
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Nishati na Madini wakiwasikiliza Wafanyabiashara wa Madini
katika Soko dogo la Madini Katoro wakati kamati hiyo ilipotembelea soko
hilo.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mariam Mzuzuri (kushoto)
akifuatilia hoja zilizokuwa zikitolewa na Wafanyabiashara wa Soko la
Madini Katoro. Katikati ni Mjumbe wa Kamati hiyo Fred Mwakajoka na kulia
ni Katibu wa Kamati hiyo Felister Mgonja.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus
Nyongo akifuatilia jambo wakati Kamati ya Bunge ikiwasikiliza
wafanyabishara wa madini , kamati hiyo ilipotembelea soko la madini.
Kulia ni Mjumbe wa Kamati hiyo Mariam Msabaha na Kushoto ni Afisa
Madini Mkazi Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus
Nyongo akizungumza jambo na wafanyabiashara wa soko la Madini Katoro
wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
…………………..
Wafanyabiashara wa Madini katika
Soko Dogo la Madini Katoro wameiomba Serikali iwaruhusu kuwa na
Wasaidizi watakaowasaidia kununua madini maeneo yenye mialo ya
uchenjuaji na kuwauzia kwenye vituo vya ununuzi.
Wafanyabiashara hao wametoa ombi
hilo wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini
ilipotembelea soko hilo kwa lengo la kujifunza na kuangalia namna
masoko ya madini yanavyoendeshwa.
Akitoa ufafanuzi zaidi kuhusu
suala hilo, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amesema kuwa,
Sheria na Kanuni za biashara ya madini zinaelekeza kuwa shughuli za
uuzaji na ununuzi wa madini zinapaswa kufanyika kwenye vituo maalum vya
manunuzi hivyo suala la kuwa na wasaidizi kwenye mialo wa kuwauzia
wafanyabiashara hao linakinzana na Sheria ya Madini na Kanuni za madini
kwenye masoko.
‘’ Kamati ndiyo inaishauri
Serikali, ndiyo Bunge na Wawakilishi wa wananchi. Tutaendelea kutatua
changamoto tunazokutana nazo kwenye masoko. Sote tunajua Masoko ni
Mapya, Sheria Mpya, Kanuni Mpya, hivyo tutaendelea kutatua changamoto
hizo yakiwemo masuala ya vifaa na watumishi,’’ amesema Naibu Waziri
Nyongo.
Aidha, Naibu Waziri Nyongo
amewataka wafanyabiashara wa madini na wachimbaji kuyatumia masoko ya
madini na kueleza kuwa, kufanya biashara ya madini nje ya masoko ni
kujiweka kwenye matatizo. Pia, amewasisitiza kuhusu matumizi sahihi na
salama ya zebaki na kueleza kuwa, serikali itaendelea kuangalia njia
mbadala za teknolojia ili kuweza kuachana na matumizi ya zebaki.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mariam Mzuzuri
amewataka wafanyabiashara hao kuendelea kufanya shughuli zao kwa kufuata
sheria na taratibu wakati Serikali na Kamati zikiangalia namna ya
kuzifanyia kazi changamoto zilizowasilishwa kwao.
‘’ Kwa kuwa masoko haya yanafanya
kazi kwa mujibu wa Sheria ni vyema suala hili mtuachie kwanza sisi na
serikali ili tuliangalie,’’ amesema Mzuzuri. Kufuatia hali hiyo, Mzuzuri
ameitaka wizara kuendelea kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara na
wachimbaji wa madini ili wajue namna ya kuyatumia masoko ya madini na
kujua mwenendo mzima wa shughuli za madini na biashara ya madini
inavyofanyika.
Katika hatua nyingine, kamati
imeitaka Serikali kuhakikisha suala la Ulinzi kwenye masoko ya Madini
halisubiri michakato bali linatakiwa kufanyiwa kazi haraka kutokana na
rasilimali zilizopo katika masoko hayo.
Makamu Mwenyekiti amesema hayo
kufuatia ombi la kuimarishwa kwa Ulinzi katika Soko la Katoro
lililotolewa na Wafanyabiashara wa Madini sokoni hapo wakati wa ziara
yake mkoani Geita.
Naye, Mjumbe wa Kamati hiyo Fred
Mwakajoka ametaka taasisi zote za serikali zinazoshirikiana na Tume ya
Madini kuendesha masoko hayo ziwepo katika masoko hayo ili kurahisisha
utendaji wa majukumu ya masoko .
Baada ya kutembelea soko la
Katoro, Kamati hiyo pia imetembelea Soko la Madini Kahama na baadaye
itatembelea Nzega. Ziara ya kamati kutembelea masoko imefanywa na kamati
hiyo baada ya kutembelea Soko Kuu la Madini Geita na Maonesho ya
Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanayoendelea mkoani
Geita.
0 comments:
Post a Comment