Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameendelea kuwasisitiza
wafugaji kuendelea kufuga kisasa baada ya biashara ya mifugo katika minada ya
awali na ule wa mpakani na nchi ya Zambia katika Kijiji cha Kasesya kuwaingizia
wafugaji hao shilingi 18,890,665,000 kutokana na kuuza ng’ombe 35,532, mbuzi
2,307 na kondoo 631.
Ameyasema hayo alipokuwa akiwasilisha utekelezaji wa Ilani ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) kwenye kiako cha Kamati ya Siasa ya Mkoa kwa kipindi cha mwezi
July hadi Disemba, 2018 na kuhudhuriwa na wataalamu kutoka Halmashauri, Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa pamoja na wakuu wa Taasisi na Mamlaka za Serikali zilizopo
katika Mkoa.
Aidha, amepongeza ongezeko la makusanyo yay a vibali vya kusafirishia
mifugo kwa silimia 33.6 kwa mwaka wa fedha 2018/2019, mafanikio ambayo
yametokana na udhibiti wa pamoja wa Uongozi wa Mkoa pamoja na Wizara ya Mifugo
na Uvuvi.
“Mapato ya Serikali Kuu yanayotarajiwa kukusanywa kwa Mwaka wa Fedha
2018/ 2019 kutokana na ushuru wa vibali vya kusafirisha Mifugo ni Shilingi
80,000,000/=. Hadi kufikia tarehe 31 Desemba, 2018 Mapato ya Serikali Kuu yaliyopatikana
kutokana na ushuru wa vibali vya kusafirisha Mifugo ni Shilingi 120,
44,500/=. Makusanyo hayo ni zaidi ya Shilingi 40,444,500/= ya lengo la
Mwaka,”Alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa Reiner Lukala
amewapongeza wataalamu wanaoendelea kuitekeleza Ilani ya CCM kwa umakini pamoja
na ushirikiano wanaoutoa katika kupokea ushauri na kuufanyia kazi pale
inapostahili.
“Kwa wataalamu nichukue fursa hii kuwashukuru kwa jinsi mnavyotumia
wakati wenu, elimu yenu, ujuzi wenu na muda wenu kwa kuendelea kufanya kazi
kubwa ya utekelezaji wa Ilani, Sura ya 8 ya Ilani ya CCM ya Mwaka 2015
inatuelekeza sisi Chama cha Mapinduzi kuwasimamia ninyi kuona mnafanya nini,
lakini kwa niaba ya CCM nichukue fursa hii kuwapongeza sana kwamba mpaka wakati
huu tunaenda vizuri,” Alisema.
Katika kikao hicho cha kuwasilisha utekelezaji wa Ilani ya Chama cha
Mapinduzi Mkuu wa mkoa wa Rukwa alipewa cheti cha kutambuliwa juhudi zake za
kuhakikisha anatekeleza ilani hiyo hatua kwa hatua na kwa wakati kupitia ofisi yake
ya Mkoa pamoja na kuzisimamia kikamilifu halmashauri nne za mkoa huo.
0 comments:
Post a Comment