Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye wa kikao cha kazi cha maandalizi ya uandaaji wa Mpango mkakati wa pili wa kuendeleza uzalishaji wa zao la Mpunga nchini (National Rice Development Stratergy II - NRDS II) kilichofanyika katika Hoteli ya Edema Mkoani Morogoro, leo tarehe 24 Aprili 2019.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao cha kazi cha maandalizi ya uandaaji wa Mpango mkakati wa pili wa kuendeleza uzalishaji wa zao la Mpunga nchini (National Rice Development Stratergy II - NRDS II) kilichofanyika katika Hoteli ya Edema Mkoani Morogoro, leo tarehe 24 Aprili 2019.
Na Mathias Canal, Wizara ya
Kilimo-Morogoro
Kikosi Kazi cha CARD kwa kushirikiana na Mshauri wa
CARD, kimeagizwa kuandaa rasimu ya awali ya mkakati wa kuendeleza zao la mpunga
nchini mapema kabla ya June, 2019.
Agizo hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe leo tarehe 24 Aprili 2019 wakati wa
kikao cha kazi cha maandalizi ya uandaaji wa Mpango mkakati wa pili wa
kuendeleza uzalishaji wa zao la Mpunga nchini (National
Rice Development Stratergy II - NRDS II) kilichofanyika katika
Hoteli ya Edema Mkoani Morogoro.
Alisema kuwa ili kikamilishe
hiyo kazi lazima kuwe na takwimu sahihi zinazoonyesha hali halisi ya uzalishaji
wa mpunga nchini. ” Ni lazima kutoa takwimu zenye uhakika zitakazowezesha
mpango wa pili wa kuendeleza zao la mpunga kukamilika ipasavyo, Timizeni wajibu wenu mliopewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, inayoongozwa na Rais wetu mpendwa, Mhe Dr. John Pombe Joseph Magufuli”
Alikaririwa Mhandisi Mtigumwe
Alisema kuwa mara baada ya kukamilika kwa takwimu
hizo kikosi kazi hicho kitaanza kuandika rasimu ya mpango mkakati wa kuendeleza
zao la mpunga, awamu ya pili kwa kuzingatia kuwa CARD wameazimia kuongeza
uzalishaji mara mbili zaidi hivyo Tanzania inapaswa kuzalisha mara mbili zaidi
ya mwaka jana.
Alilitaja lengo kuu la Mpango Mkakati wa Tanzania
katika uzalishaji wa zao la Mpunga nchini, kuwa litakuwa ni kuzalisha
kutoka tani 2,219,628 za
sasa na kufikia tani 4,500,000 ifikapo mwaka 2030.
Mhandisi Mtigumwe alisema kuwa Mpango mkakati wa
kuendeleza zao la Mpunga unaandaliwa kwa kushirikiana na "Coallition
for African Rice Development" (CARD), ambapo makao makuu yake
yako Nairobi, nchini KENYA. Tanzania ni moja kati ya chi 32 ambazo ni
wanachama.
Pamoja na CARD kumaliza kipindi cha awamu ya
kwanza, mwaka 2018, nchi wanachama pamoja na wafadhili walikutana Octoba 2018
huko Tokyo, Japan ambapo walifanya tathmini ya awamu ya kwanza na ilionyesha
kuwa lengo lilifikiwa.
Aidha, walikubaliana kuanzisha awamu ya pili ya
CARD, kuanzia 2018 hadi 2030. Awamu hii inatarajiwa kuzinduliwa nchini Japan,
mwezi wa Agosti, 2019. Moja ya jambo muhimu na linalozingatiwa ili kila nchi
ipate nafasi ya kupata miradi itakayonufaika na CARD, ni kuwa na Mpango Mkakati
wa Kuendeleza zao la Mpunga Awamu ya Pili (2018-2030). Lengo kuu la CARD, awamu
ya pili ni kuongeza uzalishaji wa mpunga kutoka tani 28 milioni (zilizofikiwa
katika awamu ya kwanza mwaka 2018) hadi tani 56 milioni mwaka 2030 kwa nchi
zote wanachama.
Mtigumwe alisema kuwa kama ilivyofanyika kwa nchi
nyingine, na kwa kuzingatia kwamba zao la
mpunga ni mojawapo ya zao muhimu la chakula na biashara linalozalishwa
takribani mikoa yote hapa nchini, mwaka 2008
Wizara ya Kilimo iliandaa pia Mpango Mkakati wa Kuendeleza zao la Mpunga (NRDS
I). Mpango huo ulikuwa ni wa miaka 10 na ulikamilika
mwaka 2018 ambapo ulitoa matokeo chanya ikiwemo kuongezeka kwa uzalishaji wa
mpunga kutoka tani 899,000 mwaka 2008 hadi tani
2,219,628 mwaka 2018.
CARD ni
Muungano wa Wabia ambao hupokea maandiko mbalimbali ya miradi ya uzalishaji na
usindikaji wa mpunga na kuyatafutia fedha kwa ajili ya
utekelezaji, na huongozwa na Sekretariati ya CARD, iliyoundwa na Wabia
wanachama. Hadi sasa kuna Wabia 23. Miongoni mwa Wabia hao, kama alivyokwishawataja
Mkurugenzi ni JICA, Benki Kuu ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika na
wengineo.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment