Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo amemtaka Mkurugenzi wa
halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kusimamia kwa karibu, umakini na
kuongeza kasi ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya sumbawanga baada ya kuona
kusuasua kwa ujenzi huo tangu kuanza kwake tarehe 19 Januari, 2019 ambapo
wananchi walijitokeza kuchimba misingi ya majengo saba ya hospitali hiyo.
Amesema kuwa muda mwingi umepita tangu kuanza kwa ujenzi huo na hadi
sasa ilistahili uwe umefikia hatua ya lenta na matokeo yake bado ipo kwenye
hatua ya jamvi pamoja na changamoto zilizokuwepo na kuongeza kuwa hali hiyo
inawakatisha tamaa wananchi kwa kuona jengo halipandi tangu kuanza kushiriki
kwao kwenye ujenzi huu na kutahadharisha kuwa kwa sasa hakuna sababu ya
kusuasua katika ujenzi huo.
“Kuna haja kwa halmashauri kusimamia ujenzi huu kwa karibu kuanzia sasa
hivi kasi iongezeke mara mbili hata tatu kwa ile iliyokuwepo kwasababu kuapanga
matofali kwenda juu hata siku mbili ytatu unafika kwenye lenta lakini kutoka
kule kwenye msingi kunahitaji uangalifu na kupanga vizuri zaidi, kwahiyo
Mkurugenzi narudia tena simamia vizuri ujenzi wa hapa na kwa ukaribu zaidi,”
Alisisitiza.
Ameyasema hayo alipotembelea eneo la ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya
Sumbawanga inayojengwa katika Kijiji cha Mtowisa, Kata ya Mtowisa, bonde la
ziwa Rukwa na kuwataka mafunzi wote waliokabidhiwa kujenga majengo saba ya
hospitali hiyo kuhakikisha wanafikia ngazi ya lenta ifikapo tarehe 10 Mei, 2019
na kuongeza kuwa asiyefikia hatua hiyo atawajibishwa.
Wakati akisoma taarifa ya ujenzi wa hospitali hiyo Mganga Mkuu wa Wilaya
ya Sumbawanga Dkt. Fani Musa aliwashukuru wananchi kwa kujitolea kwao kwa kazi
za songambele zilizookoa shilingi 18,600,200 ikijumuisha kazi za kuchimba
misingi ya majengo na mtaro wa kupeleka maji eneo la ujenzi, kusogeza tofali na
ujazaji wa kifusi kwenye majengo hayo.
“Kwa ujumla kazi inaenda vizuri kwa mujibu wa ratiba ya kazi na
tunatarajia kuikamilisha kwa wakati kama ilivyoelekezwa. Halmashauri inahitaji
ushirikiano wa viongozi wote uendelee kama sasa ili kufikia mafanikio na
kukamilisha ujenzi huu wa hospitali kwa muda uliopangwa,”Alisema
Ili kukamilisha ujenzi wa majengo saba ya hospitali hiyo ambayo ni
majengo ya Utawala, Kufulia, Dawa, OPD, Maabara, Mionzi na Wazazi ni matofali
84,000 yanahitaji ambapo hadi sasa matofali 70,666 yameshafyatuliwa huku
shilingi milioni 496 zikiwa zimeshatumika.
0 comments:
Post a Comment