja nchini kwa
mbolea za kupandia aina ya DAP na kukuzia aina ya Urea. Utaratibu huu unalenga
kuhakikisha upatikanaji wa mbolea kwa wakati na kwa bei nafuu.
Mhe Mgumba
aliongeza kuwa katika jitihada za
kuongeza uzalishaji na kipato cha mkulima, Serikali hununua na kusimamia uthibiti na usambazaji wa viuatilifu
vya kupambana na milipuko ya visumbufu vya mazao na mimea kama vile
kweleakwelea, viwavijeshi, viwavijeshi vamizi, panya, nzige wekundu na nzi wa
matunda.
Kadhalika, ili kumpunguzia mkulima harubu katika
uzalishaji na uongezaji thamani ya mazao, Serikali imeendelea kutoa mikopo
nafuu ya zana za kilimo kupitia Mfuko wa Taifa wa Pambejeo za Kilimo, Benki ya
Maendeleo ya Kilimo na Shirika la Maendeleo la Taifa.
Kwa upande
wa mbegu na viuatilifu, Mhe Mgumba alisema kuwa serikali inafanya utafiti wa kubaini gharama za
uzalishaji wa mbegu kwa kulinganisha na bei za mbegu zilizopo sasa ambao
utaiwezesha Serikali kuamua endapo kuna ulazima wa kuweka bei elekezi.
Aidha, Mhe Mgumba pamoja na hatua hizo, Serikali
inahamasisha ujenzi wa viwanda vya mbolea, viuatilifu, zana za kilimo na
uwekezaji katika mashamba ya mbegu ili kupunguza gharama za pembejeo hizo.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment