Na WAMJW - DOM
Hospitali ya
Benjamin Mkapa imefanikiwa kupandikiza Figo jumla ya Wagonjwa saba tangu
ilipoanza kufanya huduma hiyo kwa kushirikiana na Madaktari kutoka shirika la
afya la Tokushukai lilopo nchi ya Japan.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakati
alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za kibingwa za magonjwa ya
Figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma.
Dkt. Ndugulile
amesema kuwa Idadi ya wagonjwa waliokwishapandikizwa figo hapa nchini ni 43,
ambapo 38 wamepatiwa huduma hiyo kwenye hospitali ya Taifa Muhimbili na
wagonjwa watano(5) hospitali ya Benjamin Mkapa
"Hivi navyoongea tayari mgonjwa mmoja amekwishapandikizwa
figo na ameshatoka salama, yupo anaendelea kuangaliwa, lakini wana mpango wa
kuwafanyia wengine wawili tutapokuwa tumekamilisha hili tutakuwa na wagonjwa
saba ambao wamefanyiwa hospitali hii" alisema Dkt. Ndugulile.
Dkt. Ndugulile aliendelea kusema kuwa, Serikali
imelenga kuhakikisha kwamba inawajengea uwezo Wataalamu wa ndani kufanya
upasuaji wa kibingwa ili waweze
kuwahudumia Watanzania bila msaada kutoka Wataalamu wa nje.
"lengo na kusudio ni kuhakikisha kwamba tunajenga
uwezo wa ndani wa kuweza kufanya upasuaji huu" Alisema Dkt. Ndugulile
Dkt. Ndugulile amesema kuwa Serikali imeokoa zaidi ya
kiasi cha shilingi bilioni 4.2 ambacho kingetumika katika matibabu ya wagonjwa
80 mpaka 100 ambao wangepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
“Wagonjwa waliokwishapandikizwa figo hapa nchini ni
42, kama tungewapeleka wagonjwa nje ya
nchi ingegharimu serikali kiasi cha shilingi bilioni 4.2 kwa idadi hiyo ya
wagonjwa. 80 mpaka 100, wakati huduma
hii hapa nchini inagharimu kiasi cha shilingi milioni 21 kwa kila mgonjwa.”
alisema Dkt. Ndugulile
Aidha, Dkt. Ndugulile amewashukuru Wataalamu kutoka
shirika la Tokushukai kutoka nchi ya Japan kwa kujitoa na kuja kuwajengea uwezo
Wataalamu wa ndani hali iliyosaidia kupunguza kiasi kikubwa cha fedha ambacho
hutumika kwa ajili ya matibabu kwa wagonjwa wanaoenda kutibiwa nje.
"Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania nimepita
kuwashukuru na kuwapongeza, kwa sababu
badala ya kutusaidia sisi samaki, wenzetu wa Japan wameamua kutupatia sisi
mishipi na kutufundisha jinsi ya kujua naamini ujuzi huu utatusaidia sana
" alisema Dkt. Ndugulile.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment